.

.

.

.

Monday, May 09, 2011

MAGUFULI KIBOKO YA WAKANDARASI WA BARABARA


WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli, amegeuka mbogo kwa wakandarasi wanaojenga barabara ya Kilwa, huku akisusa kupokea barabara hiyo kutokana na kuwa chini ya kiwango iliyojengwa kwa msaada wa serikali ya Japan.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 10 kuanzia Bendera tatu hadi Zakhiem ilijengwa na Kampuni ya Kajima kutoka Japan, Dk Magufuli alisema kukutokana na kuwa chini ya kiwango, serikali haiwezi kuipokea hata kama ni msaada.

Pia, Dk Magufuli alitoa siku kumi kwa Kampuni ya Chico kutoka China, kuanza kazi ya ujenzi wa kilomita 1.5, kutoka Zakhim hadi Tanita, vinginevyo serikali itafuta zabuni hiyo na kampuni italipa fidia na kufungiwa kufanya kazi nchini.Waziri Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza jana kwenye barabara ya barabara Kilwa, Mandela na Ndundu-Somanga.

“Haiwezekani kupokea kitu kisicho na ubora eti kwa sababu ni msaada, hiyo haiwezekani. Tutaandikia barua Serikali ya Japan kueleza fedha za walipakodi wao zimefanyiwa usanii na mhandisi na mshauri wa Japan tofauti na lengo lililokusudiwa,” alisema Dk Magufuli.

Kuhusu Kampuni ya Chico, Dk Magufuli alisema kinachoonekana ni wizi kutokana na kusaini mkataba tangu mwaka jana na kwamba, tayari imelipa Sh1.27 bilioni kama malipo ya awali.“Huu ni wizi amesaini mkataba tangu Novemba mwaka jana na amelipwa Sh1.27 bilioni za awali, lakini hadi dakika hii hakuna hata kifaa kimoja cha kufanya kazi kilichopo eneo la kazi,” alisema dk Magufuli akionekana kuchukia.

Kwa upande wa barabara ya Ndundu- Somanga, Waziri Magufuli alitoa miezi mitano kwa Kampuni ya Kharafi ya Kuwait, inayojenga barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 60 kukamilisha kazi hiyo, vinginevyo atanyang’anywa kazi hiyo.

Dk Magufuli alisema ucheleweshaji miradi hiyo inasababishwa na Makao Makuu ya Wakala wa barabara nchini (Tanroads), kutaka kusimamia miradi yote nchini.Alimwagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, kuwashirikisha wakandarasi wa mikoa na wilaya kwenye kazi zinazofanyika maeneo yao, ili wakishindwa kuwajibika wafukuzwe kazi sambamba na kufikishwa mahakamani kwa uzembe.


No comments:

Post a Comment