.

.

.

.

Friday, October 09, 2009

KESI YA EPA YASIMAMISHWA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa mara nyingine imetoa amri ya kusimamisha kesi ya wizi wa sh bilioni 3.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) inayomkabili mfanyabiashara maarufu, Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel na wenzake watatu, hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao Mahakama Kuu itakapomalizika.
Uamuzi huo ulitolewa jana na mahakimu wakazi John Mgeta na Fussi ambao walisema wamekubaliana na ombi la mawakili wa utetezi, Martin Matunda na Mabere Marando lililotaka mahakama hiyo itoe amri ya kusimamishwa usikilizaji wa kesi hiyo hadi kesi ya kikatiba inayoendelea Mahakama Kuu itakapomalizika.
“Tunakubaliana na ombi la utetezi la kutaka kesi hii isimamishwe kwa sababu kuna kesi ya kikatiba inaendelea Mahakama Kuu, na kwa sababu hiyo jopo hili limetupilia mbali pingamzi la upande wa mashitaka lililotaka kesi hiyo isisimamishwe kwa sababu tamko lililotolewa na mdaiwa wa pili, Reginald Mengi dhidi ya washitakiwa halihusiani na kesi hiyo.
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, tumebaini maombi ya upande wa utetezi ni ya msingi, kwani yameegemea kwenye haki za msingi zilizoainishwa kwenye katiba ya nchi, hivyo natoa amri ya kusimamishwa kwa kesi hii na ninaamuru jalada la kesi hii lipelekwe Mahakama Kuu ili liweze kutumika kwenye kesi hiyo ya kikatiba,” alisema Hakimu Mgeta.
Kesi hiyo ya kikatiba ambayo inasikilizwa na majaji watatu wanaoongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, inaendelea kusikilizwa ambapo upande wa walalamikaji na wadaiwa wameishawasilisha utetezi wao na imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 2 mwaka huu. Majaji wengine ni Geofrey Shahidi na Semistocles Kaijage.
Katika kesi hiyo, Jeetu na wenzake wanamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mengi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwamba kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya mdaiwa wa pili (Mengi) kuwahukumu kupitia vyombo vya habari.
Juni 4, mwaka huu, Jeetu na wenzake walifungua kesi hiyo ya kikatiba Na. 30 wakiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya ibara 13, kifungu 4, 5 na 6 (b) cha katiba ambacho kinatamka watu wote ni sawa mbele ya sheria na pia itafsiri ibara 13 (6) (b) inayosema mtu yeyote asichukuliwe ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.
Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanadai kuwa wamefikia uamuzi huo wa kuiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara hizo za katiba kwa kuwa wanaamini zimevunjwa na Mengi ambaye Aprili 23, mwaka huu, alitumia vyombo vya habari kuwahukumu kwa kuwaita ‘Mafisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi zao haijatoa hukumu.
Uamuzi huo ni wa pili kwani juzi mahakama hiyo ilitoa amri ya kusimamishwa kuendelea kwa kesi ya wizi wa sh bilioni 9 inayowakabili washitakiwa hao hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao itakapotolewa uamuzi.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka jana.
Mbali na Jeetu, washitakiwa wengine ni Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady na Ketan Chohan.

No comments:

Post a Comment