.

.

.

.

Thursday, October 16, 2008

YANGA YAZIDI KUPETA

Golikipa mzungu wa YANGA

WAKATI Yanga ikiwavurumisha wasaga unga, Azam FC mabao 3-1, mshambuliaji wake, Boniface Ambani amevunja rekodi ya mabao msimu uliopita kwa kupachika mabao 12.
Mike Katende wa Kagera Sugar, aliweka rekodi ya mabao mengi msimu uliopita, alifunga mabao 11 wakati Ambani amefunga mabao hayo katika mechi nane.
Mkenya huyo aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa nchini India, anawania kiatu cha dhahabu na kitita cha Shilingi milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo, Vodacom.
Kipigo hicho licha ya kuzidi kuiweka kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom ikiwa na pointi 21, pia kimeweza kuwarejeshea faraja mashabiki wa Yanga ambao wiki jana waliduwazwa na kipigo cha kwanza msimu huu mikononi mwa Kagera Sugar ya Bukoba.
Ambani alianza mapema kupiga hodi langoni mwa Azam FC dakika ya 11 ya mchezo huo akiunganisha pasi ya kiungo Abdi Kassim aliyerejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Muda mfupi baadaye, Ambani tena aliipatia timu yake bao la pili kwa kichwa kutokana na mpira wa krosi uliorushwa na beki Shadrack Nsajigwa.
Azam, kwa upande wao walitimiza usemi wa ngoma ya kitoto haikeshi kwa kuanza mchezo kwa kasi ya aina yake na kutawala kwa dakika 10 za mwanzo, lakini Yanga wakabadilika ghafla na kucheza mchezo wa kasi uliowawezesha kuandika mabao hayo mawili ya haraka.
Azam walianza tena kipindi cha pili kwa kasi ile ile na kufanikiwa kupachika bao sekunde 25 tu kupitia kwa Shaaban Kisiga aliyewalamba chenga mabeki na kipa Mzungu Obren Cirkovic akiuma vidole.
Kisiga aliiingia dimbani akitokea benchi na kuchukua nafasi ya mshambuliaji tishio, Yahaya Tumbo na mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa Azam.
Wasaga nafaka hao walipata pigo katika dakika ya 65 baada ya beki wao, mzoefu Said Sued kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Jerry Tegete wa Yanga ambao walikamilisha furaha kwa bao la tatu la kiungo Castory Mumbala, dakika ya 87.
Katika mchezo huo, Dusan Kondic alimtoa Ambani na kumwingiza Gaudence Mwaikimba, ambaye hajacheza soka kwa mpira mrefu.

No comments:

Post a Comment