.

.

.

.

Friday, June 05, 2009

MKULO MATATANI

BAJETI ya serikali kwa mwaka 2009/2010, imekaa vibaya na inaonyesha kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo, atakuwa na wakati mgumu wakati atakapoisoma bungeni Juni 11 kutokana na baadhi ya wabunge kutangaza dhahiri kutoa shilingi huku wakionya kuwa huenda hata bunge likavunjwa.
Onyo la wabunge hao ambao wengi ni kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kusini, limekuja baada ya Mkulo kuwasilisha Sura au Mwelekeo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2009/2010, mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, ambayo inatarajiwa kuwa ya Sh9.5trilioni ikilinganishwa na Sh7.3 trilioni za mwaka 2008/09.
Mwelekeo huo wa bajeti ya 2009/2010, unaonyesha serikali inatarajia kukusanya Sh9.5 trilioni ambazo kati ya hizo, Sh5.1 trilioni ni mapato ya ndani, Sh3.2 trilioni ni misaada na mikopo kutoka kwa wahisani na Sh1.2 trilioni, ni mapato mengine, huku matumizi ya kawaida yakitarajiwa kuwa Sh6.7 trilioni na maendeleo Sh2.8 trilioni.
Wabunge kutoka kamati mbalimbali nje ya Fedha na Uchumi, pamoja na baadhi ambao ni wajumbe wa kamati hiyo, walianza kuchambua mwelekeo huo wa bajeti kwa kumlipua Mkulo mbele ya jopo la wataalamu kutoka wizara hiyo na idara zake, hasa katika kipengele cha ujenzi wa barabara.
Walienda mbali zaidi kwa kusema kila waziri anajipendelea kwake, akiwemo waziri huyo wa fedha.

Mbunge Anthony Diallo (CCM-Ilemela), ndiye aliyeweka msimamo akimtahadharisha Waziri Mkulo kwamba bajeti hiyo kama ilivyo katika mwelekeo, haitaweza kupita bungeni na kuonya kuwa inaweza kuandika historia kwa bunge kuvunjwa.
"Nakwambia kama ndugu yangu, bajeti hii ikija kama ilivyo haitapita bungeni, Iam telling you my brother (nakwambia kaka yangu)... sikufichi, haipiti hii bajeti," alizungumza Diallo kwa msisitizo
.

Diallo alisema karibu Sh100 bilioni zimetengwa katika barabara zile zile, huku maeneo mengine ya nchi yakiwa hayana barabara za lami.
Alisema haingii akilini kuona sehemu ya barabara ya lami kutoka Same hadi Korogwe inatengewa fungu la Sh44 bilioni.
"Ukiangalia, karibu Sh100 bilioni ni barabara zile. Utakuta ni Morogoro, Dares Salaam na Iringa. Nasema kwa mara ya kwanza bunge linaweza kuvunjwa," alionya Diallo kabla ya kubeba mkoba wake na kuondoka.
Naye mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alionya bajeti hiyo inaweza kuigawa nchi kutokana na kuruhusu maendeleo makubwa katika baadhi ya maeneo huku mengine yakiwa na umasikini wa kutisha.
Dk Chegeni alifafanua kwamba, kitendo cha kukarabati barabara ya lami kati ya Chalinze-Segera-Tanga, haina mantiki wakati kuna maeneo hayana kabisa miundombinu ya lami.
Mbunge huyo wa moja ya majimbo ya kanda ya ziwa, alidiriki kusema: "Hata barabara ya Msata Bagamoyo haikupaswa kupewa kipaumbele zaidi kama kuna nyingine hazina lami. Labda kwa sababu anatoka Waziri wa Miundombinu (Dk Shukuru Kawambwa)."
Dk Chegeni alihoji barabara hiyo kuzidi kutengewa fedha wakati tayari nyingi zilichukuliwa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).
Akitoa mfano kuhusu hoja yake ya mawaziri 'kujimegea bajeti', Dk Chegeni alidai kuwa hata Basil Mramba akiwa Waziri wa Miundombinu alihamisha mabilioni ya fedha ya ujenzi wa barabara ya Usagara- Geita na kuzipeleka Rombo, ambako aliweka viwango ya Sh900 milioni kwa kilomita moja, kitu alichosema: "Kwa wakati ule haikuwezekana ni fedha nyingi."
Alisema pia haingii akilini kuona uwanja wa ndege wa Songwe Mbeya, ukitengewa tena Sh15 bilioni wakati uliwahi kutengewa Sh 30 bilioni, kitu alichosema si sahihi kwani kuna uwanja wa ndege wa Mwanza unahitaji kukarabatiwa au kujengewa eneo jingine (Terminal).
Mbunge wa Mvomero, Suleiman Saddiq (Mvomero-CCM), alitishia kwenda Ikulu kuonana na Rais Jakaya Kikwete kama barabara alizoahidiwa hazitakuwemo katika bajeti hiyo.
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na wabunge wawili ambao ni Dk Omari Mzeru (Morogoro Mjini-CCM) na Dk Abdallah Kigoda (Handeni-CCM), ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo ya fedha na uchumi.
Dk Mzeru alifafanua kwamba hakuna mantiki watu kuhoji ujenzi wa barabara ya Msata-Bagamoyo wakati ndiko anatoka Rais Kikwete, ambaye anapaswa kupita katika barabara salama yenye lami.
Kwa mujibu wa Dk Mzeru, hajaona duniani sehemu ambako wananchi hawathamini heshima ya rais wao na kuongeza kuwa eneo hilo ni la kiuchumi kwani litafungua utalii.
Dk Kigoda alihoji mantiki ya wabunge wenzake kushambulia ujenzi wa barabara ya Chalinze- Segera- Tanga, wakati ujenzi wa barabara ya Mwanza ni wa muda mrefu.
Hoja ya Dk Mzeru kuhusu heshima ya Dk Kikwete, ilipingwa na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), ambaye alisema jambo la msingi si kuangalia nani anatoka wapi, bali barabara zinapaswa kujengwa kwa kuangalia matokeo na faida kiuchumi.
"Napenda kupingana na hoja ya Dk Mzeru kuhusu ujenzi wa barabara ya Msata-Bagamoyo. Asiseme kwa sababu anatoka Rais basi ijengwe, tuangalie Economic impact (umuhimu wake kiuchumi), sasa ikiwa hivi kwingine ambako Rais hatoki itakuaje," alihoji Rashid.
Akifanya majumuisho ya hoja ya bajeti hiyo, ambayo inaonekana kurejesha kero zile zile za kodi, Mkulo alisema suala la ujenzi wa barabara hizo mbili unaweza kukwamishwa kwa chuki dhidi ya Dk Kawambwa.
Alisema barabara ya Chalinze-Segerea inajengwa na Denmark ambayo ndiyo imetoa fedha na kuchagua miradi yao hivyo, si rahisi kwa serikali kuipanga vinginevyo wangekataa na kuondoa fedha zao.
Akizungumzia bajeti yenyewe, Mkulo alisema mwaka 2009/2010, sera za mapato zinalenga kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua Sh5.1trilioni sawa na asilimia 16.4 ya Pato la Taifa (GDP), ikilinganishwa na mapato ya asilimia 15.9 kwa mwaka 2008/09.
Mkulo aliongeza kwamba pamoja na msukosuko wa kiuchumi wa dunia, serikali imeongeza nguvu katika kukusanya mapato ya ndani ya nchi.
Mchanganuo huo unaonyesha, mapato ya mikopo na misaada ya nje (MDRI/MCA -T) ni Sh3.2 trilioni, mapato ya halmashauri (Sh132 b), mapato yatokanayo na mauzo ya hisa (Sh 15 b) na mikopo ya ndani (Sh1.2 trilioni).
Akitaja mchanganuo wa bajeti hiyo kisekta kwa kujumuisha mishahara kwa mwaka 2009/2010, ambayo inaonyesha kupungua maeneo ya vipaumbele na kurejesha kodi, Mkulo alisema elimu itatengewa Sh1743.9 bilioni ikilinganishwa na Sh1,430.4 bilioni kwa mwaka 2008/09.
Kuhusu upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima na wafugaji, sekta ya kilimo kwa ujumla imetengewa Sh666.9 bilioni ikilinganishwa na Sh513.0 bilioni za mwaka 2008/09, sawa na ongezeko la asilimia 30.
Kwa upande wa miundombinu, Mkulo alisema kipaumbele kitakuwa ni kukamilisha miradi ya barabara inayoendelea, hivyo kwa ujumla imetengewa Sh1,096.6 bilioni ikilinganishwa na sh 973.3 bilioni za mwaka 2008/09, sawa na ongezeko la asilimia 12.7.
Sekta ya Afya, alisema kipaumbele ni kuendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma za uzazi na mtoto na kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika ngazi zote.
Kwa ujumla, Mkulo alisema sekta ya afya imetengewa Sh963.0 bilioni ikilinganishwa na Sh910.8 bilioni mwaka 2008/09, sawa na ongezeko la asilimia 5.7, huku huduma za maji umuhimu utawekwa katika kuboresha umwagiliaji na matumizi ya kawaida, ambayo mwelekeo unaonyesha itatengewa Sh347.3 bilioni ikilinganishwa na Sh231.6 bilioni za mwaka 2008/09.
Katika nishati na madini, Mkulo alisema kwa ujumla sekta hiyo imetengewa Sh285.5 bilioni ikilinganishwa na Sh378.8, sawa na upungufu wa asilimia 24.6.

No comments:

Post a Comment