.

.

.

.

Thursday, January 15, 2009

HASSAN AL-TURABI AKAMATWA

Kiongozi wa Kiislamu nchini Sudan Hassan al-Turabi amekamatwa baada ya kutoa matamshi ya kumtaka Rais Omar al-Bashir kujisalimisha kujibu tuhuma za uhalifu wa kivita.
Kiongozi huyo wa zamani wa upinzani ni mtu anayeheshimika sana nchini Sudan, amesema Rais ni lazima aende katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya The Hague kukabiliana na mashtaka yanayomkabili kuhusiana na mzozo wa Darfur.
Mtoto wa Bwana Turabi amesema ana hofu na afya ya baba yake ambaye ana umri wa miaka 76.
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa (ICC) bado wanajadiliana kutoa waranti ya kukamatwa Bwana Bashir.
Mwandishi wa BBC aliye mjini Khartoum Amber Henshaw amesema hali ya wasiwasi inazidi wakati huu uamuzi wa mahakama hiyo ukiwa unasubiriwa kwa shauku kubwa.
Mkuu wa idara ya usalama wa taifa nchini Sudan alisema hivi karibuni wageni huenda wakashambuliwa iwapo waranti ya kukamatwa rais wao itatolewa.
Kwa mujibu wa familia ya Bwana Turabi, kiongozi huyo wa dini alichukuliwa kutoka nyumbani kwake mjini Khartoum saa tatu usiku siku jana.
Mwanawe wa kiume, Siddig al-Turabi, ameiambia BBC kwamba ana wasiwasi na mahojiano magumu atakayofanyiwa kutokana na afya yake.

No comments:

Post a Comment