.
.
Monday, June 21, 2010
WAGOMBEA URAISI WA ZANZIBAR KUTOKA CCM KUCHUKUA FOMU LEO
LEO ni leo ambapo macho na masikio ya Watanzania, yanaelekezwa Zanzibar wakati wanachama sita wa CCM, watakapochukua fomu za kuomba wateuliwe kugombea urais wa visiwa hivyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.Hali hiyo inajitokeza huku Mohamed Aboud, akiweka bayana kwamba atachukua fomu za kuwania nafasi hiyo na kukanusha propaganda zinazodai kwamba amejitoa ili kumuunga mkono Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein.
Tayari baadhi ya wagombea wameanza kutamba na kuahidi kuzungumza na waandishi wa habari leo baada ya kuchukua fomu.
Wagombea watarajiwa walitoa ahadi hiyo ni Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha ambaye atachukua fomu saa 3: 00 asubuhi na atazungumza na waandishi katika Hoteli ya Bwawani.
Hali kadhalika, Dk Mohamed Ghalib Bilal na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna, watakaozungumza katika Hoteli ya Ocean View na Ali Karume aliyepanga kukutana na waandishi katika Hoteli ya Serena, iliyoko Mji Mkongwe.
Ratiba iliyotangazwa juzi na CCM Zanzibar, kupitia Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya chama hicho, Vuai Ali Vuai, ilisema jumla ya wagombea sita watachukua fomu leo katika Ofisi Kuu ya Kisiwandui, huku wapambe na shamrashamra katika ofisi za chama, zikipigwa marufuku.
Aboud akifafanua anataka kuifanyia nini Zanzibar, kama atakuwa Rais, alisema kwanza amejipanga vema kuhakikisha kuwa umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa visiwa hivyo, unaimarishwa na kwamba amejipanga vema kuwa rais bora wa Zanzibar, kama CCM itampitisha katika kura za maoni na kisha kuchaguliwa na wananchi.
"Jambo kubwa linalohitaji Zanzibar ni mkakati wa haraka wa kujenga umoja, Zanzibar ikiwa na umoja itapiga hatua za haraka katika maendeleo....., tutaweza kujenga uchumi imara na kuweka miundombinu yake," alisema Aboud, baada ya kuulizwa anataka kuifanyia nini Zanzibar.
Naibu waziri huyo mwenye dhamana ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema ikifikia hatua Zanzibar ikawa na umoja,huo utakuwa ni ukombozi mkubwa kwa visiwa hivyo kwani itachangia kwa kasi maendeleo yake.
"Tunahitaji kujenga uchumi, huduma bora za afya na miundombinu ya kisasa.Ninachoamini mimi haya yote ni rahisi kuyafanikisha kama tutakuwa na umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari," alisisitiza Aboud.
Aboud akidokeza hayo, kwa upande wake Balozi Karume, juzi alinukuliwa akisema Watanzania waelewa kwamba, hii ni mara yake ya kwanza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar na itakuwa ni ya mwisho pia iwapo hatapata ridhaa ya wananchi.
"Lazima watu wafahamu hivi ni vitu viwili tofauti wakati ule wa mwaka 2005 nilichukua fomu kuwania urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sasa nachukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar hii ni mara yangu ya mwanzo,lakini pia itakuwa ni mara yangu ya mwisho kama nitakuwa sijapata ridhaa mimi sifanyi marejesho," alisema Balozi Karume.
Akielezea kilichomsukuma kuchukua fomu ya urais wa Zanzibar, Balozi Karume alisema kwanza ni haki yake ya kikatiba lakini pia ushauri aliopewa na wataalamu na marais wastaafu ambao wamemwambia kuwa ni yeye pekee atakayeweza kuiendeleza Zanzibar kimaendeleo.
"Mimi nimeshauriwa na watu mbalimbali tena wakubwa tu wa nchi hii wengine wasomi, marais wastaafu, wanawake na hata vijana na wamenitaka nichukue fomu kwa kuwa wanaamini mimi naweza kuwa Rais wa Zanzibar, lakini pia wameniambia kuwa mimi naweza kukabiliana na mgombea yeyote wa upinzani," alisema balozi huyo wa Tanzania nchini Italia.
Akifafanua, alisema wazo la kutaka kuwania nafasi ya urais alikuwa nalo tangu mwaka 2000 lakini kutokana na sababu zake mbalimbali, alishindwa kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, aliahidi kumuunga mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa na chama chake ikiwa mchakato wa kumteua hautokuwa na mizengwe wala rushwa.
"Kama sipata, nitamuunga mkono mtu mgombea yeyote atakayeteuliwa na chama changu lakini awe amepita bila ya mizengwe yoyote, bila ya kutoa rushwa, na bila ya fitna na majungu hapo mimi nitamuunga mkono ikiwa atateuliwa," aliahidi.
Kwa mujibu wa katibu wa itikadi wa CCM hakutaruhusiwa shamrashamra zozote wakati wa uchukuaji fomu wala kwenda na wapambe katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Kwa upande wake, waziri Suleiman alisema "mimi ndio mimi nipo katika mchakato na natarajia siku ya Alhamisi kwenda kuchukua fomu na bila ya shaka nitakuwa mimi peke yangu siku hiyo."
Alielezea matumaini makubwa ya kupata ridhaa ya chama chake na kumpitisha katika mchakato wa kura za maoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment