.

.

.

.

Saturday, July 11, 2009

MH.MWAGUNGA AWEKWA KITIMOTO NA MH.KILANGO


Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela(kulia pichani), amelipua bomu bungeni jinsi uzembe wa Wizara ya Maliasili na Utalii unalipoteza serikali mapato katika wizi wa nyara na anakusudia kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili iundwe kamati teule ya kuchunguza hali hiyo.
Alisema hawezi kukubali kuona Watanzania wanaibiwa mali zao na kupelekwa nje ya nchi huku wao wakiendelea kubaki maskini.
Kusudio la kuwasilisha hoja hiyo alilitoa jana, wakati akichangia mjadala wa bajeti ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha wa 2009/2010 yaliyowasilishwa na (Kushoto pichani).Waziri wake, Shamsa Mangunga
“Mheshimiwa Spika, naomba kupitia kanuni ya 117 nitoe kusudio langu la kuleta hoja binafsi ya kuundwa kamati teule juu ya suala hili,” alisema.
Hoja ya Kilango inafuatia wizi wa makontena mawili ya nyara za serikali yaliyokamatwa nchini Vietnam na kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.
“Nilikuwa nawasiliana na Vietnam na nimefanya utafiti nina faili zima…zilifikaje kontena kule.
“Sikufanya utafiti wa kitoto… nimefanya kazi. Majina ya walipeleka makontena hayo ninayo sina sababu ya kuyataja kwa sababu serikali inayajua.”
Alisema utafiti wake umegundua kuwa kontena zilipitia bandari ya Tanzania na zilipofanyiwa ukaguzi zikaonyesha kuwa ndani kulikuwa na plastiki zilizorudufiwa (re-circled plastics).
Hata hivyo, alisema yalipotiliwa mashaka na kufanyika tena ukaguzi, yalikutwa yakiwa yamejaa pembe za ndovu.
Kilango alilihakikishia Bunge kuwa watu waliohusika na kusafirisha makontena hayo ana majina yao lakini alisema hawezi kuwataja bungeni.
“Kama kuna ufisadi unaua nchi hii ni huu,” alisema Kilango huku akimuomba Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuwa kama angeruhusiwa kuongezewa dakika tano angelia kwanza kutokana na ufisadi unaofanyika nchini.
Alizitaja nchi zinazoongoza kwa kupokea nyara za serikali kutoka Tanzania kuwa ni Phillipines, China, Singapore, Vietnam na Hong Kong.
Kilango alisema wizi wa aina hiyo unafanyika huku kukiwa na watendaji ambao hawafuatilii, matokeo yake wanaharibu jina la serikali na Chama Cha Mapinduzi.
“Rais wetu anasafiri nje ya nchi kila siku kuomba pesa, lakini pesa zetu zimelala kwenye makontena,” alisema.
Alisema Tanzania haistahili kuwa maskini wakati nchi imejaliwa na Mungu kwa rasimali za kutosha, alihoji wizara imeshindwa vipi kulinda mali ya Watanzania na kusababisha pesa zao kulala Vietnam.
Kutokana na kukerwa na hali hiyo, Kilango aliwataka wabunge kusoma kitabu alichokuwa nacho na kukionyesha ndani ya ukumbi huo kilichokuwa na jina la “Concession of economic hitman”. Alisema kuwa kitabu hicho kinaeleza kwa undani jinsi rasilimali za nchi zinazoendelea zinavyoporwa.
Aliwataka Watanzania kusoma kitabu hicho ili wawe na ujasiri wa kufuatilia mambo ya kifisadi.
Kilango alisema mwenyezi Mungu ameishushia Tanzania rasimali ya kutosha akitaka watu wake wale mpaka mwisho wa maisha yao, lakini hazitawasaidia kama hazitatunzwa. “Rasilimali zetu hazitatusaidia kama hatutakuwa makini,” alisisitiza.
Spika wa Bunge, akijibu hoja ya Kilango, alisema kwa mujibu wa kanuni aliyoomba Mbunge anaruhusiwa kuleta hoja binafsi na kuomba asubiri kwanza majibu ya serikali.
Mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo (Chadema), alilalamikia vivutio vya utalii nchini kutelekezwa na kuikosesha mapato serikali.
Alitoa mfano wa hoteli ya Moshi ambayo imeachwa kwa miaka 20 bila kufanyakazi na njia za kupandia mlima wa Kilimanjaro, kuachwa bila kufanyiwa ukarabati.
Aidha, alitahadharisha bei kubwa zinazotozwa kwenye hoteli za kitalii nchini kuwa zinafukuza watalii.
“Tusifikiri watalii wote ni matajiri wengine ni malofa wanasafiri kwa travelers cheque (hundi za kusafiria),” alisema.
Ndesamburo, aliitaka pia serikali kuangalia mikataba mibaya inayoingia na wawezekaji na kutoa mfano wa Kiwanda cha Sao Hill ambacho alisema wawekezaji wa Kenya wanavuna mbao za Tanzania na kumaliza misitu ya nchi huku kwao ikishamiri.
Mbunge wa Vunjo (CCM), Aloyce Kimaro, alilalamikia misamaha ya ada zinazotozwa ndani ya hifadhi za taifa.
Alisema katika miaka iliyopita serikali ilikuwa ikitoza asilimia nne kwa kila kitanda ambacho analala mgeni. Lakini baadaye Tanapa ilikaa na wamiliki wa hoteli ikaona kuwa ilikuwa inapoteza mapato na kukubaliana kuwa kuanzia mwaka 2008 iongeze kwa asilimia 25 ambapo serikali ingepata dola milioni 30.
Hata hivyo, kwa sababu ambazo hazifahamiki wageni waliendelea kulipa kati ya dola nne na sita kwa kitanda pamoja na wamiliki wa hoteli kukubali kuongeza kiwango.
Kimaro alihoji ni sababu zipi zilizofanya kushusha kiwango hicho kutoka dola 25 hadi kinacholipwa sasa.

No comments:

Post a Comment