.
.
Wednesday, January 21, 2009
SLAA AZIDI KUMKABA KOO MKAPA
Baada ya menejimenti ya mgodi wa Kiwira Coal and Power Ltd, kufichua kuwa unamilikiwa kwa pamoja na familia ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, amesisitiza kuwa Mkapa, lazima afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka. Akizungumza jana, Dk. Slaa alisema hakuna sababu ya kutomfikisha mahakamani Mkapa kwani imeshabainika kuwa alijiuzia mgodi huo kinyume cha taratibu. Alisema madai kwamba ili kumfikisha Mkapa mahakamani kunahitajika aondolewe kinga si za kweli kwani Katiba haisemi hivyo. ``Nimesoma Katiba yote hakuna sehemu ambayo tunatakiwa kumwondolea kinga Mkapa...anayehitaji kuondolewa kinga ni Rais aliyeko madarakani tu, kwa Mkapa, Katiba haisemi hivyo, kwa hiyo tusipoteze muda, tumpeleke mahakamani akajibu tuhuma dhidi yake,`` alisema. Aidha, alisema Katiba inasema ili Rais aliyeko madarakani aondolewe kinga ya kutokushtakiwa inahitajika theluthi mbili ya kura za wabunge wote lakini haisemi hivyo kwa Rais aliyemaliza muda wake. Alisema Mkapa alipewa dhamana ya kulinda rasilimali za Watanzania lakini kinyume chake aliamua kufanyabiashara akiwa madarakani. ``Hapa hakuna namna ambayo Mkapa atajinusuru, akamatwe yeye na Yona wahojiwe namna walivyojiuzia mgodi wa Kiwira na hatua za kisheria zichukuliwe,`` alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment