WADAU wa kilimo cha pamba nchini wakiwamo wamiliki wa vinu vya kuchambulia wameshitakiwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya Pamba mjini Liverpool, Uingereza, baada ya kushindwa kutekeleza mikataba waliyofunga na wanunuzi wa nje kutokana na kukosa pamba na wako hatarini kufilisiwa.
Kutokana na unyeti wa suala hilo, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi)
amewasilisha ombi rasmi kwa Katibu wa Bunge kuhusu kusudio lake la kutaka kuwasilisha hoja binafsi kuhusu pamba.
Machali akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam , alisema amewasilisha ombi kwa hati ya dharura na uharaka, ili aweze kuwasilisha hoja yake baada ya kuibuka ghafla kwa hoja hiyo kutoka kwa wakulima wa pamba na wamiliki wa vinu vya pamba.
“Kama mnavyofahamu, Bunge linakutana Dodoma, kwa hiyo kama suala hili halitashughulikiwa mkutano huo, kuna hatari wakulima wakasusia pamba msimu huu na wamiliki wa vinu wakafilisiwa baada ya kufunguliwa kesi za madai dhidi yao katika Mahakama ya Kimataifa ya Liverpool,” alisema.
Machali alisema alipata malalamiko kutoka kwa wakulima na wamiliki wa vinu kuwa zao hilo liko hatarini kuangamia na kwamba taarifa za kuaminika zinasema mwaka jana uzalishaji wa zao hilo ulianguka kwa zaidi ya asilimia 30, badala ya kuzalishwa tani 260,000 za mbegu ya pamba zilizalishwa 160,000, huku pamba ikiadimika kwa kiwango kikubwa na wakulima kupata hasara.
Kwa mujibu wa Machali, taarifa zinaonesha zaidi ya vinu 38 vinadaiwa na wanunuzi wa pamba wa nje na vingi vimeshitakiwa vikidaiwa si chini ya Sh bilioni 10.
Mbunge huyo alisema Serikali inawajibika kutoa maelezo ya kutosha kuhusu kiini cha kuanguka kwa pamba kwa kile alichoeleza kuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Bodi ya Pamba, hazijawajibika kuwasaidia wakulima na wamiliki wa vinu ambao ni wadau muhimu katika sekta hiyo ya pamba.
Kwa mujibu wa Machali wanasheria wao wameanza kuchunguza kuhusu suala hilo ili kuona nani awajibishwe vipi kutokana na tatizo hilo linalokabili sekta hiyo muhimu.
“Nataka nikaihoji Serikali kwa niaba ya wadau hawa wa pamba na kufahamu itawasaidiaje watu hao na kuwasaidia kuwaokoa kulipa deni hilo la mabilioni ya fedha … nafanya yote kwa maslahi ya Taifa ndio maana nataka kwenda kuhoji bungeni,” alisema.
Machali alisema jambo la msingi ni kuona Serikali inatoa tamko gani kunusuru hali hiyo na kuhakikisha wakulima wa pamba na wamiliki wa vinu hivyo vya pamba wanatendewa haki na kubainisha kuwa baadhi ya wanunuzi wa nje, wamekuwa wakitoa hata vitisho kwa wamiliki wa vinu vilivyoshindwa kutekeleza mikataba waliyofunga nao.
Katika hatua nyingine, NCCR-Mageuzi imesema inaendelea kusubiri Chadema kuwapa jibu iwapo imekubali ombi lao la kutaka kuunda kambi moja rasmi ya upinzani.
Hata hivyo, Machali alisema wabunge wa NCCR-Mageuzi wataendelea kufanya kazi zao hata kama watakuwa nje ya kambi rasmi ya upinzani na kuongeza kuwa wanasubiri kujibiwa, kwani si suala la kulumbana ila kukubaliana.
Machali alisema anaamini nguvu ya wabunge wa vyama vya upinzani kuungana na kuwa na kambi moja rasmi ni muhimu kwani kwa pamoja wanaweza kusimamia hoja na kuitetea kwa maslahi ya wananchi.
Mbunge huyo pia alikanusha NCCR-Mageuzi kushinikizwa na Chama cha Wananchi (CUF) kutaka kujiunga na CHADEMA ili kuunda kambi moja na kubainisha kuwa wabunge wa chama chake kila mmoja anajitegemea kimawazo ila wanaamini wabunge wa upinzani wakiwa na kambi moja rasmi watakuwa na nguvu ya pamoja bungeni kutetea hoja kwa maslahi ya umma
No comments:
Post a Comment