.

.

.

.

Wednesday, June 17, 2009

NISHATI YA MAFUTA YAPANDA BEI BONGO

SIKU moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza ongezeko la bei ya mafuta, baadhi ya vituo vya kuuzuia nishati hiyo jijini Dar es Salaam vinauza kwa bei ya juu zaidi ya iliyotangazwa na mamlaka hiyo.
Ewura ilitangaza juzi kuwa petroli itapanda kwa asilimia 5.4, dizeli (5000 ppm) asilimia 2.64, dizeli (500 ppm) asilimia 2.38 na mafuta ya taa kwa asilimia 3.79, ongezeko ambalo limekuna vichwa vya wadau.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, ongezeko hilo linamaanisha kuwa kwa Dar es salaam bei ya mafuta kati ya Sh1,418 na 1,524 kwa petroli na Sh1,338 na Sh1,473 dizeli na kati ya Sh860 hadi Sh924 kwa mafuta ya taa.
Lakini uchunguzi uliofanywa na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana umebaini kuwa vituo vinauza lita moja ya petroli kwa bei ya kati ya Sh1,330 na Sh1,770, dizeli kati ya Sh1300 na Sh 1,470 na mafuta ya taa kati ya Sh750 na Sh1,000.
"Kama kuna vituo vinauza mafuta kwa bei zaidi ya elekezi, tutafika mara moja na kuvichukulia hatua," alisema msemaji meneja uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo.
"Utakuwa umefanya vizuri kama ukitutajia ni kituo gani ili tuende mara moja na kuchukua hatua."
Kituo ambacho kinauza mafuta kwa bei juu ya iliyotolewa na Ewura kinatakiwa kupigwa faini ya hadi Sh3, kufungiwa au adhabu zote kwa pamoja.
Katika taarifa yake ya juzi, Ewura ilieleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunatokana na sababu mbili kuu, ambazo ni ongezeko la bei za kununulia mafuta kwenye soko la dunia, ambako petroli imepanda kwa asilimia 46.31, dizeli (11.98%), na mafuta ya taa (6.42%).
Sababu ya pili imeelezwa kuwa ni kushuka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.
Naye mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Ezekiel Sekilasa alisema kupanda huko kwa bei ya mafuta hakutaathiri viwango vya nauli nchini.
Aliliambia gazeti hili jana kuwa bei ya mafuta haijapanda kwa kiwango cha kusababisha viwango vya nauli kubadilika.
“Viwango vya nauli haviwezi kupanda kwa sababu, hatutegemei bei za mafuta kuendelea kupanda,” alisema Sekilasa.
Alisema pia kuwa sababu nyingine ni wastani wa asilimia saba iliyotangazwa kuachwa na Ewura ili kufanya mabadiliko ya bei ya mara kwa mara ili yasivuruge kwa kiasi kikubwa bei za nishati hiyo nchini.
Wakati huo huo, wadau wa sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam jana walikutana kujadili viwango vipya vya nauli ya wanafunzi.
SOURCE : MWANANCHI

No comments:

Post a Comment