.

.

.

.

Thursday, January 27, 2011

MTANZANIA AFUNGWA MAISHA KWA UGAIDI

MFUNGWA wa kwanza katika jela ya Guantanamo kushtakiwa kwenye mahakama ya kiraia, Ahmed Ghailani, ambaye ni raia wa Tanzania, amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Mahakama ya Jimbo la Manhattan baada ya mwaka jana Ghailani kutopatikana na hatia katik
a kesi ambayo alishtakiwa kwa mauaji pamoja na mashtaka mengine kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 1998 katika balozi za Marekani mjini Nairobi, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania.

Hata hivyo, pamoja na mwaka jana kukutwa bila hatia katika makosa hayo, jopo la majaji hata lilimkuta na hatia ya kufanya njama ya kuharibu majengo ya serikali.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, upande wa mashtaka ulijaribu kumshawishi jaji kwamba Ghailani alipaswa kuonewa huruma kwa sababu hakujua kuhusu njama hiyo.

Mbali na kutofahamu kuhusu njama hizo upande huo wa utetezi vile vile ulisema kuwa, Ghailani aliteswa na makachero wa CIA baada ya kukamatwa.

Hata hivyo, pamoja na utetezi huo,waendesha mashtaka walitaka apewe kifungo cha maisha gerezani huku wakisisitiza kuwa alijua kuhusu njama hizo.

Akijiandaa kutoa hukumu yake, Jaji Lewis Kaplan alisema ilikuwa siku ya haki kwa jamii za watu 224 waliofariki kwenye mashambulizi ya mabomu ya mwaka wa 1998 pamoja na wale wote waliojeruhiwa.

Jaji Kaplan alisema aliridhishwa na ushahidi aliopata kwamba Ghailani alijua kwamba watu wangekufa kutokana na vitendo vyake.

“Uhalifu huu ulikuwa ni wa kutisha na kwamba yalikuwa ni mauaji ya umwagaji damu baridi yaliyosababisha vifo vya watu wasio na hatia kwa kiasi kikubwa sana,” alisema Jaji Kaplan.

Kwa upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eric Holder, alisema kifungo cha maisha kwa Ghailani kinaonyesha uwezo wa mfumo wa sheria za Marekani kuwakamata magaidi kuwajibika kwa matendo yao.

“Ni matumaini yetu hiki kifungo cha maisha kitaleta baadhi ya kipimo cha haki kwa waathirika wa mashambulizi ambao walisubiri muda mrefu kwa ajili ya siku hii,” alisema katika taarifa yake.

Ghailani alikamatwa nchini Pakistan mwaka 2004 na kupelekwa kwenye kambi ya siri inayosimamiwa na shirika la Ujasusi la Marekani, CIA kabla ya kupelekwa Guantanamo Bay, Cuba, mwaka 2006.Baada ya kusota kwa muda mrefu,baadaye alihamishwa hadi mjini New York ambako alishitakiwa na hatimaye kuhukumiwa.

No comments:

Post a Comment