.

.

.

.

Friday, August 20, 2010

JK AMTETEA MWANAE

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa, Rais Jakaya Kikwete amesema hana tatizo na wanachama wa chama hicho wanaohamia vyama vingine,lakini wasijaribu kukihujumu.

Kikwete amesisitiza kuwa,walioenguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wataelezwa kwa maandishi sababu za kuenguliwa.

Aidha amesema,mwanawe Ridhiwani hahusiki katika sakata la kuenguliwa kuwania ubunge Jimbo la Nzega, Hussein Bashe kama ilivyoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari.

Rais Kikwete aliyasema hayo Dar es Salaam kwenye Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, wakati akiwahutubia mamia ya wanachama wa chama hicho mara baada ya kurejesha fomu zake za kuwania Urais kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema,wakati wa kura za maoni, wengi walijitokeza kugombea, lakini lazima mmoja ashinde na wengine washindwe, lakini wapo waliogombea kwa kutaka washinde wao na hao ndiyo ambao sasa wanahamia vyama vingine.

“Katika uchaguzi lazima mmoja ashinde. Tatizo kuna wagombea waliingia katika ushindani ili wao tu washinde, hiyo ndiyo sababu ya kutaka kuhama…anayehamia kwingine sina haja naye, aende anakotaka, mbaya ni kukihujumu chama,” alisema Rais Kikwete jana.

Alisema hata kama aliyegombea hakuridhishwa na mazingira ya namna aliyeshinda alivyoshinda, ndiyo ameshapata,hivyo jambo la msingi ni kuacha makundi yaliyokuwepo wakati wa kura za maoni, bali wajielekeze katika kutafuta ushindi wa kishindo huku wakijiandaa kwa kugombea kipindi kingine.

Kikwete alisema,utaratibu huo wa kura za maoni utaendelea ingawa mchakato ulikuwa na changamoto mbalimbali ambazo wamejifunza na kuwahakikishia kuboresha mapungufu yaliyojitokeza ili yasitokee na wanaendelea kuzichambua kasoro hizo na baada ya uchaguzi watazifanyia kazi.

”Pamoja na mapungufu yaliyojitokeza, mamlaka tuliyowapa wanachama wa CCM hatutawanyang’anya, ila jukumu ni kurekebisha kasoro zilizojitokeza kwani imesaidia kuwapata wagombea wanaohitajika huku wakijitokeza wanachama wengi kugombea nafasi mbalimbali,” alisema.

Kuhusu Bashe, Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisema kuenguliwa kwa kijana huyo kulifanywa na Kamati Kuu ambayo ilifanya hivyo kwa manufaa ya chama.

Alisema Kamati Kuu hiyo ilijitahidi kuheshimu uamuzi ya wanachama wake, lakini kutokana na sababu mbalimbali kama uraia na utovu wa maadili ambao ungesababisha chama hicho kuanguka katika jimbo husika, walimteua wanayeona anafaa.

Alisema kuna magazeti yanasema maneno mengi ili wanachama wa chama hicho wachukiane na yakishindwa kuona mema ya chama hicho kwa mwaka mzima.

Aliwaomba Makamu wake, Pius Msekwa na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba kuacha kujibizana katika magazeti, badala yake, majibu yatapatikana katika kura baada ya CCM kushinda kwa kishindo.

Bashe ambaye alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), alienguliwa na Kamati Kuu baada ya kubainika kuwa si raia wa Tanzania, na kutakiwa na NEC kuanza mchakato wa kupata uraia. Anadaiwa kuwa raia wa Somalia na alivuliwa uanachama na kupoteza nafasi zote za uongozi.

Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuenguliwa kwa Bashe aliyeongoza kwa kura zaidi ya 14,000 dhidi ya wagombea wengine wawili, Lucas Selelii na Dk. Hamis Kigwangala, kumetokana na tofauti zake na Ridhiwani ambaye kama Bashe ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM.

Aidha, Rais Kikwete aliwataka wana-CCM kutoa jasho katika kutafuta ushindi kwa kupita nyumba kwa nyumba, chumba kwa chumba na hata mtu kwa mtu kuwashawishi wananchi watatu wasiokuwa mwanachama wa chama hicho kupigia kura CCM, hivyo kati ya wanachama milioni tano waliopo, kila mmoja akiwa na watatu, watakuwa wamepata kura milioni 15 ambao ni ushindi wa kishindo.

Mgombea Mwenza wa Rais Kikwete kwa chama hicho, Dk. Mohamed Gharib Bilal, alisema wamemaliza awamu ya kwanza ya kutimiza masharti kikatiba, sasa wanaanza awamu nyingine kuelezea sera ya chama chao hivyo, aliwataka wanachama kujitokeza katika uzinduzi wa kampeni wa chama hicho
.

No comments:

Post a Comment