VILIO, mayowe na simanzi jana vilitawala katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa mwanasiasa mkongwe na mmoja wa waasisi wa taifa, Mzee Rashid Mfaume Kawawa.
Rais Jakaya Kikwete, aliwaongoza wanafamilia, viongozi mbalimbali na mamia ya wananchi kuuaga mwili wa Mzee Kawawa majira ya mchana katika ukumbi huo.
Kawawa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Makamu wa Kwanza wa Rais na mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa taifa hili, alifariki dunia juzi asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa ghafla akisumbuliwa na maradhi ya kisukari na figo.
Mwili wa marehemu uliokuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo, uliwasili kwenye viwanja vya Karimjee saa 8:10 mchana, ukiwa ndani ya jeneza lililovikwa bendera ya taifa na kubebwa katika gari maalum la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Ukitokea Lugalo, mwili huo ulipitia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Kinondoni, Jangwani na hatimaye kuingia katikati ya mji, katika msafara uliopambwa kwa magari na pikipiki zaidi ya 60 zilizokuwa zikipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete akiongozana na mkewe, Salma Kikwete, walikuwa wa kwanza kuuaga, wakifuatiwa na wanafamilia wa marehemu, katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa pia na viongozi wengine wakuu wa kitaifa, wakiwemo wabunge, mabalozi, wanasiasa wa vyama vya upinzani, viongozi wa dini na wanaharakati.
Kabla ya tukio la kuuaga mwili wa marehemu, kulifanyika hitma na baadaye mnajimu maarufu, Sheikh Yahya Hussein kumsomea Kuran tukufu, akigusa aya iliyotoa ujumbe kuhusu mauti.
“Aya aliyosoma Sheikh Yahya inahusu suala zima la mauti. Kila nafsi itaonja mauti, lakini kuonja mauti si mwisho wa uhai wa binadamu. Ni hali ya kubadili tu mazingira ya uhai kutoka katika uhai huu na kuingia katika uhai mwingine ambao Mwenyezi Mungu (SW) ameuwekea pazia. Na safari ya uhai huo mpya inaanzia kaburini,” alifafanua mwendeshaji mkuu wa shughuli hiyo, Shaaban Kisu.
Sheikh Mkuu, Mufti Issa bin Shaaban Simba, ndiye aliyeongoza dua ya kumuombea marehemu.
Miongoni mwa viongozi wakuu wa kitaifa walioshiriki shughuli hiyo iliyoanza saa nane mchana, ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid.
Mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu, Salim Ahmed Salim pamoja na waziri mkuu aliyejiuzulu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, nao walishiriki katika shughuli hiyo.
Hata hivyo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa hakuonekana katika shughuli hiyo, kwa sababu ambazo hazikuweza kujulikana mara moja.
Katika hali inayoweza kuibua maswali, kwa kipindi kirefu sasa Mkapa amekuwa akikosekana katika matukio ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya miaka 48 ya Uhuru wa Tanganyika, yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Desemba 9, mwaka jana.
Wengine waliohudhuria jana, ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM Bara), Pius Msekwa, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Sheikh Mkuu, Mufti Simba na aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodius Kilaini.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kyela, Dk. Harrisson Mwakyembe (CCM) na Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (CHADEMA).
Mara baada ya shughuli nzima ya kuuaga mwili wa marehemu kukamilika, mwili huo uliondolewa ndani ya ukumbi huo saa 12 jioni chini ya uangalizi wa askari wa JWTZ, ulipelekwa nyumbani kwake Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Leo mwili huo umezikwa huko Madale saa 7 mchana, katika mazishi yaliyoongozwa na Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment