.

.

.

.

Monday, March 16, 2009

KIKWETE KUZUNGUMZA LEO HAPA UINGEREZA

Rais Jakaya Kikwete akiagana na Mku wa Majeshi ya ulinzi Davis Mwamunyange (kushoto) Inspekta jenrali wa Polisi, Said Mwema na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kabla ya kusafiri kwenda London Uingereza kwa ajili ya ziara maalumu.
RAIS Jakaya Kikwete ameondoka nchini kwenda London, Uingereza kuhudhuria mkutano
maalum ulioitishwa na waziri mkuu wa nchi hiyo, Gordon Brown kujadili kuporomoka kwa uchumi duniani.
Kikwete ni mmoja wa viongozi wachache wa Afrika walioalikwa na Gordon Brown kwa ajili ya mkutano huo unaofanyika leo kwenye jengo la Lancaster House, kujadili kuyumba huko kwa uchumi duniani na jinsi kunavyoliathiri bara la Afrika.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema kwenye mkutano huo wa leo unaojulikana kama Pre-G20 London Summit Africa Outreach Consultative Meeting, Waziri Brown anataka kupata msimamo na kuisikia sauti ya bara la Afrika, sauti ambayo itawasilishwa katika mkutano wa mataifa ya G-20 uliopangwa kufanyika London, Uingereza mwezi ujao.
Brown ndiye mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano huo na nchi tajiri zenye viwanda vingi zaidi duniani na zile zinazochipukia haraka kwa nguvu za kiuchumi.
Kwenye mkutano wa leo, Rais Kikwete, ambaye amemaliza kipindi chake cha uenyekiti wa Umoja wa Afrika mapema mwaka huu, atawasilisha maazimio yaliyofikiwa katika mkutano kati ya nchi za Afrika na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) uliofanyika mjini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia Jumanne ya wiki iliyopita.
Mkutano huo wa kwanza wa aina yake, mbali na kujadili uhusiano kati ya Afrika na IMF, ulijadili kwa kina kuyumba kwa uchumi duniani na mtikisiko wa taasisi za kifedha ulivyoliathiri bara la Afrika.
Mkutano huo pia ulipendekeza njia ambazo jumuia ya kimataifa inatakiwa kuzichukua kupunguza makali hayo kwa bara la Afrika na katika jitihada za jumla za kupambana na umasikini na kuwezesha kufanikisha Malengo ya Milenia (MDG's).

No comments:

Post a Comment