.

.

.

.

Wednesday, February 23, 2011

ALBINO ALIEPOTEA APATIKANA MSITUNI

MTOTO mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Juma Kapela (3) aliyekuwa ameibwa tangu Jumatano iliyopita wilayani Mpanda mkoani Rukwa, amepatikana akiwa hai, lakini akiwa amechanjwa chale mwili mzima na ametelekezwa msituni.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay, jana alithibitisha kupatikana kwa mtoto huyo na kumpokea ofisini kwake, lakini akiwa amechanjwa chale mwili mzima, kutokana na kile kinachoaminika kuwa ni imani za kishirikina na jitihada za kumdhuru kushindikana.

Njoolay alisema alimpokea Juma na dada yake ambaye pia ni albino, Wande Kapela (5), ambao walikuwa wamefuatana na bibi yao ambaye pia ni mlezi wao, Maria Elias (60) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Naomi Nnko.

Juma na dada yake, Wande, wamekuwa wakilelewa na bibi yao kijijini Itunya kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda, na Juma aliliripotiwa kuibwa Jumatano iliyopita na mtu asiyefahamika kwa kile kinachodaiwa ni imani za kishirikina.

Mkuu wa Mkoa alisema awali mkoa ulipendekeza kuwa watoto hao wapelekwe kuishi kwenye Shule ya Msingi ya Malangali mjini hapa pamoja na wenzao ambao ni albino, lakini baada ya kubaini kuwa bado ni wadogo haikufanyika hivyo lakini sasa wamekubaliwa na wataishi kwenye nyumba ya watoto yatima mjini hapa ya Mt Martin de Pores iliyopo Katandala.

“Hii ni faraja kubwa, hata Waziri Mkuu Pinda nilipomfahamisha kuhusu kupatikana kwa Juma akiwa hai, alisema tu ‘Mungu ni Mkubwa’. Nimekuwa nikimjulisha kuibwa kwa mtoto huyu tangu Jumatano iliyopita.

Pia nimeendelea kufanya hivyo hadi alipopatikana akiwa hai juzi, na leo muda mfupi ujao nitamtaarifu kuwa watoto hawa sasa wataishi na kutunzwa kwenye nyumba hiyo ya watoto yatima,” alisema Njoolay.


Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, kupatikana kwa Juma kunatokana na msako mkali uliofanywa siku nne mfululizo ukijumuisha Jeshi la Polisi , Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi wa maeneo ya vijiji vilivyopo si tu mwambao wa Ziwa Tanganyika bali pia wilayani Mbozi, Mbeya.

Akizungumza kwa Kiswahili kidogo huku akichanganya na Kisukuma, bibi wa watoto hao, Maria, alidai kuwa amekuwa akiishi na kuwatunza watoto hao tangu miaka miwili baada ya baba mzazi wa watoto hao aitwaye Kwangulija Kapela kumtelekeza mama wa watoto hao na kwenda kuishi Urambo, Tabora.

Alisema baba huyo ambaye ni mwanawe, alimtelekeza mkewe, Mbaru Busagija, akimtuhumu kumzalia mfululizo watoto albino ambapo alidai kuwa uzazi wa watoto hao umetia nuksi familia yao. Mama yao huyo ameolewa na anaishi pia Urambo .

Akielezea mkasa huo, bibi alisema siku ya tukio, Juma alikuwa na dada yake Wande karibu na nyumba yao wakati yeye amekwenda kutafuta mboga ndipo alipotokea mtu wasiyemfahamu na kuwafukuza na kumkamata Juma na kutoweka naye.

“Nilipojulishwa kuibwa kwa mjukuu wangu nililia sana ndipo majirani walipokuja na kwenda kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji ambao waliitaarifu Polisi na msako ukaanza,” alisema bibi huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Isuto Mantage, alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo na kwamba msako wa kumtafuta mtuhumiwa unaendelea.

No comments:

Post a Comment