.

.

.

.

Monday, May 18, 2009

RAIS KIKWETE AENDA MAREKANI


Rais Jakaya Kikwete aliondoka nchini jana mchana kwenda Marekani kwa ziara ya kikazi ambako atakuwa na shughuli katika miji mitatu ya nchi hiyo, ukiwamo mji mkuu wa nchi hiyo, Washington, D.C. Wakati wa ziara yake, Rais
Kikwete atakutana na kuzungumza na viongozi wa Kampuni ya Teknolojia ya Kompyuta ya IBM mjini San Francisco kuhusu jinsi kampuni hiyo inavyoweza kusaidia zaidi maendeleo ya teknolojia hiyo nchini.
Tayari kampuni hiyo ya IBM imetoa wataalamu wa kuanzisha shule ya kisasa ya teknolojia ya kompyuta katika Chuo Kikuu kipya cha Dodoma kutokana na maombi ya Rais Kikwete kwa kampuni hiyo.
Rais Kikwete pia atakuwa mgeni rasmi katika hafla rasmi iliyoandaliwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Madaktari wa Marekani kwa ajili ya Afrika - Doctors for Africa (USDFA) - kwa kushirikiana na taasisi ya Los Angeles World Affairs Council. Hafla hiyo itafanyika mjini Los Angeles. Katika hafla hiyo, Rais Kikwete atatunukiwa nishani kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya afya katika Tanzania na Afrika kwa jumla.
Mjini Washington, D.C. Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi za kimataifa za fedha kuhusu hali ya sasa ya uchumi duniani na jinsi taasisi hizo zinavyoweza kuisaidia Tanzania kukabiliana na machafuko ya uchumi duniani. Rais pia atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa idara za Serikali ya Marekani.
Rais Kikwete vile vile atashiriki katika tukio maalumu la kuadhimisha umuhimu wa maji salama duniani la Global Safe Water. Kwenye tukio hilo, lililoandaliwa na taasisi ya Mohan Corporation, Rais Kikwete anatarajiwa kukabidhiwa gari maalumu la kusafisha maji ambalo linaweza kutumika popote iwe mijini ama vijijini.

No comments:

Post a Comment