.

.

.

.

Sunday, April 18, 2010

SIMBA NA YANGA KUKIPIGA JIONI HII

Simba na Yanga zinapambana leo kwenye Uwanja wa Taifa, ikiwa ni mechi ya 21 ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Simba inaingia uwanjani ikiwa na ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufikisha pointi 56 huku mtani wake huyo, Yanga akiwa na pointi 48. Simba imetwaa ubingwa kwa kuwa hakuna timu inayoweza kufikia.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka hapa nchini, lakini kikubwa ni heshima kwa wachezaji wa timu hizo mbili ingawa ushindani unaweza kuwa baina ya Mussa Hassan Mgosi na Mrisho Ngassa wanaowania tuzo ya mfungaji bora.

Pamoja na matokeo yoyote ya mchezo huu kutokuwa na athari katika msimamo wa ligi Yanga wameahidi kutibua furaha ya Wanamsimbazi hao kwa kuhakikisha wanashinda ili kuweza kudhihirisha ubabe wao.

Yanga haijaifunga Simba kwa muda mrefu kwenye mechi za ligi isipokuwa mwishoni mwa mwaka jana, Desemba 24, ilipoifunga timu hiyo mabao 2-1 katika michuano ya Tusker.

Simba itaingia uwanjani bila ya kocha wake, Mzambia Patrick Phiri ambaye yupo nchini kwake akiuguliwa na mwanaye, lakini wamejipanga vema katika mchezo huo na kujipa matumaini ya kufanya vizuri.

Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Selemani Matola amepewa mikoba ya kuinoa timu hiyo akisaidiana na Amri Said. Matola alikuwa akiinoa Simba U-20 akisaidiana na Madaraka Seleman kabla ya kuchukuliwa na African Lyon.

Simba imepania ushindi mchezo leo, kwani Phiri alisema raha ya ubingwa itahitimishwa kwa kuifunga Yanga.

Ukiachilia kutibua chereko za Simba za ubingwa, Yanga itataka kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Oktoba 31 mwaka wakati huo Kostadin Papic alikuwa ndiyo kwanza anaanza kuitumikia Yanga.

Lakini anafahamu raha ya kuifunga Simba kwani aliichapa timu hiyo katika michuano ya Tusker kwa kuifunga mabao 2-1

Katika mchezo wa leo, Simba itakuwa ikiangalia muunganiko wa Mgosi, Emmanuel Okwi, Hillary Echessa na Ulimboka Mwakingwe katika safu ya ushambuliaji wakati Uhuru Suleiman, Mohamed Kijuso watakuwa wakisubiri.

Kwenye kupandisha mashambulizi, Mohamed Banka na Ramadhani Chombo 'Redondo' watakuwa na kazi hiyo wakati katika ngome pembeni wanatarajiwa kuwepo Juma Jabu na Salum Kanoni.

Pia katikati wapo Juma Nyosso, Kelvin Yondan na Joseph Owino huku langoni akitarajiwa kusimama Juma Kaseja.

Kwa upande wa Yanga, safu ya ushambuliaji itaongozwa na Ngassa, Jerry Tegete na Boniface Ambani wakiunganishwa na Kiggi Makasi na Geofrey Bonny pamoja na Shadrack Nsajigwa na Amir Maftah wanaopandisha mipira pembeni.

Ngome itaongozwa na Nadir Haroub 'Cannavaro' pamoja na Wisdom Ndhlovu wakati langoni anatarajiwa kusimama, Obren Curkovic.

Ngassa na Mgosi ambao wana mabao 14 kila mmoja wanawania kuondoka Sh2,000,000 za ufungaji bora.

Baada ya mchezo huo, timu hizo zitakuwa zimebakiwa na mchezo mmoja, Simba dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro wakati Yanga itapambana na Prisons kwenye Uwanja wa Uhuru Jumatano.

No comments:

Post a Comment