.

.

.

.

Tuesday, September 22, 2009

MAMBO SI SHWARI UNGUJA

AMANI katika Visiwani Zanzibar, inazidi kuwa tete hasa kufuatia vurugu zilizozuka jana na kulilamizimisha Jeshi la Polisi kurusha mabomu ya kutoa machozi kutoka kwenye helikopta yake, ili kuwatawanya watu waliokuwa wakifanya vurugu katika vituo kadhaa vya kujiandikisha katika Daftari la Wapiga kura.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema vurugu hizo zilizuka saa 6:00 mchana, katika kisiwa kidogo cha Tumbatu, kilichoko katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako maafisa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), walikuwa wanaandikisha watu.
Inadaiwa kuwa jeshi hilo lilimau kutumia helikopta kurusha mabomu ya kutoa machozi, baada ya kushindnwa kuwatawanya wananchi hao kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi ya kurushwa kwa mkono na risasi zilizofyatuliwa hewani.
"Lengo lao lilikuwa kuwatawanya wananchi waliokuwa wametanda katika kituo hicho ili kushinikiza waandikishwe katika daftari hilo licha ya kwamba hawakuwa na vitambulisho vya makazi hapa Zanzibar, "alidai mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Alisema kabla mabomu ya kurushwa kwa helikopta, polisi walipambana na wananchi ambao hata hivyo hawakuonyesha kutishika na kutii amri ya kuwataka waondoke.
"Baadaye tukaona helkopta ya polisi ikipita juu na kuanza kumimina mabomu ya mchozi iliyowafanya wananchi wote wakimbie vituo,"alidai shuhuda huyo.
Alisema wakati helkopta hiyo inakaribia katika eneo hilo ambalo wananchi walikuwa wamejikusanya, ilishuka chini umbali wa takriban mita 15 na kuanza kumimina mabomu yaliyowatawanya wananchi hao.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo,Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Msellem Masoud Mtulya alisema mabomu hayakutoka kwenye helkopta ilipita angani wakati askari wakirusha mabomu hayo kwa mkono.
Awali, Kamanda Mtulya alisema hakuwa na taarifa kuhuu matukio hayo kwa sababu alikuwa jijini Dar es Salaam.
Habari zaidi zilisema wananchi wengi waliokuwa walioelekezewa mabomu walitawanyika kwa hofu huku wakiangua vilio na kwamba baadhi yao walikuwa wamekanyagwa baada ya kuanguka chini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mzanzibari hataruhusiwa kuandikishwa katika daftari hilo kama hana kitambulisho cha ukazi wa Zanzibar.
Hata hivyo, wakati mabomu hayo yakitumika kuwatawanywa wananchi katika kituo cha Tumbatu, hali iliendelea kuwa tete katika kijiji cha Kichangani baada ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa vyama vya CCM na CUF kupambana kwa mawe na silaha nyingine za kienyeji.
Taarifa zilisema vurugu hizo ziliibuka baada ya wafuasi wa CUF kuwazuia wenzao wa CCM, waliotaka kujiandikisha katika kituo hicho.
"Si kwamba hatutaki wao waandikishwe, lakini kwa nini wao tu ndio wawe wamepewa vitambulisho, Sisi sote na watoto wetu hatujapewa Zan ID, kwani sisi si Wazanzibari na wao tu ndio Wazanzibari?" alihoji mmoja mtu aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Ame.
Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim, alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba jana ilikuwa katika mapumziko.
Habari tulizopata wakati tunakwenda mitamboni, zilisema Kituo cha Uandikishaji cha Skuli ya Jongowe ,kililazimika kufungwa kutokana na wananchi kususia.
Kutoka Wete Pemba, Salma Said, anaripoti kuwa siku mbili baada ya CCM kuipongeza ZEC kwa kuendelea na kazi ya uandikishaji wa wapigakura katika visiwani humo, tume hiyo imesema hairidhishwi na zoezi hilo kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.
Taarifa iliyosambazwa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Afisa Habari wa ZEC, Idrissa Haji Jecha imesema zoezi hilokatika Mikoa ya Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba, halikutoa mafanikio yaliotarajiwa.
"Takwimu zonaonyesha kuwa wapigakura walioandikishwa Kaskazini Pemba ni 852 na Unguja ni watu 7,634," ilisema taarifa hiyo.
Tangu zoezi hilo lianze Septemba 12 mwaka huu uandikishaji umekuwa wa kudorora hasa katika kisiwani Pemba ambako wananchi wengi wamekosa kwenda kujiandikisha kwa madai ya kutokuwa na vtambulisho vya Uzanzibari, ambavyo ni moja ya sifa za kuandikishwa katika daftari hilo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa zoezi hilo limefanikiwa kidogo katika siku mbili za mwisho mkoani wa Kaskazini Unguja ambako idadi ya watu waliojitokeza, iliongezeka ikilinganishwa na awali.
Imesema katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, idadi ya watu wanaojitokeza na kujiandikisha bado ni ndogo licha ya tume hiyo kutumia ushawishi wa kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi.
Akizungumza na Mwananchi, Afisa Uchaguzi wa ZEC, Bakari Suleiman, alielezea kuridhishwa kwake kuhusu kurejea kwa amani katika vituo mbali mbali vya uandikishaji wapigakura katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
"Kwa kweli mimi binafsi nimerishishwa sana na hii hali ya amani ya leo (jana) tukilinganisha na siku za nyuma ambapo mabomu na maji ya kuwasha yalitumika kutawanya wananchi," amesema Suleiman.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi, amesema hali ya usalama imeimarishwa na fujo zimepungua kwa kiasi kikubwa.

CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment