.

.

.

.

Thursday, February 04, 2010

MAAFA YA JENERETA UNGUJA

WATU wanne wa familia mmoja wamekufa katika eneo la Kibweni Bububu, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, baada ya kuvuta hewa inayosadikiwa kuwa na sumu iliyotokana na moshi wa jenereta.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku katika nyumba inayomilikiwa na Ali Shamsi Salum, ambayo vioo vyake vilifungwa na kusababisha hewa iliyotokana na genereta lenye ukubwa wa KVA 4.1. kuingia ndani na kushindwa kutoka.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai visiwani Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba wakati inatokea, ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na watu sita.
"Watu waliokufa ni wanne, waliofariki watatu walifariki hapo hapo na mmoja wao alifariki katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, alikuwa amepelekwa kwa matibabu," alisema.
Akiwataja walifariki katika ajali hiyo ni pamoja na mke wa mmiliki wa nyumba hiyo, Safia Shaaban Shadadi (51) kaka wa mama huyo Ahmed Shaaban Shadadi (48), mgeni kutoka Canada, Anwar Saleh (26) na mfanyakazi wa ndani, Sikuzani Nassor (18).
Antar ambaye alikuja Zanzibar hivi karibu, alikuwa mbioni kurejea Canada leo.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi, mmiliki wa nyumba hiyo (Ali) amenusurika katika ajali hiyo kwa kuwa alikuwa amelala katika nyumba yake nyingine iliyoko Michenzani, Unguja.
Wengine walionusurika katika ni, Sharifa Ramadhan Mohammed (35) na mtoto wake Nahad Ali Said (12) ambao walikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja kwa matibabu.
Mussa alisema watu hao wamekufa kwa sababu walikosa hewa katika nyumba waliyokuwa wamelala wakati huo genereta likiwa linafanya kazi na kusababisha moshi kushindwa kutoka nje.
Alisema kwa mujibu wa majirani walioingia ndani ya nyumba hiyo ili kuwaisia kuwaokoa watu, waliwakuta wakikohoa kutokana na kuvuta hewa chafu.
Naibu mkurugenzi huyo aliwataka wananchi waepuke kuweka majenereta ndani ya nyumba kwa sababu ni hatari kwa usalama.
Kwa muda sasa, Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na tatizo la kukosekana na huduma za umeme, jambo linalowalazimisha wananchi kutumia majenereta, ili kupata umeme.

1 comment:

  1. Hapa inatakiwa Rais Karume na serikali yake yote wajiuzulu kwani huu ni uzembe kupitiliza nchi inakosa umeme miezi 3, huu ni ujinga na sisi watanzania ujinga ndio jadi yetu sasa tujiulize tutaendelea hivi mpaka lini? Viongozi wetu hawa wanafanya makosa ya makusudi watu wanapoteza maisha kama hivi, malazi yanaongezeka, nk. Umasikini ndio tunaumwagilia maji uneemeke huku baadhi ya hao viongozi wachache wakizidi kuneemeka. Hapa tusishangae ikizuka RICHMOND mpya. Hii ni ujuma ya makusudi ili waje na dili zao chafu kujidai eti wanaokoa jahazi, na wakati huo watu tayari washakua-desparate watawaona kama waungu watu,so people don't fools ourselves let's act now.

    ReplyDelete