.

.

.

.

Thursday, February 11, 2010

RAIS Jakaya Kikwete amekamilisha uteuzi wa nafasi zake 10 za uteuzi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua Jussa Ismail kutoka Chama cha Wananchi (CUF) na Janet Mbene ambaye ni kada wa CCM.


Kabla ya uteuzi wa jana, Rais Kikwete alishateua watu nane kuwa wabunge.
Akitangaza uteuzi huo mara baada ya kumalizika kwa mjadala wa sakata la Richmond bungeni mjini Dodoma jana, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alisema Rais Kikwete amekamilisha uteuzi wa nafasi 10 za ubunge kwa kuteua wabunge wawili.
"Waheshimiwa wabunge kabla sijamwita mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, kuna taarifa hapa, nimepata barua kutoka kwa Mheshimiwa Rais, chini ya Ibara ya 66 (1) ya Katiba mheshimiwa rais, sasa amekamilisha uteuzi wa wabunge," alisema Spika Sitta na kuongeza:
"Alikuwa ameteua wabunge wanane na sasa amekamilisha wabunge wawili nao ni wafuatao; ndugu Ismail Jussa Ladu na Janet Mbene."


Jussa ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CUF na msaidizi maalumu wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif ambapo Mbene aliwahi kugombea nafasi ya ubunge katika Bunge la Afrika ya Mashariki bila mafanikio.


Vilevile, Mbene ambaye amebobea katika masuala ya biashara, amefanya kazi katika mashirika mbalimbali ya kimataifa, ikiwamo Oxfarm.



"Mnaona rais wetu amezingatia 'fifty-fifty' (asilimia 50 kwa 50) ameteua mwanaume mmoja na mwanamke mmoja," alisema Sitta.
Baada ya kutoa taarifa hiyo kutoka kwa rais, Spika Sitta alimtaka Katibu wa Bunge kuandaa utaratibu wa kuwaita wateule hao ili kuapishwa leo kwa kuwa kesho Mkutano huo wa Bunge utafungwa.
"Kwa taarifa hiyo namuomba Katibu wa Bunge utaratibu ufanyike ili, kesho (leo) wabunge hawa waapishwe, kwa sababu keshokutwa (kesho) ni siku ya kufunga Bunge," aliagiza Sitta.
Mwananchi ilimtafuta mbunge mteule Jussa ambapo, alisema alipata taarifa ya kwanza ya uteuzi wake kutoka kwa Mhariri wa Habari wa Gazeti la The Citizen, Peter Nyanje na kudai kuwa alishangaa sana kwa sababu hakutegemea.
"Nilishangaa sana baada ya kupata taarifa kutoka kwa Nyanje kwa sababu sikutegemea na nilimwambia unanitania, lakini akaniambia utanipigia ukithibitisha,"alisema Jussa.
"Lakini baada ya muda mfupi nilipata simu kutoka Ikulu ya Dar es Salaam na kunipa taarifa ya uteuzi huo. Kimsingi nimefurahi kwa imani ya rais kwangu, kwa chama changu na kwa Wazanzibari, ni heshima kubwa niliyopata kwa uteuzi huu."
Jussa aliongeza kuwa, ingawa ameteuliwa huku Bunge likiwa linaelekea ukingoni mwake, lakini, aliahidi kukitumia vizuri kipindi hicho kifupi bungeni kwa maslahi ya wananchi.
Hivi karibuni Rais wa Zanzibar Aman Abeid Karume naye aliteua watu wawili kutoka CUF kuwa wajumbe wa Baraza la Wawikilishi la Zanzibar, ikiwa ni hatua ya maridhiano baina yake na Maalim Seif.

CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment