SERIKALI itagharimia maziko ya marehemu wote wa ajali ya milipuko ya makombora katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyopo Gongo la Mboto nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete akitoa taarifa maalumu kuhusu ajali hiyo kwa Taifa Februari 17, alisema Serikali imeamua kugharimia maziko ya marehemu wote ikiwemo kuwasafirisha popote ndugu zao watakapoamua wakazikwe.
Sambamba na hatua hiyo, Rais Kikwete alisema pia ndugu wa marehemu watapewa kifuta jasho na kwa wale waliojeruhiwa katika maafa hayo, Serikali itagharimia matibabu yao na watakapotoka hospitali watapewa kifuta jasho kutokana na ulemavu waliopata.
Rais Kikwete aliagiza Kamati ya Maafa ya Mkoa kwa kushirikiana na Kitengo cha Maafa cha Taifa kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu, itawahudumia wananchi waliopoteza makazi yao au waliokimbia makazi yao kwa nia ya kuokoa maisha yao.
Pia aliagiza wananchi hao wapatiwe makazi ya muda pamoja na huduma za malazi, chakula, maji, afya na usafi wa mazingira.
Kwa mujibu wa maagizo ya Rais Kikwete, Kamati ya Maafa ya Mkoa inapaswa kutengeneza utaratibu mzuri wa haraka iwezekanavyo ili wananchi hao warejee makwao waendelee na shughuli zao za kawaida kwa kuwa hakuna hatari tena ya milipuko.
Aliagiza kamati hiyo na Kitengo cha Maafa cha Taifa kuzitambua mapema iwezekanavyo nyumba zilizoharibiwa, wenye nyumba na kuhakikisha uthamini unafanyika ili walipwe fidia wanayostahili bila kuchelewa.
Kamati hiyo kwa kushirikiana na Polisi imetakiwa iwatafute watoto waliopotea na kuwaunganisha na familia zao na kuongoza, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa maziko, matibabu kwa majeruhi na huduma kwa waliohama makazi yao.
Katika hatua nyingine, aliwapongeza viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Bohari Kuu ya Dawa kwa kuhakikisha dawa na vifaa vya tiba vinapatikana na kuokoa maisha na kuwapunguzia machungu wananchi waliojeruhiwa.
Alisema Baraza la Usalama lililoketi juzi kumshauri, liliagiza Jeshi lifanye uchunguzi wake wa ndani wa chanzo cha ajali hiyo kama Sheria ya Ulinzi wa Taifa inavyoagiza na kuomba vyombo vingine vya ulinzi na usalama visaidie katika uchunguzi huo.
Pia baraza hilo liliamua kuwa, Serikali ya Tanzania iombe nchi rafiki zisaidie katika uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo na kushauri namna bora zaidi ya kuimarisha usalama na uhifadhi wa mabomu na risasi katika maghala ya hapa nchini.
Rais Kikwete alisema ajali hiyo ni janga ambalo pamoja na kusikitisha, limeleta uchungu hasa kwa kuwa limetokea ikiwa ni miaka miwili baada ya janga la Mbagala.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali imeamua kulishughulikia tatizo lenyewe na athari zake sasa na siku za usoni kwa uthabiti mkubwa, huku akiwataka wananchi waendelee na imani na Jeshi lao.
Milipuko hiyo imesababisha maghala 23 kuteketea kabisa na majengo kadhaa ya shughuli mbalimbali kikosini hapo kuharibika kwa viwango mbalimbali.
Aidha mabweni mawili ya kuishi wanajeshi nayo yaliteketea na risasi na mabomu mengi, silaha na magari kadhaa nayo yameharibiwa na mengine kuteketea na kusababisha hasara kubwa kwa jeshi.
Mbali na hasara hiyo, Rais Kikwete alisema wananchi pia wameathirika kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyumba kadhaa za kuishi na majengo ya huduma za jamii nayo kuharibika kwa mabomu yaliyoangukia humo.
No comments:
Post a Comment