MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa anadaiwa kuwa alifahamu kuwa, Josephine Mushumbusi, ni mke wa mtu licha ya kuendelea kuzini naye.
Madai hayo yametolewa na mume wa ndoa wa Josephine, Aminiel Mahimbo, katika hoja
yake aliyowasilisha katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, akijibu hoja za Dk Slaa.
Mahimbo katika kesi hiyo dhidi ya Dk Slaa anadai malipo ya Sh bilioni moja za fidia ya kudhalilishwa na mgombea huyo wa urais ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema.
Katika hoja yake Mahimbo anadai kuwa si kweli kwamba Dk Slaa hakuwa anajua kwamba
Josephine ni mkewe wa ndoa, hivyo kuendelea kumtambulisha kuwa ni mchumba wake hata
katika majukwaa ya kisiasa.
Aidha, alidai kuwa baada ya kumtambulisha mwanamke huyo kuwa mchumba wake, habari
hiyo ilinukuliwa na karibu vyombo vyote vya habari vya magazeti na televisheni; na kwamba uhusiano wao ni wa uzinzi.
Mahimbo alidai pia kuwa pamoja na Dk Slaa kujua kuwa Josephine ni mkewe wa ndoa bado ameendeleza uhusiano naye.
Alipinga maombi ya Dk Slaa kuitaka mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo kwa madai kuwa
haina msingi kwa sababu mdai alijidhalilisha mwenyewe kwa kukubali kutumiwa na chama
(hakukitaja) kutoa habari hizo kwenye vyombo vya habari na kukubali kuhama nyumbani
kwake kwenda kuishi kwa mwanamke ambaye ni kiongozi wa chama hicho.
Pia alikanusha hoja ya Dk Slaa aliyodai kwamba kwa mlalamikaji kutoa habari hizo kwenye vyombo vya habari, ni wazi kuwa hana maadili na hivyo mahakama hiyo imwamuru
alipe gharama za kesi hiyo.
Dk Slaa katika hoja zake, alidai kuwa hakujua kuwa Josephine ni mke wa mtu na kwamba hata yeye hakuwa amemweleza kuwa ameolewa na kwamba taarifa hizo kwa mara ya kwanza alizisikia kwenye vyombo vya habari.
Mahakama ilipanga Oktoba 15 pande hizo zikutane ili kupanga namna ya uendeshaji wa kesi
hiyo.
Mahimbo anadai Septemba 7,2002 alifunga ndoa na Josephine huyo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Kijitonyama na kuishi maeneo mbalimbali ikiwamo Kimara Baruti, Dar es Salaam.
Mahimbo alidai alishangaa kusikia mkewe ananadiwa na Dk Slaa katika majukwaa ya siasa kuwa ni mchumba wake.
Anadai pia kuwa katika ndoa wamebahatika kupata watoto wawili; Upendo aliyezaliwa Mei
Mosi, 2003 na Precious wa Machi 14, 2007. Mahimbo alidai, ndoa kati yake na Josephine haijavunjwa na chombo chochote na bado ni mkewe halali.
Mlalamikaji huyo alidai, uhusiano uliopo kati ya watu hao wawili umemfanya adhalilike na
kunyanyasika katika jamii na kuiomba Mahakama imzuie Dk. Slaa kuendelea kujihusisha na
mkewe.
Katika madai yake, aliambatanisha cheti cha ndoa yao, picha za harusi, vyeti vya kuzaliwa watoto na nakala za vipande vya magazeti vyenye picha zilizopigwa wakati Dk. Slaa akimtambulisha.
No comments:
Post a Comment