.

.

.

.

Saturday, November 29, 2008

TAIFA STARS YAIFUNGA SUDAN 3 - 1


NI raha, raha tupu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya ushindi mzuri wa Taifa Stars wa mabao 3-1 dhidi ya Sudan katika mchezo uliofanyika jana kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania.
Ushindi huo umeifanya Tanzania kujiweka pazuri kwa mchezo wa marudiano na kuanza kupigia mahesabu safari ya Ivory Coast kwenye fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN, Julai mwakani.
Stars sasa inahitaji sare ya aina yoyote iweze kukata tiketi ya fainali katika mchezo wa marudiano utakaofanyika kati ya Desemba 13 na 15.
Katika mchezo huo ambao Stars walianza kwa mashambulizi tangu dakika ya kwanza baada ya Athumani Idd kupaisha mpira akimwangalia kipa wa Sudan Akram Elhad.
Stars wakionekana kutulia na kupanga mashambulizi ya kushitukiza waliliandama lango dakika tano za kwanza lakini Jerry Tegete mara zote hakuwa makini.
Katika dakika ya 12, nusura Haruna Moshi 'Boban' aipatie Stars bao baada ya kupiga shuti kali na kipa wa Sudan, Elhad kulipangua.
Kadri muda ulivyokuwa unakwenda ndivyo Stars ilivyozidisha mashambulizi langoni mwa Sudan na kufanikiwa kuandika bao la kwanza katika dakika ya 25 lililofungwa na Tegete baada ya kazi ya Mrisho Ngasa aliyewatoka mabeki watatu wa Sudan na kutoa pasi kwa mfungaji.
Stars waliokuwa wakishangiliwa uwanja mzima huku wakiwa na uhakika wa kupata Sh1milioni kila mchezaji kutoka kwa wadhamini, Kampuni ya Bia ya Serengeti, SBL, walicheza kwa nguvu huku kila mmoja kuonekana kujituma vilivyo.
Hata hivyo, Sudan walichafua gazeti baada ya kusawazisha bao dakika 27 kupitia kwa Saifeldin Ali Idris.
Kipindi cha pili, Stars ilibadilika hasa katika kiungo na kukamata kila idara ya Wanubi hao na katika dakika ya 59, Athuman Idd 'Chuji' ambaye katika mchezo huo hakuwa katika kiwango chake aliipatia Stars bao la pili kwa shuti la umbali wa mita 40 na kuamsha hoi hoi na nderemo kwa mashabiki.
Kigi Makasy ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Henry Joseph ambaye aliumia mguu aliifungia Stars bao la tatu dakika ya 67 kilaini akipokea pasi ya Tegete hivyo kumuacha kipa wa Sudan akishindwa la kufanya.
Licha ya Sudan kutaka kusawazisha mabao yao ilishindwa kutokana na umakini wa mabeki wa Stars wakiongozwa na Salum Sued na kipa Shaaban Dihile ambaye ni mechi yake ya pili ya kimataifa kuidakia Stars.
Sudan walipata pigo dakika ya 90 ya mchezo baada ya kipa wao Elhad kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Mnkant Ntaban kutoka Zimbabwe baada ya kumkata mtama Ngassa aliyempiga chenga na kuelekea kufunga bao la nne.
Kocha mkuu wa Stars, Marcio Maximo aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo, lakini akasema bado wana kazi ngumu kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika wiki mbili zijazo nchini Sudan.
" Timu imecheza vizuri hasa wachezaji wangu vijana, tunafurahia ushindi lakini lazima tutambue kuwa tuna kazi bado tena mara mbili tukifika kwao, kwani Sudan ni timu nzuri yenye uzoefu mkubwa na ngumu kufungika kwao lakini tutapambana," alisema Maximo.
Naye kocha wa Sudan Mohamed Abdallah aliwasifu Stars kwa mchezo mzuri waliouonyesha lakini akaahidi kushinda mabao 2-0 mchezo wa marudiano mjini Khartoum.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko safarini Doha, Qatar, ametuma salaam za pongezi kwa vijana wake kutokana na ushindi huo.

No comments:

Post a Comment