.
.
Wednesday, August 11, 2010
CCM VUGUVUGU LA JOTO
MAANDAMANO, urudishwaji wa kadi na vurugu zimeendelea kutawala maeneo mbalimbali nchini kutokana na wanachama kupata taarifa kutoka ndani ya vikao vya kamati za siasa za mikoa za CCM zinazoonyesha kuwa baadhi ya wagombea walioibuka washindi wamewekewa alama za chini au kuondolewa na kurejeshwa wale walioshindwa.
Kamati hizo zinachambua washindi wa kura za maoni za ubunge na udiwani na kuweka alama kwa wagombea ili kuiwezesha kamati kuu ya CCM kutoa orodha ya mwisho ya wagombea ambao hawatakuwa na matatizo wakati Tume ya Uchaguzi itakapotoa orodha ya majina ya waliopitishwa kugombea nafasi hizo.
Lakini uchambuzi huo wa kamati za siasa unaonekana kukera wanachama, hasa waliowapigia kura baadhi ya wagombea walioibuka kidedea kwenye kura za maoni, ambao sasa wanaendelea kuandamana na kuzingira ofisi za CCM kupinga maamuzi hayo.
Tayari katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati ameshatetea maamuzi hayo ya kamati za siasa akisema kuwa wale watakaobainika kucheza rafu wataenguliwa, huku makamu mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Bara, Pius Msekwa akisema kuwa watakaobainika kusababisha kukithiri kwa vitendo vya rushwa hawatapona.
Rushwa iliripotiwa kwa wingi wakati wa kampeni huku ukiukwaji wa taratibu ukijitokeza wakati wa kupiga kura, ikiwa ni pamoja na kuibuka kwa wanachama wapya, kutokuwepo kwa leja za wanachama na vurugu zilizosababisha baadhi ya vituo kutokuwa na upigaji kura.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kutoka maeneo mbalimbali nchini, wanachama hao wakiwa katika makundi waliandamana maeneo mbalimbali, kurudisha kadi, kutishia kuwapigia kura wagombea wa vyama vya upinzani na wengine kutishia kuhamia upinzani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment