.

.

.

.

Tuesday, October 19, 2010

WACHEZAJI YANGA KUPEWA DONGE NONO

Jerry Tegete



SIKU chache baada ya kuilaza Simba, uongozi wa klabu ya Yanga unakutana leo kujadili jinsi ya kuwagawia Shilingi 50 milioni wachezaji wake huku ukiwaondoa hofu na kuwataka watulie wakati wakiandaliwa mazingira mazuri ya kukabidhiwa vitita vyao.

Zawadi hizo zilitokana na ahadi, mchango wa wadau na ushindi wa bao 1-0 uliopatikana Jumamosi dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Hata hivyo, uongozi huo umedhamiria kukabidhi kitita hicho kimya kimya ili kuwaepusha wachezaji hao na usumbufu unaoweza kujitokeza.

Klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani na Twiga chini ya uongozi wa wakili Lloyd Nchunga uliwaahidi wachezaji hao Shilingi 40 milioni kama watafanikiwa kuifunga Simba.

Mshambuliaji Jeryson Tegete ndiye aliyepachika na kuipa ushindi wa 1-0 dhidi ya wapinzani wao na hivyo kujihakikisha kifuta jasho hicho.

Akizungumza na Mwananchi jijini jana, ofisa habari wa Yanga, Luis Sendeu alisema hakuna tatizo lolote linalohusu malipo ya wachezaji kwa sababu zoezi hilo linashughulikiwa na muda wowote kuanzia sasa watakabidhiwa pesa zao.

‘’Tuliwaahidi wenyewe na tutawapa kiasi hicho kama ilivyopangwa, lakini kimya kimya bila watu kujua ili kuwaepushia usumbufu, hatutaki wachezaji wetu wasumbuliwe hata kidogo si unajua tena watu wakijua wanazo we...’’alisema Sendeu.

Aliongeza : ‘’Bado uongozi unashughulikia zoezi hilo la malipo na watakabidhiwa muda wowote kuanzia sasa."

Hata hivyo, Sendeu alisema timu hiyo imeanza maandalizi tangu jana kujinoa kwa mchezo ujao Alhamisi dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Aidha, uongozi wa klabu hiyo utakutana leo kufanya tathmini ya mechi yao dhidi ya Simba.

Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisema jana kuwa mbali ya tathmini hiyo watajadili mgao wa fedha za wachezaji baada ya awali kuwaahidi wachezaji wao milioni 40, lakini baadaye wadau walijiotokeza waliongeza dau hilo mpaka kufikia milioni 50, hivyo ni vyema wakawagawia kama walivyowahaidi.

Alisema kuwa awali walisema kila mhezaji atapata milioni moja huku benchi la ufundi wakipata Sh700,000 kila mmoja na kocha wao Kostadin Papic akipata milioni 1.5, lakini kutokana na kuongezeka kwa fedha zilizochangwa na wadau kila mchezaji atapata zaidi ya walichoahidi awali.

Nchunga alisema kitendo cha kuingia madarakani na kuifunga Simba inaonyesha ushujaa wao na mshikamano walionao wa kuakikisha wanaipeleka Yanga kwenye mafanikio makupwa na kuyaendeleza yale walioachiwa na Iman Madega.

Aliongeza kuwa baada ya kumaliza mchezo huo wa Simba kamati yao inakutana leo ili kujadili mchezo huo na mchezo mingine iliyobaki ili kuhakikisha timu yake haipotezi mchezo hata mmoja.

'' Ni lazima tuanze kujipanga mapema kuhakikisha tunachukua ubingwa mapema kwani pointi tulizowaacha watani wetu siyo nyingi, hivyo ni lazima tuakikishe hatupotezi mchezo hata mmoja,'' alisema Nchunga.

Alisema michezo miwili iliyopo mbele yao kati ya JKT Ruvu Jumatano na Azam ni migumu sana, hivyo ni kuhakikisha wanafanya vizuri hivyo wanatakiwa kuanza kujipanga mapema.

Katika hatua nyingine, mshambuliaji Jerryson Tegete amesema kitu pekee kinachomsaidia mara kwa mara kumfunga kipa Juma Kaseja ni utulivu na kujiamini kila anapopata nafasi.

Tegete ambaye katika mchezo wa Jumamosi alishuhudia Kaseja huyo huyo akizima juhudi zake za kuandika bao la kipindi cha kwanza, aliiambia Mwananchi jana jijini Dar es Salaam kuwa licha ya ubora alio nao Kaseja kwenye Ligi Kuu amekuwa na bahati ya kumfunga na ataendelea kumfunga.

"Nafikiri kitu ambacho mshambuliaji mzuri anatakiwa kuwa nacho ni utulivu na kujiamini pindi anapopata nafasi kwenye eneo la hatari licha ya kujua kuwa mabeki wapo kwa ajili ya kuondoa hatari lango kwao na ndiyo siri yangu kubwa kumtungua Kaseja kila mara,"alisema Tegete.

Alisema atakuwa hawatendei haki wenzake wote katika kikosi cha Yanga wanaompa ushikiano mkubwa na kuongeza kama wataendelea na ushirikiano huo, basi ataibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Hadi sasa, Tegete ndiye anaongoza kwa ufungaji wa mabao Ligi Kuu akiwa ameshazifumania nyavu mara tano baada ya mechi saba za ligi hiyo akifuatiwa na mfungaji bora wa msimu uliopita, Musa Hassan Mgosi mwenye magoli matatu.

*Imeandaliwa na Doris Maliyaga, Clara Aphonce na Calvin Kiwia
KIANZILISHI: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment