.

.

.

.

Friday, November 28, 2008

SHEIKH OMARI BAFADHILI AFARIKI DUNIA

Aliyewahi kuwa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Sheikh Omari Bafadhili, amefariki dunia baada ya kuugua ghafla na kuanguka mahakamani. Sheikh Bafadhili alifariki dunia jana wakati akikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa huo kwa matibabu. Alifariki muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, kuahirisha kesi ya madai ya kashfa iliyokuwa ikimkabili na wenzake wawili. Kesi hiyo, ambayo wadai wanataka walipwe fidia ya Sh. milioni 9, iliahirishwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Amiri Msumi hadi Januari 5, mwakani baada ya wakili wa wadai kushindwa kufika mahakamani kutokana na kuugua. Hakimu Msumi, alisema Sheikh Bafadhili, alikuwa mdaiwa namba moja katika kesi hiyo iliyofunguliwa mahakamani hapo mwaka 1993. Alisema, Sheikh huyo na Sheikh Abdul Hamadi na Bodi ya Usajili ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), walifunguliwa kesi hiyo mahakamani hapo, kila mmoja akidaiwa Sh. milioni 3. Hakimu huyo, alisema madai hayo yalifunguliwa mahakamani hapo na wadai, ambao ni pamoja na Sheikh Musa Suleiman, Sheikh Yahya Othmani na Sheikh Elbadai Mohamed. Alisema katika madai yao, wadai hao wanadai Sheikh Bafadhili na wenzake hao, waliwakashifu na kuiomba mahakama hiyo iwaamuru amlipe kila mmoja kiasi hicho cha fedha. Alisema kwa mara ya kwanza, wadaiwa walifikishwa mahakamani hapo Februari 23, mwaka 1993 wakidaiwa kuwakashifu masheikh hao kwa kuandika, kueneza barua na kuweka kwenye ubao wa matangazo siku ya sala ya Ijumaa bila uhalali. Hata hivyo, Hakimu huyo, alisema Machi 5 mwaka 1993, Sheikh Bafadhili, akiwa anatoa mawaidha msikitini kwenye sala ya Ijumaa, aliwasisitiza waumini wasome barua hiyo iliyokuwa kwenye ubao wa matangazo msikitini hapo. Alisema katika hukumu iliyotolewa Aprili 8, mwaka 2002 na Hakimu David Mrango, aliwaamuru wadaiwa kulipa fidia hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kutoa kashfa msikitini. Hakimu huyo alisema kuwa Sheikh huyo hakuridhika na hukumu hiyo, hivyo aliandika rufaa kupitia madai ya rufaa namba 73 ya mwaka 2002 aliyowasilishwa Mahakama Kuu Dar es Salaam mbele ya Jaji Njengafibili Mwaikugile. Alisema rufaa hiyo ilitupiliwa mbali katika hukumu iliyosomwa Agosti 19 mwaka 2003. Alisema kuwa Sheikh Bafadhili, aliamua kuomba maombi mengine ya rufaa kupeleka Mahakama Kuu mbele ya Jaji Thomas Mihayo, rufaa ambayo pia ilitupiliwa mbali katika hukumu iliyosomwa Aprili 19, mwaka 2004. Hata hivyo, Hakimu Msumi, alisema kesi hiyo ilirudishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kukaziwa hukumu kwa fomu CC namba 10 ambayo ilimtaka mdaiwa huyo kulipa fidia ya Sh. milioni 3 na akishindwa akamatwe na kufungwa kama mfungwa wa madai. Alisema mdaiwa huyo hakukubaliana na kitendo cha kukamatwa na alipinga kwa kupeleka kiapo chake cha maandishi mahakamani hapo. Hakimu huyo, alisema wakiwa katika hatua za kupanga tarehe ya kusikiliza maombi ya utekelezwaji wa hukumu hiyo jana, wakili wa upande wa wadai alikuwa anaumwa na kusababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi Januari 5, mwakani kwa kutajwa tena. Alisema baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Sheikh huyo alianguka na kubebwa kwa ajili ya kukimbizwa hospitalini kwa matibabu na kufariki dunia. Kaimu Mganga Mkuu wa zamu wa Kitengo cha wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Munira Vejtani, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho. Dk Vejtan alisema walimpokea Sheikh huyo akiwa amefariki dunia. Alisema inawezekana alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitalini kwa kuwa walianza kumpeleka Hospitali ya Aga Khan. Alisema kifo chake kimetokana na mshtuko wa ghafla, kwani wakati wa uhai wake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na shiniko la damu. Shekh huyo, aliondolewa madarakani mwaka 2006 na Mkutano Mkuu wa Masheikh uamuzi ambao ulitangazwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, naye amethibitisha kutokea kwa kifo hicho.

No comments:

Post a Comment