.

.

.

.

Tuesday, July 21, 2009

ATM BONGO ZAWINDWA NA MAHARAMIA

Siku moja tu baada ya Jeshi la Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam kufanikiwa kuwanasa wazungu wawili waliotaka kukomba kiujanja mamilioni ya pesa katika ATM, leo tena kuna mijizi imefumwa ikitaka kukomba tena mapesa.
Taarifa ambazo zimezipatikana ni kwamba mijizi hiyo, ilikaribia kukomba pesa katika ATM za mabenki mawili maarufu pale katika maeneo ya Posta Jijini kabla ya jaribio lao hilo kuzimwa tena na Polisi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ni kwamba, kwa kutumia janja kama ile ya wazungu wa Bulgaria walionaswa jana, mijamaa hiyo ilikaribia kukomba tena pesa, lakini taarifa zikafika polisi na mara moja, kikosi cha askari shupavu wa jeshi hilo kikatua haraka kwenye eneo husika na kuifanya mijizi itimke kimyakimya.

Hata hivyo, akizungumza leo asubuhi kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema ni kweli kulikuwa na taarifa za wizi mwingine katika ATM mbili za eneo la Posta Jijini, maeneo ya jirani na Jengo la Mavuno.
Akasema baada ya polisi kupokea taarifa hizo, polisi wenye silaha waliwahi mara moja katika eneo la tukio.
"Tuko makini. Wakati wote tunapopata taarifa sahihi za tukio huwa tunawahi na ndivyo ilivyokuwa leo asubuhi... vijana waliwahi kwenye ATM hizo, lakini wakakuta kuko shwari," akasema.
"Huenda walijaribu au walikimbia baada ya kutuona tumefika kwa wakati... lakini tunachoshukuru ni kwamba ATM zote za eneo husika zilikuwa salama. Tunaomba wananchi waendelee kutupa ushirikiano na bila shaka tutaendelea kukomesha vitendo vya uhalifu Jijini," akasema Kamanda Kova.
Jana, Polisi Jijini waliwatia mbaroni wazungu wawili, raia wa Bulgaria kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kukomba mapesa kwenye mashine hizo za kutolea fedha (ATM).
Habari hizo za kipolisi zilidai kuwa hadi wakikamatwa, wazungu hao wawili walikuwa tayari wameshajichotea jumla ya shilingi milioni 70 kutoka kwenye akaunti za watu mbalimbali Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment