.

.

.

.

Tuesday, December 09, 2008

WAZANZIBARI ???

KIKUNDI cha Wazanzibari wanaotaka kutambuliwa kwa uhuru wa Zanzibar wa Desemba 10, mwaka 1963 kimeibuka na kuandaa sherehe za kuadhimisha miaka 45 ya uhuru huo.
Mratibu wa sherehe hizo, Daudi Seif jana aliwaeleza waandishi wa habari kuwa maadhimisho hayo yatafanyika katika mikoa miwili ya Unguja na katika nyumba za ibada.
Alisema kwamba wameamua kuandaa sherehe hizo ili kuwakumbuka wanaharakati waliopigania kudai uhuru wa Zanzibar kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza, kabla ya kufanyika Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964.
Alieleza kwamba kwa kuwa maadhimisho hayo yatafanyika katika nyumba za ibada wameona hakuna sababu ya kuomba kibali chochote kutoka jeshi la Polisi Zanzibar.
Aliyataja maeneo yatakayohusika na sherehe hizo ni katika mkoa wa Kaskazini Unguja, katika kisiwa cha Tumbatu, Donge na Mkwajuni.
“Maadhimisho yatatanguliwa na kisomo maalum cha kuwakumbuka wanaharakati waliofanikisha uhuru wa Zanzibar mwaka 1963, kwa vile wamekuwa hawaenziwi licha ya kuwa na mchango mkubwa katika ukombozi wa Zanzibar”, alisema Seif.
Alisema katika mkoa wa Mjini Magharibi wananchi watakusanyika katika msikiti wa Mabluu mtaa wa Gulioni na kutakuwepo na matamko maalum, ili kuwakumbusha vijana wa sasa hivi historia ya Zanzibar kwa vile wengi wao hawatambui uhuru wa 1963.
Aidha alisema baada ya hitma hiyo kukamilika katika misikiti hiyo kutatolewa sadaka itakayojumuisha haluwa na kahawa kwa watu watakaoshiriki.
Seif alisema wameamua kufanya sherehe hizo sasa kutokana na kuimarika uhuru wa Demokrasia ambapo huko nyuma haukuwepo.
Alieleza kwamba ni jambo la kushangaza kuona uhuru wa Tanganyika huadhimishwa kila ifikapo Desemba 9, lakini Uhuru wa Zanzibar umesahaulika na badala yake kuadhimishwa siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, 12 Januari, 1964.
Alisema matayarisho yote yamekamilika, ikiwemo fulana maalum zitakazovaliwa siku hiyo, zenye maandishi yanayosomeka ‘10 Desemba, 1963 Uhuru wa Zanzibar na upande wa pili zikisomeka 10 Desemba, 1963 Zanzibar, United Nation Organization’.
Alisema kwamba fulana hizo zimechapishwa nchini Thailand na sehemu kubwa ya gharama zilitokana na michango ya Wazanzibari waliopo nchini na nje ya nchi.
Hata hivyo, serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema haina taarifa yoyote kuhusiana na sherehe hizo zinazofanyika leo.
Waziri wa nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan alisema maadhimisho hayo hayatambuliwi kwa vile hayamo katika sherehe za kitaifa.
Alisema uhuru wa Zanzibar unatambulika kuwa ni Januari 12, 1964 ambao ulipatikana kwa njia ya Mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa Kisultani na kuongeza kuwa taarifa hizo ni ngeni na kuahidi kuwasiliana na vyombo vya sheria, kwa vile Zanzibar hakuna uhuru wa mwaka 1963, uhuru wa Zanzibar ni mmoja tu wa Januari 12.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Shaaban alisema kuwa Polisi haina taarifa yoyote juu ya maadhimisho hayo.
Vikundi kama hivyo vya watu wanaojiita wazalendo wa Zanzibar vimekuwa vikiibuka mara kwa mara na kudai vinatetea hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Hivi karibuni kikundi cha Wazanzibari 11 walizuiwa kufanya maandamano waliyokuwa wameyaandaa kupinga kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa Bungeni kuwa Zanzibar si nchi.
Wakati hayo yakijitokeza Wazanzibari wanaoishi Uingereza wameandaa kongamano litakalofanyika Disemba 13 na 14 huko Uingereza kujadili hatma ya Zanzibar, Katika kongamano hilo baadhi ya wajumbe wamealikwa kutoka Zanzibar na tayari wamewasili nchini Uingereza wakiwemo waandishi wa habari maarufu wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment