.

.

.

.

Monday, March 15, 2010

SUMAYE ASEMA HAHUSIKI NA CCJ

WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema: "mimi si CCJ (Chama cha Jamii); siijui na wala sihusiki nayo."

Sumaye alisema hayo baada ya kutakiwa kutoa msimamo wake kuhusu chama hicho ambacho kimekuwa kikihusishwa na makada wa CCM ambao wanapingana na mwenendo wa chama hicho tawala kwa sasa na ambao wanadaiwa kusubiri wakati muafaka wajitangaze rasmi.

"Mimi si CCJ, siijui na wala sihusiki nayo,"alisema Sumaye: Duniani kote wanachama wa chama kilicho madarakani hawampingi rais aliyeko madarakani na ukifanya hivyo unajimaliza kisiasa na mwaka huu sitogombea nafasi yoyote hata ile ya udiwani."

CCJ imekuwa ikikanusha kuhusishwa na vigogo wa CCM, lakini haijaweza kutuliza habari zinazokihusisha chama hicho na makada wa chama hicho tawala.

Tayari vigogo kadhaa wameshakanusha habari za kuhusishwa kwao na CCJ, akiwemo Spika Samuel Sitta, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, mawaziri wakuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na John Malecela.

Kwa sasa CCJ ina usajili wa muda ilioupata Machi 2 na inahaha kusaka angalau wanachama 2,000 kutoka Bara na Visiwani katika kipindi cha miezi sita ili kiweze kupata usajili kamili. Lakini katika muda mfupi, chama hicho kimeshatangaza kuwa kimevuna wanachama 7,700 katika mikoa 11.

Sumaye hakutaka kuzumzia zaidi kuhusu chama hicho ambacho kilitamba kwenye habari kubwa za magazeti mara kabla na baada ya kutangaza rasmi kuanzishwa kwake.

Katika hafkla ya kukabidhi hundi ya Sh5 milioni kwa Jukwaa la Wahariri, Sumaye alizungumzia mambo kadhaa likiwemo suala la mgombea binafsi ambalo linaonekana kupingwa na serikali baada ya Mahakama Kuu kubatilisha sheria inayozuia mgombea wa aina hiyo.

Akizungumzia suala hilo, Sumaye alisema kuwa haoni sababu ya kuzuiwa kwa wagombea binafsi katika uchaguzi.

"Kwa kuwa suala la mgombea binafsi lipo kikatiba, hivyo halina tatizo lolote. Na uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mzuri," alisema Sumaye.

Alisema kinachotakiwa kwa sasa katika suala la mgombea binafsi ni kuwepo kwa sheria ambayo itatumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Kuhusu mpango wa kuwepo kwa sheria ya kutenganisha siasa na biashara pamoja na muswada wa sheria ya udhibiti fedha katika uchaguzi uliopitishwa hivi karibuni na Bunge, Sumaye alisema kwamba nia ya uanzishwaji wa sheria hizo ni njema lakini tatizo litakuwa ni katika utekelezaji wake.

"Nia ya kutaka kuwepo sheria itakayotenganisha siasa na biashara pamoja na kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi ni nzuri, lakini utekelezaji wake utakuwa ni mgumu kulingana na mazingira yalivyo," alisema Sumaye.

Katika utenganishwaji wa siasa na biashara, Sumaye, ambaye aliwahi kushauri wafanyabiashara wajiunge na CCM kama wanataka mafanikio, alisema utekelezaji wa suala hilo utafanikiwa endapo maadili ya Azimio la Arusha yatarudishwa.

'Labda tu maadili ya Azimio la Arusha yarudi ndio tutaweza kutenganisha siasa na biashara," alisema Sumaye.

Akizungumzia makundi ndani ya CCM, Sumaye alisema hali ya kuhitilafiana na kupishana kimtazamo ni lazima iwepo katika masuala ya kisiasa na kwamba matatizo hayo yatakwisha.

"Haya matatizo ya makundi pamoja na mambo mengine ndani ya CCM hayaninyimi usingizi na kwa kuwa CCM ni bingwa wa kutatua matatizo yake, haya yote yatakwisha na tutaingia katika uchaguzi tukiwa pamoja,"alisema.

Kuhusu tuhuma zinazomkabili rais mstaafu Benjamini Mkapa, Sumaye alikataa kusema lolote kwa madai kuwa limekwishatolewa maelezo na Rais Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

No comments:

Post a Comment