.

.

.

.

Tuesday, November 18, 2008

BASIL PESAMBILI MRAMBA KUPANDISHWA KIZIMBANI

Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni Mbunge wa Rombo Mhe. Basil Pesambili Mramba anatarajiwa kufikishwa Mahakamani wakati wowote kuanzia sasa imefahamika. Waziri huyo ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za juu tangu utawala wa awamu ya kwanza na kushika nafasi ya uwaziri katika awamu ya tatu na awamu ya nne hadi pale alipotemwa katika mabadiliko ya Mawaziri mapema mwaka huu.
Mhe. Mramba anatarajiwa kufikishwa mahakamani kutokana na makosa mbalimbali ya yanayohusiana na utendaji wake wa kazi akiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na inawezekana pia kutokana na nafasi aliyowahi kushirikia ya Wizara ya Miundo Mbinu. Wachunguzi wengine wanaelezea pia Waziri mwingine wa zamani wa serikali ya Rais Mkapa Bw. Daniel Yona naye ajiandae kukutana na kibano cha sheria.
Endapo Bw. Mramba atafikishwa mahakamani kama ilivyotarajiwa atakuwa ni waziri mwingine wa serikali ya Mkapa kupanda kizimbani. Huko nyuma Bw. Nalaila Kiula aliyekuwa Waziri wa katika mhula wa kwanza wa utawala wa Rais Mkapa alijikuta akipandishwa kizimbani kufuatia mashtaka ya ufujaji wa mali ya umma yenye thamani ya zaidi ya bilioni 3 na kukutwa na hatia hata hivyo hukumu yake ilitupiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa.
Kesi dhidi ya Mramba inatarajiwa kuletwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kufuatia uchunguzi wake wa msamaha wa madeni ya Alex Stewart na pia malipo ya mabilioni ya shilingi yaliyofanyika miezi michache (na wakati mwingine wiki chache) kabla ya kikomo cha muhula wa pili wa utawala wa Rais Mkapa.
Chanzo chetu katika uchunguzi huo kimesema kuwa "Bw. Mramba akiwa Waziri wa Fedha ndipo tunaweza kuona malipo ya kushangaza na miradi ya ajabu ikiibuka nayo ikihusisha Benki Kuu." Chanzo chetu hicho cha kuaminika chenye ujuzi wa maendeleo ya uchunguzi huo kimesema kuwa "kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, serikali ya Tanzania chini ya Rais Mkapa iliingia na kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo ununuzi wa Rada, Ndege ya Jeti ya Rais (Mramba alinukuliwa kusema kuwa "hata ikibidi Watanzania wale majani ndege ya itanunuliwa"), wizi kutoka Akaunti ya EPA (ambapo watu zaidi ya 20 wameshafikishwa mahakamani), malipo kwa makampuni ya Mwananchi Gold, Deep Green Finance, Meremeta na kuongezewa muda kwa mkataba wa kampuni ya Makontena ya TICTS".
Chanzo hicho kimesema kuwa "kinyume na mawazo ya watu wengi fedha hizi nyingi hazikwenda kwenye uchaguzi wa CCM bali zilikwenda kwenye mifuko ya watu wachache katika utawala wa serikali ya Mkapa na sasa zimehifadhiwa kwenye akaunti mbalimbali duniani hasa kwenye nchi zenye sheria zinazosaidia watu kuficha fedha zao kama Uswisi, Cayman Islands, Bahamas, na Isle of Man".
Katika mazungumzo chanzo hicho kimefafanua zaidi kuwa "kuna kiasi ambacho kilitumika katika kampeni lakini kile kikubwa kimeenda mifukoni mwa watu. Hata zile fedha za "vijisenti" vya Mhe. Chenge ni sehemu ya fedha hizo ikiwa ni malipo kwake kama Mwanasheria Mkuu kuweza kufanikisha madili yote yale na ili kumuweka katika kujua akapewa nafasi ya kugombea Ubunge ili baadaye awekwe ndani ya Baraza la Mawaziri na hivyo kuwa 'inside man' wa Mkapa katika serikali ya Kikwete".
Alipoulizwa kama kuna watumishi wengine kutoka serikali ya Rais Mkapa ambao wanakabiliwa na mkono wa sheria chanzo hicho kilisema kuwa "ingekuwa hatuna kinga ya Rais, tungemsimamisha Mkapa mwenyewe kizimbani lakini katika hili hatuna msalie mtume kwani tutawakusanyika jamaa zake hadi wa mwisho wao"!


No comments:

Post a Comment