.

.

.

.

Saturday, November 15, 2008

MWANAFUNZI AJINYONGA

Mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari ya Imezu Wilaya ya Mbeya Vijijini, Ambrosi Mwantambo (23), amejiua kwa kujinyonga kwa kamba kwa kile kinachodaiwa ni mshtuko uliotokana na kifo cha Mbunge wa Mbeya Vijijini, Richard Nyaulawa. Taarifa kutoka kijijini hapo zinadai mwanafunzi huyo alifikia hatua hiyo baada ya kupata taarifa kuwa Nyaulawa aliyekuwa akimlipia ada ya shule, amefariki na hivyo kukosa tumaini la kuendelea na masomo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen alithibitisha kutokea kwa tukio la mwanafunzi huyo kujinyonga, akisema lilitokea juzi katika Kijiji cha Inyala majira ya saa 3:00 asubuhi. Kamanda alidai mwanafunzi huyo alijinyonga kwa kutumia kamba ya mti aina ya Mtiyombo. Hata hivyo, alisema sababu za mwanafunzi huyo kujinyonga hazijajulikana kutokana na kutoacha ujumbe wowote kueleza sababu za kujiua. Alisema kutokana na tukio hilo, polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini sababu za mwanafunzi huyo kuamua kujiua. Taarifa zaidi kutoka kijijini hapo zinadai mazishi ya mwanafunzi huyo yalifanyika jana. Taarifa zaidi kutoka Kijiji cha Inyala ambako alikuwa akiishi marehemu Nyaulawa, zinaeleza kuwa mbunge huyo alikuwa akiwasomesha watoto wengi yatima ambao wamefiwa na wazazi wao ambao baada ya kupata taarifa za kifo chake wengi walichanganyikiwa. Hata hivyo, wakati baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Inyala wakidai kifo cha mwanafunzi huyo kimetokana na mshtuko wa kifo cha mbunge huyo, mmoja wa walimu wa shule ya Imezu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alidai habari za kifo hicho zimekuwa na mkanganyiko. “Wengi wanasema zimetokana na mshtuko wa kifo cha mbunge, lakini wengine wanadai mbuzi aliokuwa anachunga walipotea na kwamba alifokewa nyumbani kwao na kuagizwa kuwa asirudi nyumbani hadi awe amewapata mbuzi hao,” alidai mwalimu huyo. Nyaulawa alifariki dunia alfajiri ya Jumapili iliyopita nyumbani kwake Kawe Beach, Dar es Salaam baada ya kuugua muda mrefu saratani ya ini na alizikwa Inyala juzi. Katika tukio jingine, mkazi wa Kijiji cha Mwaselela, Mbalizi Wilaya ya Mbeya, Stella Kayuni (25), amejiua kwa kunywa sumu akiwa nyumbani kwake kijijini hapo juzi saa tatu usiku.

No comments:

Post a Comment