.

.

.

.

Wednesday, July 01, 2009

MKOA MAALUMU WA KIJESHI KUUNDWA !!!!!

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameupa uongozi wa Mkoa wa Mara muda wa miezi sita kuanzia leo ili kuwasilisha mpango mkakati wa kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika Wilaya za Tarime na Rorya, vinginevyo serikali italazimika kuunda mkoa maalumu wa kijeshi katika wilaya hizo.
Akihutubia wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya serikali za mitaa kilichofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Mukendo mjini hapa, Waziri Mkuu alisema mapigano yanayoendelea katika wilaya hizo, yanatia aibu huku serikali ya Mkoa ikiwa imenyamaza bila kuonyesha namna yoyote ya kutatua tatizo hilo.

Pinda alisema endapo uongozi wa mkoa utashindwa kuliondoa tatizo hilo katika kipindi hicho, serikali italazimika kuunda mkoa maalumu wa kijeshi na kwamba utaongozwa na Jenerali wa jeshi.
Alisema lengo kuunda utawala wa aina hiyo ni kurejesha amani miongoni mwa Watanzania.
Pinda alizitaka Halmashauri za wilaya hizo mbili kutokwepa jukumu la kudumisha amani na aliwataka watendaji wengine wilaya hizo, kushiriki kikamilifu katika kumaliza tatizo hilo.
“Ni jukumu la serikali za mitaa kukuimarisha amani na utulivu katika maeneo yao, zikiwemo Halmashauri za Tarime na Rorya, hivyo hakikisheni mnarejesha amani hiyo katika maeneo yenu vinginevyo tutazifuta,” alisema Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu hadi kufikia jana maiti 32 zilikuwa zimeokotwa porini, nyumba 400 zimechomwa moto huku watu 3000 wakikosa mahala pa kuishi kufuatia mapigano yaliyozuka Juni 25, mwaka huu kati Wajaluo walioko wilayani Rorya na Wakurya wilayani Tarime baada ya kuibiana mifugo.
Mapigano hayo yalianza Juni 25, mwaka huu na kuhusisha wakazi wa kata za Kitenga na Kwisarara, ikidaiwa kusababishwa na wizi mkubwa wa mifugo, unaofanywa na makabila ya Wakurya na Wajaluo.
Kutokana na hali hiyo, timu ya viongozi wa ngazi ya taifa, akiwamo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hamis Kagasheki, Kamishna wa Polisi Kitengo cha Operesheni Taifa, Paul Chagonja, IGP Said Mwema na maofisa kadhaa wa polisi mkoani Mara, walilazimika kwenda eneo la mapigano hayo kwa helikopta.

No comments:

Post a Comment