.

.

.

.

Saturday, July 04, 2009

MSICHANA ALBINO AUWAWA MWANZA

Msichana Jesica Charles (23) ambaye ni albino, mkazi wa Igoma, jijini Mwanza, amekutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa katika mapango ya mlima Kishiri eneo la Igoma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jamal Rwambow, alisema ofisini kwake jana kuwa mwili wa Jesica, ulikutwa ukiwa hauna baadhi ya viungo na hivyo tukio hilo kuhusishwa na imani za kishirikina.
Alisema kabla ya kukutwa na mauti, Jesica aliondoka nyumbani kwao Juni 21, mwaka huu na kuaga kuwa anakwenda katika mahubiri yaliyokuwa yakifanyika jirani na nyumbani kwao.
Hata hivyo, alisema hakurejea nyumbani hadi siku iliyofuata jioni ambapo baba yake, Charles Joshua (50), alipoamua kutoa taarifa polisi akiamini kwamba ametoroshwa na mwanamume.
Alisema sababu ya baba huyo kuhisi kuwa binti yake ametoroshwa na mwanaume inafuatia harakati za msichana Steri Chenja (19) kuwa karibu na marehemu na kuonyesha kila dalili za kumtafutia wanaume.
“Huyu baba wa marehemu alipokuja kutoa taarifa hakuwa na wazo kwamba binti yake ameuawa isipokuwa aliamini kuwa amekwenda kwa mwanaume ambaye alitafutiwa na Steri,” alisema Kamanda Rwambow.
Kufuatia taarifa hizo, Kamanda Rwambow alisema polisi walifanya msako na kuwakamata watu watatu ambao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo kwa namna moja ama nyingine.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Steri Chenja, mkazi wa kijiji cha Mbiti Bariadi mkoani Shinyanga, Vumilia Julius (35), mkazi wa Igoma na Melkiadi Christopher (27), anayeaminika kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu.
Kwa mujibu wa Kamanda Rwambow, baada ya kukamatwa, Steri alikiri kumtafutia Jesica mwanaume aliyemtaja kuwa ni Melikiadi Christopher lakini alikana kuondoka naye wakati akirejea kwao Bariadi.
Aidha, alisema kwa upande wake alipohojiwa Melikiadi alikiri kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Jesica na kwamba kwa mara ya kwanza walikutana kimwili Juni 16, mwaka huu na walikuwa wamekubaliana tena Juni 20 au 21, mwaka huu.
Aliongeza kwamba, Jeshi la Polisi pia lililazimika kumkamata Vumilia Julius au Mama John ambaye ni jirani kutokana na kuanzisha uhusiano wa karibu na Jesica kabla ya kifo chake.
"Tulilazimika kumkamata pia Vumilia kutokana na taarifa kwamba aliwahi kuhojiwa na mama wa Jesica sababu za kuwa karibu na binti yake, naye akajibu kwamba kwa nini hataki binti yake apate wanaume,” alisema.
Kamanda Rwambow alisema mwili wa Jesica umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando baada ya kuokotwa ukiwa umeharibika vibaya na kwamba uchunguzi zaidi wa mauaji hayo unaendelea.


Chanzo : NIPASHE

1 comment:

  1. Wana kitu cha kutueleza, how comes wote majirani na shoga walikuwa busy kumtafutia mwanaume, then jamaa kala mzigo mara moja na mtoto amepota, na ndio tarehe walikuwa warudie gemu??? Rwambowe hao wabanwe, na CID waendelee kuchunguza kama kunayejificha nyuma ya pazia hili

    ReplyDelete