.

.

.

.

Friday, February 18, 2011

MUHUTASARI WA MABOMU YA GONGO LA MBOTO

MILIPUKO ya mabomu iliyotokea usiku wa kuamkia jana katika ghala la kuhifadhia silaha la JWTZ, Kambi ya Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, imesababisha vifo vya watu 39 na majeruhi 292.
Imebainika kuwa maiti na majeruhi hao walifikishwa kwa nyakati tofauti juzi katika Hospitali za Wilaya ya Ilala (Amana), Temeke na Muhimbili za jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa uchunguzi , Hospitali ya Taifa Muhimbili hadi jana mchana ilikuwa imepokea maiti 18 na majeruhi 80, Amana maiti 19, majeruhi 138 na Temeke maiti wawili na majeruhi 74.

Hata hivyo, Serikali ilisema waliokufa katika milipuko hiyo ni watu 20 na majeruhi ni 300.

AMANA
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshaki Shemweta amesema kuwa siku ya tukio, hospitali hiyo ilipokea majeruhi 157.
"Majeruhi 40 walifanyiwa uchunguzi na kuruhusiwa, wengine 63 bado wanaendelea na matibabu hapa na majeruhi 19 walifariki dunia baada ya kufikishwa hospitalini hapa," alisema Shemweta na kueleza kuwa hata hivyo, idadi hiyo inaendelea kuongezeka.

Majina ya waliokufa
Shemweta aliwataja waliofia hospitalini hapo kuwa ni watu watatu wa familia moja; Neema, Tina na Stela Nyigiogo. Kwa mujibu wa mganga huyo, wengine waliokufa ni Zahari Imamu, Ally Chambusa na Hadija Ally.
Wengine ni Sofia Salumu, Mwindini Mamla, Hansi Ibrahimu, Neema James, Vivian Suma, Mainda Ismail, Salehe Musa, Amina Kihiyo, Rose Anthony na Sia Salum.
Shemweta alisema kuwa miili ya wanaume wawili haijatambulika, hivyo bado jihada za kuitambua zinaendelea ambapo kati ya marehemu, wanaume ni 8 akiwamo askari magereza mmoja na wanawake ni 11.
Hata hivyo, Shemweta alieleza kuwa maiti kumi zilitarajiwa kupelekwa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi
“Miili hiyo inahamishwa pamoja na majeruhi 35 wanaopelekwa katika kitengo cha mifupa cha MOI kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kufanyiwa upasuaji,” alisema Shemwela.

MUHIMBILI
Habari kutoka Muhimbili zimeeleza kuwa hospitali hiyo imepokea maiti 18 na majeruhi 80 waliotokana na milipuko hiyo.
Afisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha aliliambia gazeti hili kuwa kati ya maiti hao, wanawake ni saba na wanaume 11.
“Jana (juzi) tulipokea maiti tano na leo hii tumepokea maiti 13 kutoka Hospitali ya Amana na jumla yake kuwa 18 kati yao wanawake ni saba na wanaume ni 11,"alisema Aligaesha.
Aligaesha aliwataja marehemu hao kuwa ni Zainabu Mohamedi kutoka trafiki makao makuu, Baba Lyaiya ambaye ni mkazi wa Kivule, Hadija Aly, Sofia Salumu, Mwidini Mwaule, Hamisi Hasani na Zaharani Imamu wote wakazi wa Gongo la Mboto Mwisho pamoja na Aly Chambulo, Neema James, Theolas Katombo na Aly Ibrahimu.
Hata hivyo, ofisa habari huyo alieleza kuwa badhi ya maiti zilikuwa bado zinaletwa na polisi katika hosipitali hiyo na kwamba zilikuwa bado hazijatambuliwa.
“Miongoni mwa majeruhi 80 tuliowapokea na waliopo wodini mpaka sasa ni 18 na madaktari kwa kushirikiana na wauguzi wanaendelea kuhakikisha wanapata huduma sitahiki,”alisema na kueleza kuwa majeruhi 44 wamepelekwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), kwa ajili ya matibabu zaidi.


TEMEKE
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya Temeke, Marium Malliwah alisema hosipitali yake ilipokea majeruhi 74 na wawili kati yao walifariki dunia.
Alisema baada ya matibabu, majeruhi 34 waliruhusiwa na wengine wanane wakapelekwa katika Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Wengi wavunjika mikono, miguu

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu huyo, wengi wa majeruhi waliofikishwa hospitali hapo walikuwa wamevunjika mikono na miguu na baadhi yao walikuwa kwenye hali mbaya.

“Katika hospitali yetu tumepokea majeuhi 74; wawili wamepoteza maisha, wagonjwa wanne tumewapeleka Muhimbili baada ya kuonekana kuvunjika mikono na miguu na kuwa katika hali mbaya. Majeruhi waliobaki tumewapeleka katika kambi ya majanga ambapo wamelazwa kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Malliwah.

JWTZ
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa JWTZ, Luteni Kanali Kapambala Mgawe alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa watu 20 wamekufa katika tukio hilo.
Aidha, alisema watu 500 wamejeruhiwa katika tukio hilo na wanatibiwa katika hospitali tofauti za jijini Dar es Salaam.
Mgawe amewataka wananchi kutoondoka kwenye maeneo wanayoishi kwa kuwa mabaki ya mabomu yaliyozagaa mitaani hayawezi kulipuka.
“Ninachowaambia wananchi ni kwamba msiondoke kwenda kokote, mabomu hayawezi kulipuka tena, ila msiyaguse yaacheni hadi askari watakapokuja kuyachukua,” alisema.

MABOMU YAZAGAA HOVYO
Imeshuhudiwa mabaki ya mabomu yakiwa yamezagaa ovyo huku mengine yakiwa ndani ya nyumba katika eneo la Gongo la Mboto.
“ Wanatuambia tusihame, hivi unaweza kuendelea kulala katika kitanda huku pembeni kukiwa na bomu, wasituletee siasa tunaondoka ili kuokoa roho zetu, “ alisema Hamis Chande ambaye nyumba yake imetobolewa na bomu.
Alisema pamoja na bomu kubomoa sehemu ya nyumba hiyo, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa katika familia hiyo yenye watu watano.

KINA MAMA NA WATOTO

Mamia ya wanawake na watoto walionekana wakitembea kwa miguu wakitokea Gongolamboto kwenda katika maeneo mbalimbali ili kunusuru maisha yao.


WIZARA YA AFYA
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Blandina Nyoni, aliwataka wananchi waliopatwa na mshituko uliotokana na milipuko ya mambomu hayo, waende hospitali ili wakapimwe afya zao.

“Wito wangu ni kwa wananchi wote ambao kwa namna moja ama nyingine milipuko ya mabomu imewaathiri, wasijifiche majumbani waende hospitali kwa uchunguzi ili kubaini kama wameathirika pia, tumeandaa mazingira mazuri ya kukabiliana na mahitaji yote ya tiba kwa wahanga hao,” alisema Nyoni.

Watoto 300 wapotea Dar

Zaidi ya watoto 300 wamepotea jijini Dar es Salaam kutokana na milipuko hiyo ya mabomu, polisi wamesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime aliliambia Mwananchi jana kuwa, katika Uwanja wa Uhuru walikohifadhiwa waathirika wa milipuko hiyo kuna idadi kubwa ya watoto waliopotezana na wazazi wao wakati wakiyakimbia makazi yao.


“Idadi ni kubwa, watoto zaidi 300 hawajulikani walipo, lakini tunafanya kila iwezekanavyo ili kuhakikisha watoto wanapatikana na kuwaleta kwenye makambi ya hapa uwanjani kwa ajili ya kutambuliwa na wazazi wao,”alisema Misime.


Mmoja wa waathirika hao aliyejitambulisha kwa jina la Mariam Ndwanga alisema alipotezana na watoto wake wawili alipokuwa akikimbia kutoka Pugu hadi Uwanja wa Uhuru.
“Nilipofika hapa nilimwona mwanangu mmoja, lakini sijui hatma ya mwanangu wa pili.,”alisema Mariam.
Uwanja wa Uhuru ndio ulioteuliwa na Serikali kuwa eneo la muda la kuwahifadhi waathirika hao. Tayari mahema kadhaa yamejengwa katika uwanja huo ijapokuwa hayakidhi haja kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kuhitaji msaada.


Kamanda Misime alisema wanaendelea kupokea watoto kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwarahisishia mawasiliano kati yao na wazazi wao.


Mkurugenzi wa Maendeleo ya Shirika la Msalaba Mwekundu, Julias Kejo alisema idadi ya watoto waliopokelewa uwanjani hapo usiku wa kuamkia jana ni 179, ambapo baadhi ya watoto hao walitambuliwa na wazazi wao.
Kejo alisema zaidi ya wazazi 254 waliofika kwenye kambi hiyo ya muda ili kuwatambua watoto hawakuweza kuwaona watoto wao hivyo walilazimika kukaa na kuendelea kusubiri wakati polisi na watu waokoaji wa chama cha msalaba mwekundu wakiendelea kuwaokota watoto na kuwapeleka kwenye makambi.
“Wazazi endeleeni kusuburi kwa kuwa watoto wengi wanaendelea kuokotwa sehemu mbalimbali, na watapoletwa mtaweza kuwatambua watoto wenu ili muweze kuondoka nao mnachotakiwa muwe wavumilivu,”alisema Kejo.

Wizara kuwahudumia waathirika
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nyoni alisema Serikali imejiandaa kutoa huduma kwa waathirika wa mabomu ikiwa pamoja na dawa ,chakula na maji ili kunusuru afya zao hadi watakapotambuliwa na ndugu zao au kupata hifadhi.


“Wengine tangu milipuko ya mabomu ilipotokea hawajala kitu chochote hadi sasa, hivyo Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha waathirika hao wanapata huduma muhimu kama maji, chakula na dawa,”alisema Nyoni.
JK tangaza msiba wa kitaifaMKUU WA NCHI

RAIS Jakaya Kikwete amesema mabomu yaliyolipuka kwenye maghala 23 juzi usiku katika Kambi ya Jeshi 511 Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam jana ni Maafa ya Kitaifa.


Akizungumza wakati alipotembelea kambi hiyo, Rais Kikwete alisema kikosi hicho ndio makao makuu ya hifadhi za mahitaji ya kijeshi, hivyo kilichoteketea sio silaha tu, bali hata sare za wanajeshi.
“Haya ni maafa ya kitaifa, kwa sababu kikosi hiki ndio makao makuu ya hifadhi ya kijeshi, ikiwemo silaha na mavazi yao ambayo mpaka sasa hivi naongea vyote vimetekelea kwa moto,”alisema Kikwete.
Aliongeza kutokana na hali hiyo msiba uliojitokeza kwa wananchi, ni msiba wa kitaifa, hivyo basi wapo pamoja nao katika kuomboleza na kuwaondoa hofu juu ya hilo.


Alisema, mpaka sasa Baraza la Taifa la Usalama litafanya kikao ili liweze kujua ukubwa wa tatizo, kisha kuchukua hatua stahiki za kuwaeleleza wananchi juu ya tukio hilo.
“Tumepoteza ndugu zetu, mali za kijeshi ambazo zote zilikuwa zinahifadhiwa humu ndani, lakini mpaka sasa kuna watalaam tayari wameanza kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo,ninawaomba wananchi watulie ili waweze kufanya kazi yao,”alibainisha.

Kwa mujibu wa Kikwete, baada ya kupata taarifa za milipuko hiyo aliitisha kikao cha dharura Ikulu na Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange, majira ya saa 9:00 usiku kwa ajili ya kujadili tatizo hilo.
Alisema kutokana na hali hiyo, mkuu wa kambi hiyo, aliwapa taarifa kwamba, maghala hayo yameungua na vifaa vyote vilivyomo ndani yake, lakini askari mmoja ndiye aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
“Kwa taarifa nilizonazo ni askari mmoja aliyejeruhiwa, hivyo basi ninawaomba wananchi waondoe wasiwasi juu ya tukio hilo, Serikali iko pamoja nao kuhakikisha kuwa hatari zilizopo zinadhibitiwa, na kwamba wananchi wanarudi katika hali yao ya kawaida,”alisema Kikwete.

JWTZ yaunda tume
Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Meja Generali Abdulrahaman Shimbo alisema wameunda tume ya kijeshi ya kuchunguza tukio hilo na kuokota mabomu yaliyodondoka kwenye makazi ya watu.
Alisema tayari askari wameanza kupita kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kutafuta mabaki hayo ili waweze kuyawasilisha kikosini kwa ajili ya kuyatekeleza.


“Tumeunda tume ya kijeshi ya kuchunguza tukio hilo, na kwamba tayari askari wameanza kupita kwenye makazi ya watu kwa ajilii ya kuokota vipande vilivyobaki ili waweze kuleta kikosini kuyatekeleza,”alisema Shimbo.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo wananchi wametakiwa kuondoa hofu juu ya tukio hilo kwa sababu hayawezi kulipuka tena, hivyo basi mabomu hayo wawaonyeshe askari hao ili waweze kuyachukua.
Alisema, taarifa zilizotolewa na wananchi juu ya kulipuka kwa mabomu mengine ni uvumi wa uongo, hivyo basi wananchi wametakiwa kuondoa wasiwasi juu ya hali hiyo.


NAULI ZA USAFIRI JUU
Nauli za kuelekea Gongo la Mboto kutoka Ubungo jana zilipanga ghafla kutoka Sh250 hadi Sh1000 kutoka Ubungo.
Nauli ya Bajaji na pikipiki ilikuwa Sh20,000 hadi Sh30,000 kutoka Ubungo kwenda Gongo la Mboto.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema gharama hiyo ni kubwa, na kwamba inawaumiza kutokana matatizo waliyopata.

“Hatuna budi kupanda kwa sababu mpaka sasa tumetembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta usafiri ambao hivi sasa ni gharama na magari hakuna,”alisema Mwajuma Omary(40) mkazi wa Gongo la Mboto.
Aliongeza kuwa gharama ya kukodi pikipiki au bajaji katiya Gongo la Mboto na Ubungo ni kati Sh 20,000 hadi 40,000 wakati nauli ya daladala Sh1000 kwa mtu mmoja.

Alisema kutokana na hali hiyo magari hayo yamepandisha nauli hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu waliopo vituoni jambo ambalo limewafanya wapandishe nauli hiyo ghafla.
Nao baadhi yawaendesha piki piki na Bajaji wamesema kuwa, tukio hilo ni sawa na “kufa kufaana”, kwa sababu abiria waliopo vituoni ni wengi, jambo ambalo limewafanya wapandishe nauli ili waweze kupata faida zaidi.

“Kufa kufaana,lazima tupandishe nauli ili na sisi tuwezen kufaidika, kwa sababu gharama ya mafuta ni kubwa, na kwamba sisi tunatoa msaada tu,”alisema Juma Abdul(31) mkazi wa Buguruni.


Habari hii imeandaliwa na Alphey Athanas, Hidaya Kivatwa, Edom Mwasamya, Elias Sichalwe, Pamela Chilongola, Patricia Kimelemeta, Hussein Issa na Raymond Kaminyoge


2 comments:

  1. thank you jesse for updating us na hali hii inasikitisha sana..,

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli inasikitisha sana nanajaribu kufikiria kwa undani kweli hii ni ajali au mipango maana itawezekenaje kitu hichi kitokee kwa mara ya pili kwa kweli kuna jambo litatokeza natutajua nini hasa njama hizi.Labda wanajaribu kuwafukuza kijanja wakazi wa maeneo hayo.Kweli ndugu zangu tuangalia hii mambo kwa makini sielewi uzembe gani umefanyika kwa mara ya pili.

    ReplyDelete