TAARIFA KWA UMMA
USAJILI WA NAMBA ZA SIMU ZA MKONONI
1. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa agizo kuwa namba
zote za simu za mkononi zisajiliwe kati ya Julai 1 2009 hadi
Desemba 31, 2009; na baadaye muda huo kuongezwa hadi tarehe
30 Juni 2010 ikitamkwa wazi kuwa muda huo wa ujasili
hautaongezwa tena. Sababu za kuanzisha utaratibu wa kusajili
namba za simu zimeelezwa mara kadhaa zikiwemo:
(i) Kuwalinda watumiaji dhidi ya matumizi mabaya ya huduma za
mawasiliano
(ii) Kuwezesha na kurahisisha utambuzi wa wateja watumiapo
huduma mbalimbali kama M – Pesa, Z-pesa, ZAP na huduma
nyingine za malipo ya Ankara kama za Umeme, Maji,
Televisheni n.k.
(iii) Kuimarisha usalama wa nchi.
(iv) Kuyawezesha makampuni ya simu kuwafahamu wateja wao
vizuri zaidi ili kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma
kwao.
2. Wakati tunakaribia tarehe 30 Juni 2010, utaratibu umepangwa
kupitia Makampuni ya simu kuwa kuanzia tarehe 1 Juni 2010
kuhakikisha laini yoyote itakayonunuliwa itatumika kwa kupiga au
kupokea simu na kutuma au kupokea ujumbe ikiwa imesajiliwa
tu na si vinginevyo.
2
3. Baada ya saa sita usiku tarehe 30 Juni yaani saa 00.00 kuanzia
tarehe 1 Julai, 2010 namba yoyote ambayo itakuwa haijasajiliwa
itafungiwa kupiga ,kupokea simu pamoja na ujumbe wa maandishi
(SMS) kwa siku 90 hadi tarehe 30 Septemba 2010. Katika kipindi
hiki cha siku 90 endapo mtumiaji ataisajili namba yake
itafunguliwa. Kwa namba ambazo hazitakuwa zimesajiliwa ifikapo
tarehe 30 Septemba zitafutwa na kuondolewa kwenye mitandao
kabisa.
4. Mamlaka ya Mawasiliano imekubaliana na Makampuni ya simu
kufanya uhakiki wa usajili wa laini za simu za wateja kwa kutumia
namba 106 kupitia simu za mkononi. Kwa wateja wa mitandao
iliyoko katika mifumo ya GSM, kama Zain, Vodacom, MIC (Tigo) na
Zantel, wateja wanatakiwa kuingiza *106# na kwa wateja wa
mitandao inayotumia mfumo wa CDMA kama BOL, TTCL mobile na
SASATEL wateja watatakiwa kupiga namba 106 na watapokea
taarifa za usajili.
5. Hivi karibuni mswada wa sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na
posta ulipitishwa na Bunge kuwa sheria. Sheria hiyo inafanya usajili
wa namba za simu za mkononi kuwa ni wa lazima kwa mujibu wa
sheria hio kuanzia sasa na kutofanya hivyo ni kosa la jinai. Adhabu
ni pamoja na faini au kifungo au vyote pamoja.
6. Mamlaka ya Mawasiliano inapenda kuyashukuru makampuni ya simu
na watumiaji kwa ushirikiano ambao wameonesha mpaka sasa kwa
ajili ya kufanikisha zoezi hili.Tunawasihi wote waendelee kusajili
laini mpya kabla ya matumizi baada ya tarehe 30 juni 2010 na
kuendelea kuhakiki laini zote zilizosajiliwa ili kukamilisha usajili
kama ilivyokusudiwa.
Imetolewa na
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA
No comments:
Post a Comment