.

.

.

.

Tuesday, April 26, 2011

AJALI YA MOTO WA MAFUTA MANYONI

IDADI ya watu waliokufa kutokana na ajali ya lori la mafuta kugonga kichwa cha treni, kisha kulipuka na kuteketea kwa moto wilayani Manyoni mkoani Singida, imeongezeka hadi kufikia 16.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka watu sita walioripotiwa hapo awali baada ya askari Polisi na baadhi ya raia waliokuwa wamelazwa hospitalini Dodoma, Manyoni na Itigi kwa matibabu kufariki dunia juzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Celina Kaluba alifafanua kuwa hadi kufikia sasa vifo vya askari vimefikia sita na raia 10 huku majeruhi 21 wakiendelea kutibiwa katika Hospitali ya Misheni Itigi na Dodoma.

Wakati idadi ya vifo vya ajali hiyo ikiongezeka kila kukicha, baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Manyoni wanataka ufanyike uchunguzi wa kina juu ya askari Polisi na hatua zichukuliwe dhidi yao kwa madai kuwa wao ndio walikuwa chanzo cha watu kufa na kujeruhiwa.

Wananchi hao walidai kuwa kitendo cha askari zaidi ya 15 wa Kituo Kidogo cha Manyoni kulundikana kwenye tukio moja kwa kisingizio cha kulinda lori na kuanza kuuza mafuta ndicho kilichosababisha wananchi wengi kukimbilia kununua petroli, hali iliyosababisha vurugu kabla ya tangi kulipuka moto.

Hata hivyo, Kamanda Kaluba alisema iwapo kuna mwananchi mwenye ushahidi wa kutosha, aupeleke ofisini kwake ili uchunguzi ufanyike na askari waliosalia wachukuliwe hatua baada ya kupona majeraha.

Ajali hiyo ilitokea Aprili 10, mwaka huu saa 2 usiku mjini Manyoni katika eneo la mzunguko wa Barabara Kuu ya Singida - Dodoma baada ya lori la mafuta kugonga kichwa cha treni.

Kutokana na tangi la lori hilo lililokuwa limebeba lita 40,000 za petroli kupasuka na kuanza kuvuja, wananchi walianza kuchota mafuta hayo kabla ya kulipuka moto na kusababisha vifo na majeruhi.

No comments:

Post a Comment