MTANDAO wa Kigaidi wa al-Qaeda umethibitisha kwamba kiongozi wake mkuu, Osama bin Laden ameuawa, lakini, wakasisitiza kuwa watalipiza kisasi.Taarifa iliyosambazwa jana na washirika wa mtandao huo na taarifa ya wanaharakati wenye kufuata sera za kigaidi, zimeeleza kwamba hawatakubali damu ya kiongozi wao imwagike hivihivi tu.Walionya kuwa ni lazima watalipiza kisasi kwa kuzidisha mipango ya mashambulizi dhidi ya Marekani na washirika wake na kwamba furaha ya sasa kuhusu kifo cha Osama, “itageuka kuwa maombolezo makubwa”.
Walisema kuwa kifo cha Osama kitakuwa sababu ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Marekani na mkakati wa mapinduzi Pakistani.
Katika taarifa hiyo, al-Qaeda wameahidi kwamba watatoa maelekezo ya Osama yaliyorekodiwa wiki moja kabla ya kuuawa kwake."(Damu ya Osama) itaendelea kudumu na kwa uwezo wa Mungu aliye mkuu wa yote itakuwa ni kichocheo cha kuwafukuza Wamarekani na mawakala wao na tutawafuata kokote ndani na nje ya nchi zao,” ilieleza taarifa hiyo ya al-Qaeda.
“Furaha yao itageuka kuwa maombolezo na watatoa machozi yaliyochanganyika na damu. Tunataka Waislamu wa Pakistani ambao kwenye ardhi yao, Osama ameuawa kuanzisha vuguvugu la uasi.”
Taarifa hiyo iliyoonyesha kuandikwa Jumanne wiki hii haikuwa na uthibitisho wa moja kwa moja kuwa imeandaliwa na viongozi wa al-Qaeda.
Hata hivyo, iliingizwa kwenye mtandao wa kompyuta kupitia njia na tovuti ambazo zimekuwa ni kawaida kutumiwa na magaidi kusambaza taarifa zao.Taarifa zinaeleza kwamba watu wengi walihamasika kufanya maandamano Pakistani ya kupinga kitendo cha Marekani kuingia katika ardhi yao kwa nguvu na kufanya mauaji.Walisema kwamba makamanda wa kijeshi wa Pakistani walishirikishwa kwenye mkakati huo wa Marekani ingawa serikali ya nchi hiyo imekuwa ikikanusha jambo hilo tangu tukio hilo lilipotokea.
No comments:
Post a Comment