.

.

.

.

Thursday, June 11, 2009

MWARABU NA MH.NDIO WANUNUZI WA VIUNGO VYA ALBINO

Mayenga Matongo, shahidi wa kwanza katika kesi ya mauaji ya albino inayomkabili mshtakiwa wa kwanza, Mboje Mawe, amedai kuwa mshitakiwa huyo katika mahojiano yake na polisi alimtaja mfanyabiashara mwenye asili ya Kiarabu, Yusuph Ibrahim, kuwa ndiye angemuuzia viungo vya marehemu Lyaku Willy. Mfanyabiashara huyo anafanya shughuli zake katika kijiji cha Lamadi, wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza.
Katika kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu maalum ya Shinyanga, mbele ya Jaji Gadi Mjemas, Matongo ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alidai kuwa alimtaja mfanyabiashara huyo wakati akihojiwa na polisi katika kijiji cha Halawa, mkoani Shinyanga.
Kesi hiyo ambayo jana iliingia siku ya tatu, inasikilizwa na Jaji Mjemas wakati upande wa mashitaka unaongozwa na Wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki akisaidiana na Renatus Mkude.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 25 ya mwaka 2009 ni Chenyenye Maganyale au Kishiwa, Sayi Gamanya au Mwanopili na Sayi Mofizi.
Alipoulizwa na mawakili wa utetezi kumtambua mahakamani mfanyabiashara huyo, Matongo alijibu kuwa hayupo mahakamani hapo na wala hamfahamu, ila alisikia ni Mwarabu na kwamba alikamatwa na polisi miezi michache iliyopita na kuachiwa. Naye shahidi wa pili, Yusuf Ramadhani (43), alidai mahakamani kuwa alimuona Mboje Mawe akifukua viungo vya marehemu Lyaku Willy nyumbani kwake chini ya ulinzi wa polisi.
Shahidi huyo wa pili huku akiongozwa na Wakili wa Serikali, Renatus Mkude, alidai kuwa mshitakiwa akiwa ndani ya gari la polisi walikwenda hadi nyumbani kwake ambapo alianza kufukua kichwa na baadaye miguu ya marehemu, vyote vikiwa ndani ya mfuko (sandarusi) akiwa amevifukua katika maeneo mawili tofauti.
Alidai kuwa baada ya kutoka nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza, walielekea nyumbani kwa mshtakiwa wa pili, Chenyenye Maganyale kwa ajili ya kuchukua kisu kilichotumika katika mauaji hayo. Alidai kuwa washtakiwa hao walikamatwa siku ya Desemba 7, mwaka jana wakati yeye alipokuwa akienda gulioni na kwamba aliona gari la polisi likiwa limekusanya watu wengi naye akasogelea eneo hilo. Alieleza kuwa ndani ya gari hilo kulikuwepo na watu sita wakiwemo washtakiwa wanne waliofikishwa mahakamani hapo.
Naye Shahidi Ramadhan, mkazi wa kijiji cha Nkindwabiye akiongozwa na Wakili wa serikali, Renatus Mkude, aliieleza Mahakama Kuu kuwa kiwiliwili cha marehemu Lyaku kilikutwa kikielea katika mto Kidamlida wilayani Bariadi na kwamba alimtambua marehemu kutokana na nguo alizokuwa amezivaa. Mahojiano kati ya Ramadhan na Mkude yalikuwa hivi:
Wakili: Ulipata wapi taarifa za kifo cha marehemu Lyaku Willy?
Shahidi: Mnamo tarehe 29 mwezi wa 11 mwaka 2008 nilikutana na kundi la wanawake lililotoka kuchimba mchanga kwa ajili ya ujenzi wa sekondari na kunipa taarifa, lakini kutokana na hofu ya kusumbuliwa na polisi nilikaa kimya.
Wakili: Wewe ulikuwa wapi wakati huo?
Shahidi: Tulikutana barabarani wakati nikienda centre kwa ajili ya ujenzi wa sekondari.
Wakili: Hatua gani ulichukua baada ya kupokea taarifa?
Shahidi: Ilipofika Desemba 4, 2008 nilitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji cha Nkindwabiye, Mayenga Matongo, ambaye ni shahidi wa kwanza.
Wakili: Baada ya hapo ulifanya nini?
Shahidi: Nilirudi nyumbani, majira ya saa 12.30 na nilisikia mayowe ya wanakijiji yakielekea mtoni, na mimi nilikwenda huko na kukuta kundi la watu, akiwemo Mtendaji wa Kijiji.
Alieleza kuwa Disemba 5, walirudi tena mtoni ambapo walimkuta Diwani Juma Bupilipili wa Kata ya Dutu huku Mtendaji akiwa ameenda polisi kutoa taarifa. Alidai kuwa diwani huyo aliwashauri waopoe kiwiliwili hicho majini ili aweze kumtambua na ndipo walipofanya hivyo na kumtambua kuwa alikuwa Lyaku Willy baada ya kuona nguo alizokuwa amevaa.
Alieleza kuwa polisi walifika katika eneo la tukio wakifuatana na daktari aliyefahamika kwa jina moja la Maduhu na baada ya kuufanya uchunguzi walimkamata Sayi Gamanya ambaye alikuwa akiishi na marehemu kama shemeji yake.
Gamanya ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Isanya ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo.
Shahidi huyo aliwatambua washtakiwa wa kwanza hadi wa tatu kwa kuwagusa mahakamani hapo baada ya kuelekezwa kufanya hivyo na wakili wa serikali.
Katika hatua nyingine, ulizuka ubishi wa kisheria baada ya upande wa utetezi kupinga hoja ya upande wa mashitaka uliouomba upande wa utetezi kukubali kutumia nyaraka halisi zilizoandikwa kwa mkono badala ya zile zilizochapwa kubainika kuwa na tofauti na zile walizokuwa nazo upande wa utetezi.
Hata hivyo, Jaji Mjemas alilazimika kusitisha mahakama kwa muda wa saa mbili ili nyaraka zilizoandikwa kwa mkono zirudufiwe na kusambazwa kwa mawakili wa utetezi pamoja na yeye.
Hata hivyo, mahakama haikuweza kuendelea kufuatia wakili wa mshitakiwa wa kwanza, Serapion Kahangwa, kuugua homa na kukimbizwa hospitalini. Kesi hiyo itaendelea leo.
Kahama mfanyabishara mwingine atajwa
Nayo Mahakama Kuu ya Tanzania inayosikiliza kesi za mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) mjini Kahama, mkoani Shinyanga, imeelezwa kuwa wauaji wa mtoto albino, Matatizo Dunia (13) aliyeuawa katika kijiji cha Bunyihuna walipanga kuuza viungo vyake kwa wafanyabiashara mjini Kahama kwa Sh. milioni 350.
Katika ushahidi wake wa upande wa mashitaka, shahidi wa tano katika kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia, Thenesco Sabuni, jana alieleza Mahakama Kuu jinsi mshitakiwa wa kwanza alivyotoa maelezo yake kwake kama Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ituga, muda mfupi baada ya kukamatwa na wananchi katika pori alilokuwa amejificha la kitongoji cha Ituga Kaskazini.
Sabuni alidai mahakamani mbele ya Jaji Gabriel Rwakibalila, anayesikiliza kesi hiyo na wazee wa Mahakama kuwa katika maelezo yake mbele ya mlinzi wa amani, mshitakiwa huyo, Masumbuko Madata, alikiri kushiriki mauaji hayo na kwamba wangeuza viungo vya marehemu huyo kwa wafanyabiashara hao kwa kulipwa Sh.milioni 350 fedha taslimu ambazo wangepewa Desemba mosi, mwaka jana saa saba mchana, lakini kabla ya muda huo kufika walikamatwa.
Aliwataja wafanyabiashara hao mbele ya Mahakama hiyo kuwa ni Machunda ambaye ni mfanyakazi wa kiwanda cha KTM na kuieleza mahakama kuwa ni kiwanda kinachojishughulisha na ununuzi wa pamba na mtu mwingine aliyemuita jina la “Mheshimiwa” ambaye alidai kuwa Madata hakumtaja ni mheshimiwa gani wa mjini Kahama.

No comments:

Post a Comment