.

.

.

.

Thursday, November 27, 2008

MANJI AUGUA GHAFLA KWA MARA YA PILI


MFADHILI mkuu wa Yanga, Yusuf Manji jana alilazimika kukimbizwa nchini Kenya kwa matibabu zaidi baada ya kuugua ghafla kwa mara nyingine.
Hii ni mara ya pili kwa mfadhili huyo wa Yanga kukimbizwa hospitali Nairobi kwa matibabu zaidi, mapema mwezi uliopita ilielezwa kuwa alipatwa na malaria kali na kukimbizwa hospitali ya Aga Khan na baadaye Nairobi, Kenya.
Hali kama hiyo ilimjia mfadhili huyo wa Yanga siku chache baada ya timu yake kuichapa Simba bao 1-0, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania.
Awali taarifa za kuugua kwa mfadhili huyo zilisambaa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kwa kile kilichodaiwa kuwa alikunywa sumu kujaribu kujiua.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata na kudhibitishwa na baadhi ya madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo zilisema kuwa Manji alifikishwa hospitalini hapo juzi akiwa na hali mbaya na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Kwa mujibu wa chanzo cha habari hicho baada ya kufikishwa hospitalini hapo, moja kwa moja alipelekwa ICU akiwa hajitambui na asubuhi ya jana alisafirishwa kwenda Kenya kwa matibabu.
Habari zaidi zilisema kuwa mfadhili huyo alisafirishwa kwenda Kenya akiwa hajitambui baada ya kuchomwa sindano ya usingizi kutokana na kugoma kupelekwa huko akitaka atibiwe nchini.
“Ndugu zake baada ya kuona hali yake ni mbaya walimshahuri kumpeleka nchini Kenya lakini alikataa nao wakaona jambo la maana ni kumdunga sindano ya usingizi kisha kumsafirisha bila kujijua na hivi tunavyoongea ameshafikishwa Hospitali ya Aga Khan ya Kenya kwa matibabu,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa mfadhili huyo amejiua kwa kunywa sumu, Mwananchi ilifika hospitalini hapo ili kuthibitisha tetesi hizo lakini ilithibitishiwa kuwa alifika hapo juzi kutokana na magonjwa mengine ambayo hata hivyo vyanzo mbalimbali havikuwa tayari kuyataja kwa madai kuwa si wasemaji wa hospitali hiyo.
Mwananchi iliyokuwa inafuatilia, ilifika hospitalini hapo hadi chumba namba 52 kilichopo ghorofa ya tatu ilichoelezwa kuwa Manji amelazwa lakini hata hivyo baada ya kufuatilia ilikuta katika kitanda hicho amelazwa mwanamke aliyefahamika kwa jina Joyce Silikani na huku Manji akiwa tayari keshasafirishwa.
Baadaye gazeti hili lilizungumza moja kwa moja na Manji ambaye alisema anaendelea vizuri japokuwa sauti yake ilikuwa ikitoka kwa tabu.
“Niko nje ya nchi na naendelea vizuri,” alisema Manji kwa kifupi

No comments:

Post a Comment