.

.

.

.

Tuesday, August 18, 2009

SPIKA SITTA MOTONI DODOMA

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, jana jioni alilazimika kuwaomba radhi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kunusurika na hatari ya wazi ya kupoteza uanachama iliyoanza kujionyesha tangu juzi jioni.
Hatua hiyo ya Sitta kuomba radhi ilikuja baada ya wajumbe takriban wote wa vikao viwili vya juu vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) vya chama hicho kujenga hoja za kumshambulia wakipinga namna anavyoliendesha Bunge katika mwelekeo wa kukidhalilisha chama hicho na serikali yake.
Habari za uhakika kutoka ndani ya vikao hivyo vilivyokuwa vikifanyika katika Ukumbi wa Mlimani mjini hapa tangu juzi, zinaeleza kwamba, takriban wajumbe wote waliokuwa wakisimama kuzungumza katika vikao hivyo walikuwa wakitaka kuona Sitta akipokonywa uanachama wa chama hicho, ili liwe fundisho kwake binafsi na wana CCM wengine.
Taarifa kwamba Sitta angeomba radhi zilianza kusikika tangu jana asubuhi baada ya wajumbe kadhaa wa vikao hivyo kuieleza Tanzania Daima kwamba spika huyo alifanya kikao na Rais Kikwete kabla ya NEC kuanza.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho cha siri kati ya rais na Sitta zinaeleza kwamba, mwenyekiti huyo wa CCM alimtaka kiongozi huyo kutafakari kwa makini tuhuma zote zilizokuwa zikielekezwa kwake na kutoa utetezi ambao utamuepusha katika hatari ya kupokonywa kadi ya uanachama na hatimaye uspika wake.
“Kuna taarifa kwamba Rais Kikwete alipokutana na Sitta leo asubuhi (Jumatatu), alimuomba kiongozi huyo atumie busara kulimaliza suala hilo ambalo hatima yake ingeweza kuwa mbaya,” alisema mjumbe mmoja.
Tukio hilo baya kabisa kuwahi kumfika Sitta ambaye amekuwa akijinadi kuwa ni spika wa kasi na viwango, lilihitimishwa na uamuzi wa NEC kuunda kamati maalumu kuchunguza kiini cha kufikia hapo.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo vya CCM, zinaeleza kuwa, kamati hiyo maalumu itaongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na wajumbe wake wengine watakuwa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Pius Msekwa na mwanasiasa mkongwe, Abdulrahman Kinana.
Kwa mujibu wa habari hizo, mwelekeo wa wana CCM hao kutaka kumwadhibu Sitta ambaye katika siku za hivi karibuni amejizolea umaarufu wa kisiasa ndani na nje ya Bunge, hata kuwa na uwezo wa kumnyoshea kidole mtu au taasisi yoyote, ulianza kujitokeza tangu katika Kamati Kuu juzi.
Hali hiyo ya mambo, ilimlazimu Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuwaomba wajumbe wa CC, wamruhusu kuipeleka ajenda hiyo ya Sitta katika kikao cha NEC kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa uamuzi.
Mjadala huo ulipoanza ndani ya NEC, wajumbe takriban wote waliokuwa wakizungumza walionekana kumshutumu Sitta wakihoji namna anavyoliendesha Bunge katika misingi isiyozingatia taratibu na kanuni za mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola.
“Jana na leo ni siku mbaya na ngumu kwa Sitta, kwani kati ya wajumbe zaidi ya 40 waliozungumza, ametetewa na wajumbe watatu tu, ambao wote waliposimama kuzungumza walikuwa wakizomewa hata kusababisha mwenyekiti kuingilia kati na kutaka hali ya utulivu,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye alionekana dhahiri akiwa upande uliokuwa ukimshambulia spika huyo.
Habari zaidi zinasema, mjumbe mmoja alisimama na kumshutumu Sitta kuwa ndiye chimbuko la kuongezeka kwa ufa wa makundi ndani ya chama hicho, kutokana na tabia yake ya kuliendesha Bunge akiwa ameambatana na kundi moja la wabunge wanaomuunga mkono.
Mjumbe huyo (jina tunalo), alifikia hatua ya kusema Sitta ameanzisha kikosi cha wabunge wake (aliowaita first 11) ambao siku zote amekuwa akiwapanga kuzungumza wakiwalenga watu fulani na wakati mwingine kuirarua serikali bungeni kwa sababu tu ya kutimiza malengo yao binafsi.
Mbali ya huyo, mjumbe mwingine kati ya wajumbe zaidi ya 50 waliozungumza tangu juzi, alifikia hatua ya kufananisha mashambulizi hayo na kitendo cha wawindaji kumjeruhi nyati na kumwacha pasipo kumuua kabisa, akisema ni cha hatari kwa maisha ya wawindaji.
Wajumbe wa NEC waliozungumza na Tanzania Daima wanasema, mjumbe huyo alifikia kutoa matamshi hayo, lengo likiwa ni kukitaka kikao hicho cha NEC kuhitimisha mjadala mzima wa juzi na jana kwa kumpokonya kadi ya uanachama kiongozi huyo.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, mjumbe mwingine aliyekuwa akiunga mkono hoja hiyo alifikia hatua ya kusema, CCM haiwezi kutikisika iwapo Sitta atapokonywa uanachama, akisema katika wakati tofauti chama hicho kimepata kupoteza makada maarufu katika siku zilizopita.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, makada wengine wa chama hicho aliokuwa akiwazungumzia walikuwa ni aliyekuwa Makamu wa Rais, Aboud Jumbe, ambaye mwaka 1984 alivuliwa wadhifa wake na NEC, baada ya kuvuja kwa taarifa zilizokuwa zikimhusisha na mipango ya kuudhofisha muungano.
Mwingine aliyetajwa katika kundi hilo ni Maalim Seif Sharif Hamad na wana CCM wengine 16 wa Zanzibar ambao walivuliwa uanachama mwaka 1988, wakituhumiwa kukihujumu chama hicho na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kada wa tatu wa chama hicho aliyelazimika kukihama chama hicho akiwa na umaarufu aliyetajwa na mjumbe huyo kuwa mfano wa watu walioondoka CCM na kukiacha kikiendelea kuwa imara, ni Augustine Mrema, ambaye aliondoka mwaka 1995 kutokana na kuhitilafiana na serikali na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Cleopa Msuya, akamshauri rais amfukuze kazi.
Wakati mjumbe huyo akitoa matamshi hayo, mjumbe mwingine aliitaka NEC kutohofia uamuzi wa kumvua Sitta uanachama, akitaka wajumbe wajifunze kutoka nchini Afrika Kusini ambako chama tawala kilifikia hatua ya kumvua madaraka rais wa nchi (Thabo Mbeki) na bado kikajihakikishia ushindi uchaguzi mkuu ulipoitishwa tena.
Mjumbe mwingine wa CC na NEC aliyezungumza na Tanzania Daima jana alisema, mwelekeo wa vikao hivyo, zilikuwa ni salamu tosha kwa Sitta na makamanda wenzake wa ufisadi wakati huu chama hicho kinavyojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwakani.
“Huyu jamaa (Sitta) na wapambe wake wamekuwa wakikivuruga chama na serikali ndani na nje ya Bunge kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, kwa kisingizio cha ufisadi. Leo hii wamejionea wenyewe namna damu ya watu waliowaonea kama Edward Lowassa na wenzake inavyowalilia,” alisema mjumbe huyo aliye karibu kimtazamo na waziri mkuu huyo aliyejiuzulu Februari mwaka jana baada ya jina lake kuhusishwa katika sakata la Richmond.
Wakati mjumbe huyo akitoa maoni hayo, mwingine aliyezungumza na gazeti hili alisema, mtiririko mzima wa hoja ndani ya vikao hivyo, unaonyesha namna kundi moja la watu wenye fedha lilivyojipanga kuhakikisha linammaliza Sitta kwa kutumia kila mbinu.
Hata hivyo, habari zaidi kutoka ndani ya vikao hivyo zinaeleza kwamba, kikubwa kilichoonekana kumfikisha Sitta hapo alipo ni namna ambavyo amekuwa akilishughulikia sakata la Richmond na mengine yanayohusu ufisadi ndani na nje ya Bunge.
Baadhi ya wajumbe waliozungumza na Tanzania Daima ambao walieleza kutoridhishwa na namna suala la Sitta lilivyoshughulikiwa, walisema kwa jinsi mjadala ulivyokuwa ukienda, wachangiaji wote ni kama vile walipangwa kummaliza Sitta, kwa madai kuwa amekuwa akiruhusu mijadala inayokimaliza chama kwa hoja ya kupambana na ufisadi.
Wajumbe hao walielezea wasiwasi wao kuwa endapo Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Kikwete angekubaliana na matakwa ya wajumbe wengi ya kutaka Sitta apokwe uanachama, hali hiyo inaweza kuibua tatizo kubwa, si nchini tu, bali pia kimataifa.
Nje ya Ukumbi wa White House ambako mkutano huo ulikuwa ukiendelea, vikundi vya baadhi ya wajumbe walionekana kutofautiana kuhusu suala hilo, kwa madai kuwa limeibuliwa kwa makusudi na watu wachache wenye ushawishi kifedha ili kupunguza makali ya Sitta.

1 comment:

  1. na ccm ikitaka kuanguka 2010 wamtoe sitta. yani wao wanaona kunyonya w2 ndo vizuri ,sasa tutapambana. ccm umaarufu wake umeisha kabisa. wakitaka kupata kura za kishindo kama za mwaka 2000 basi wamuweke waziri mkuu aliyoko sasa kugmbea. lowasa na watoto wake wanakula raha sisi tunalala njaa, eti wanamuonea huruma,kwanza mwakani wabunge wengi wa CCM watakosa ubunge labda kama wakiiba kama kawaida yao. CCM, CCM nini bwana, hawana utu viongozi wake kazi kufuata mkumbo natamani kuwatoa wote,yapo tu,viongozi gani hawa, kujisahau na kukutunyonya ila siku ipo watakufa mmoja mmoja, na maisha yataendelea. nini wanachokifanya kizuri anaetenda haki anauawa, anae ua watu anathaminia.uu ndo ujumbe wa CCM.tumechoka, tumechoka kabisa,tutaunana kama mbeya na tarime, hawapati kitu

    ReplyDelete