.

.

.

.

Thursday, April 07, 2011

SUSAN MASHIBE MWANAMKE WA SHOKA TANZANIA


ULE usemi “usitathmini kitabu kwa kuangalia jalada lake ” una maana kubwa unapomzungumzia Susan Mashibe.

Mashibe ni Rubani, Mhandisi wa masuala ya ndege na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni mbili zinazoshughulika na masuala ya anga, lakini unapokutana naye kwa mara ya kwanza huwezi kuamini kama mwanadada huyo ana sifa hizo ndio maana nikakumbuka ule usemi, ‘usitathmini kitabu kwa kuangalia jalada lake.’

Kuthibitisha uwezo wake mkubwa katika fani hiyo, hivi karibuni Mashibe alichaguliwa na Taasisi ya World Economic Forum (WEF) kuingia katika kundi dogo la heshima la vijana waliothibitisha vipaji vya uongozi la Viongozi Vijana Duniani (Young Global Leader- YGL)) kwa mwaka huu wa 2011.

Sambamba na Susan, Mtanzania mwingine Elsie Kanza, Mshauri wa Uchumi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete amechaguliwa na taasisi hiyo pia kuingia katika kundi hilo.

Mashibe na Kanza walichaguliwa kutoka miongoni mwa viongozi vijana 5,000 waliopendekezwa kutoka duniani pote na hatimaye kupitishwa katika mchujo na kuchaguliwa kwenye mchujo mkali na Kamati Maalumu chini ya uenyekiti wa Malkia Rania Al Abdullah wa Ufalme wa Hashemite wa Jordan.

Susan ndiye Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Kampuni ya TanJet, kampuni ya ya kimataifa na ya kwanza ya aina yake nchini inayoshughulikia masuala ya kiufundi katika ndege binafsi, za biashara na hata za kidiplomasia.

TanJet imebadilisha namna biashara ya huduma ya anga inavyoweza kufanya kazi Afrika Mshariki na miongoni mwa wateja wake ni viongozi wa nchi mbalimbali, wafalme, watendaji, watu maarufu na ndege za kijeshi.

Mwanadada huyu pia anamiliki kampuni nyingine inayojulikana kama Kilimanjaro Aviation Logistic Center, ambayo inashughulikia taratibu za utuaji na urukaji wa ndege binafsi katika Bara la Afrika.

Aidha, ameanzisha Huduma ya Matengenezo na Ukarabati wa Ndege Kilimanjaro kwa lengo la kutoa huduma za kisasa, yenye kiwango na salama katika usafiri wa anga wa jumla na ushirika katika eneo la Afrika.

Lakini pia Susan ndiye mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki mwenye Cheti cha Rubani cha FAA na Mhandisi Matengenezo wa Ndege. Tangu kuanzisha TanJet mwaka 2003, Mashibe ametunukiwa Tuzo mbalimbali ikiwemo ya Askofu Desmond Tutu ya mwaka 2009 na ile ya Mwanamke Mjasiriamali mwenye Mafanikio ya mwaka 2009.

Susan anajisikiaje kwa kuwa mtu pekee nchini ambaye ni Rubani na Mhandisi wa Ndege? Hasiti kutoa maoni yake kwani anasema “ najisikia kawaida tu. Sipendi sifa hizi zote…ninachotaka ni kuhamasisha vijana kupitia hadithi yangu ili nao watimize ndoto zao na wasikubali kitu chochote kiwakatishe tamaa.”

Ndoto ya Susan ya kutaka kurusha ndege haikuanza wakati akiwa chuoni la hasha! bali akiwa na umri wa miaka minne tu ndipo alipogundua sehemu inayomfaa ni kwenye `mawingu’. Anasema,“ nilizoea kuwaona wazazi wangu na ndugu zangu wakipanda ndege na kuondoka, wakiniacha.

Wakati huo tulikuwa tukikaa Kigoma na walikuwa wakirudi Dar es Salaam, na niliachwa na bibi. “Nilipokuwa nikiangalia ndege ikiondoka nikawa nafikiria kama ningekuwa najua kurusha ndege nisingeachwa tena,” anasema Susan ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto sita.

Wakati huo wote, Susan alikuwa na shauku kufahamu ni kitu gani cha kufanya ili mtu awe rubani, na kufahamu namna ndege inavyofanya kazi. Anaendelea kusema kuwa, “bado nakumbuka hisia nilizopata nilipoona Ndege ya Shirika la Ndege ya Uingereza aina ya Boeing 737 kwa mara ya kwanza, nilikosa maneno ya kusema, nilikuwa sijaona kitu kizuri na kikubwa kama kile, lakini kilichonivutia zaidi ni namna ndege inavyoanza kuruka.”

Hisia alizopata Susan ziligeuka kuwa mapenzi na kitu cha kuvutia ambavyo vilimtawala binti huyo tangu akiwa mdogo. Mapenzi yake yalitimizwa zaidi pale mjomba wake alipompeleka kwenda kutembea uwanja wa ndege wakati alipokwenda Dar es Salaam kumtembelea akiwa na umri wa miaka 10.

Kila mtu katika familia yake alifahamu malengo ya binti huyo. Kwa hiyo haikuwa kazi ngumu kwa Susan kumshawishi baba kubariki kazi aliyoichagua baada ya kumaliza Kidato cha Nne. “Nilichaguliwa kujiunga na ualimu, lakini baba aliyekuwa mfanyakazi wa umma aliniuliza nataka kufanya nini. Nikamwambia nataka kuwa Rubani, kisha akaniambia timiza ndoto yako.”

Hivyo kweli Susan ametimiza ndoto yake. Mwaka 1993 alianza kozi ya Uhandisi wa Ndege katika Chuo cha South Western Michigan nchini Marekani ambapo dada yake alikuwa akiishi. Baba yake alimshauri kuchukua kozi hiyo nchini Marekani na alilazimika pia kujifunza lugha ya Kiingereza.

“Niliambiwa siwezi kuwa rubani kama sizungumzi Kiingereza kwa sababu nitatakiwa kuwasiliana na mnara wa kuongozea ndege,” anasema. Hata hivyo, mwaka 1995 mambo yalikuwa magumu baada ya familia yake nyumbani Tanzania kusema haiwezi kumsaidia kielimu kutokana na matatizo ya kifedha.

“Kwa muda nilifikiria ndoto yangu imekufa…nilipoteza matumaini, hamu ya kula na matokeo yake niliumwa.” “Nililazwa hospitalini na wakalazimika kunirudisha nyumbani ili nipate nguvu, jambo ambalo nilifanya. Lakini nikiwa nyumbani nilitafuta ufumbuzi wa muda mrefu kuwa kuanzia sasa sitamtegemea mtu ila mimi mwenyewe, niliamua nitarudi kumaliza shule na nitarusha ndege mwenyewe.”

Hicho ndicho alichofanya. Kwa namna fulani alirudia hatua zake na kurudi shule na alihitimu mwaka 1996. Mwajiri wake wa kwanza ilikuwa Kampuni ya Duncan Aviation, iliyokuwa mjini Michigan, Marekani. Susan alianza kazi ya ukaguzi mkubwa katika ndege kadhaa za kibiashara.

“Nilianza masomo ya kurusha ndege katika Chuo Kikuu cha Western Michigan, nikisimamia zaidi katika ndege. Ilikuwa gharama kubwa, na nililazimika kufanya kazi saa nyingi usiku ili niweze kuhudhuria darasa, “ anasema.

Lakini bahati nzuri alikuwa akichukua masomo katika kampuni yake kwa hiyo alilipa nusu ya ada, faida ambayo mwajiri alikuwa akitoa kwa wafanyakazi wake. Mwaka 2002, Susan alipata cheti cha kutambuliwa kufanya kazi katika ndege za biashara, baada ya kumaliza Shahada ya Kwanza ya Utawala wa Mambo ya Anga.

Hata hivyo, maisha yalianza kuwa magumu kwa yeyote aliyeko katika biashara ya ndege kwa sababu ya tukio la mashambulizi ya kigaidi Septemba 11, 2001 nchini Marekani. “Baada ya tukio la Septemba 11, mashirika ya ndege yalipata misukosuko, watu walikosa huduma.

Ilikuwa kazi ngumu, baadhi ya kampuni zilifungwa, kwa hiyo nikaamua nyumbani ndipo natakiwa kuwepo,” anasema. Susan alishajinyima sana na kuweka akiba ya kutosha kurudi nayo nyumbani kwa ajili ya kuanzisha biashara yake.

Kwanza alifikiria kutafuta ajira, lakini kampuni nyumbani Tanzania zilisema elimu yake iko juu sana. Hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kutumia akiba yake na kukodi chumba chenye ukubwa wa mita za mraba 13 tu katika Uwanja wa Ndege ambapo alifungua kampuni yake Julai 1, 2007.

“Kila mtu alidharau uamuzi wangu, wakiniambia muda wa miezi mitatu tu nitakuwa nimefunga ofisi, lakini nipo mpaka leo,” anasema na kueleza namna biashara yake inavyolipa. Mteja wake wa kwanza alikuja siku 20 baada ya kufungua biashara yake na alikuwa Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye alifika kutembelea Tanzania.

Washirika wake walioko Afrika Kusini walimuunganisha na kazi ya kuhudumia ndege ya Zuma. Ilikuwa ni hatua kubwa kwake kupata tenda hiyo ya kusimamia ndege zote zilizopo chini ya Ubalozi wa Marekani.

Wakati akifurahia mafanikio hayo makubwa, Susan anasema furaha yake ilikuwa alipoweza kulipa kodi inayofikia kiasi cha Sh milioni 500 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ulikuwa mchango mkubwa uliowashtua wengi. Kama ilivyo kwa wanawake wengi wanapofanya kazi zilizotawaliwa na wanaume zaidi naye amekumbana na vikwazo.

Baadhi ya watu walidharau kwa kumuangalia tu. Anakumbuka aliwahi kuzuiwa kuingia katika ndege ya kidiplomasia kwa sababu walinzi walidhani hana shughuli ya kumuingiza humo. Lakini baadaye walishtuka walipobaini kuwa mwanadada huyo ndio alipewa jukumu la kusimamia ndege hiyo.

“Mimi ni mwanamke, navaa viatu virefu, napaka vipodozi na mambo mengine kama hayo, kwa hiyo rubani anapoangalia na kuona mimi ndiye ninafanya kazi ya kuhudumia ndege yao hushtuka na kudhani sina uwezo huo, wengine hunisimamia ninapofanya kazi, lakini sura zao hubadilika wanapobaini ninachoweza kufanya,” anasema.

Huyo ndiye Susan Mashibe, Rubani na Mhandisi wa Ndege mwenye umri wa miaka 37 ambaye baada ya kujichimbia Marekani akisoma na kupata ujuzi kuhusiana na urubani na uhandisi wa ndege, ameweza kutimiza ndoto yake ya utoto na kukataa kuruhusu vikwazo na kukatishwa tamaa.

CHANZO :HABARI LEO

No comments:

Post a Comment