.

.

.

.

Tuesday, April 14, 2009

DARAJA LA KIGAMBONI KUKAMILIKA 2013

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetangaza kuwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni, jijini Dar es Salaam litalokagharimu Euro 45 milioni utaanza 2011.
Daraja hilo ambalo litakuwa na upana wa mita 640 na njia sita, ambazo kila upande utakuwa na njia tatu, linatarajiwa kuondoa kero ya usafiri kati ya Kigamboni na katikati ya jiji.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa wabunge wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa NSSF Yacoub Kidula alisema, mchakato wa utekelezaji mradi huo utaanza rasmi Mei, mwaka huu.
“Waheshimiwa wabunge tutaanza kumpata mshauri wa mradi Mei mwaka huu, kuandaa nyaraka za kuleta mapendekezo Oktoba na kuzitaka kampuni zilete mapendekezo mwezi Disemba mwaka huu,” alisema Kidula na kuongeza:
“Febuari mwaka 2010 tutafanya uteuzi wa mbia binafsi, Julai mwaka huohuo tutapitia upya mradi kwa pamoja, baada ya hapo tutapata idhini ya Serikali kuendelea na mbia huyo mwezi Oktoba 2010”.

Alifafanua kuwa,
Aprili mwaka 2011 watapitia michoro na nyaraka za zabuni ya mradi huo, ili kupata nafasi ya kumteua Mkandarasi wa kufanya kazi hiyo Septemba mwaka huohuo.
“Kuanzia
Disemba mwaka 2011 kazi ya ujenzi wa daraja itaanza rasmi na tutahakikisha kuwa hadi kufikia
Disemba 2013 ujenzi huo uwe umekamilika na kuanza rasmi kutumika kwa daraja hilo” alisema Kidula.

Kwa mujibu wa Kidula, ujenzi wa daraja hilo utafanyika katika eneo la mkondo wa maji ya bahari uliopo Kurasini baada ya Bandari ya kuu ya Dar es Salaam,
Alisema, daraja hilo litakuwa na barabara tatu kila upande, ambapo upande wa Kigamboni itakuwa na umbali wa kilomita moja na nusu, huku upande wa katikati ya jiji ukiwa na kilomita moja pekee.
Kidula alieleza kuwa, daraja hilo litakuwa ni kivuko cha uhakika na salama kwa watu wote na kwamba litafungua milango ya vitega uchumi vyenye manufaa ya kijamii na kiuchumi; ikiwa ni pamoja na majengo ya wazalishaji, hoteli, nyumba za kuishi na hata vituo vya kibiashara.
Alisema, NSSF ilitangaza kumpata mbia binafsi na kwamba makampuni sita yalipitishwa kati ya yale yaliyoomba Februari mwaka huu.
“Makampuni hayo yataalikwa kuleta mapendekezo baada ya nyaraka muhimu kukamilika na tunatarajia kuwa, mchango wa kifedha wa mbia binafsi utafikia asilimia 70 ya gharama zote” alisema.
Alisema, utaratibu mpya wa utekelezaji wa mradi huo ulichangia kuchelewa kuanza kwa mradi na kwamba, chini ya utaratibu wa awali, daraja lingeanza kujengwa mnamo mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment