VITA ya kufutwa posho za wabunge na watumishi wengine wa umma, imechukua sura mpya, baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kusema kwamba Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe anaweza kufukuzwa ubunge kwa kutosaini karatasi za mahudhurio.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge baada ya kuahirisha mkutano wa asubuhi, Makinda alisema Zitto anaweza kukumbwa na adhabu hiyo iwapo hatasaini karatasi za mahudhurio ambazo ndizo zinazothibitsha uwepo wa mbunge katika mikutano na vikao vyake.
"Kwa mujibu wa kanuni zetu, asipohudhuria mara tatu anakabiliwa na adhabu tena ya kufukuzwa bunge, hizo ndivyo kanuni zinavyosema." Hata hivyo, Zitto amepuuza kauli hiyo ya Spika akisema kwamba kama ni kwa ajili ya kukataa posho, yuko tayari kufukuzwa bungeni.
"Nitafanya hivyo tuone. Kanuni inasema mikutano mitatu mfululizo na siyo vikao vitatu mfululizo. Nitatumia uzoefu wangu wa siasa za wanafunzi kukwepa mtego wake. Lakini kama anadhani ni sawa kunifukuza ubunge kwa kukataa posho, nipo tayari," alisema Zitto.
Kauli ya Makinda inafuatia msimamo wa Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), kukataa posho za vikao na kwamba kwa kuwa kinachohalalisha yeye kulipwa posho ni karatasi za mahudhurio basi hatasaini karatasi hizo.Zitto alisema juzi mjini Dodoma kuwa, tangu Juni 10, mwaka huu alijibu barua ya Spika akikataa "kushinikizwa kuchukua posho za vikao" na kwamba hatua atakayoichukua ni kutosaini karatasi za mahudhurio katika vikao vyote.
Mahudhurio hayo ndiyo hulalalisha mbunge kupewa posho hizo.
"Kuanzia kikao cha juzi cha Tume ya Mipango, sikusaini na mkitaka nendeni mkaangalie ile orodha na kesho ndani ya Bunge sitasaini ili kuondoa uhalali wa kupewa posho hizo.
Sasa hapo tutaona watanilazimisha kwa njia gani," alisema Zitto.Lakini jana, Makinda alisema mujibu wa sheria malipo yote lazima yapelekwe kwa mbunge mwenyewe na kwamba ofisi yake haitafanya vinginevyo kwa wabunge ambao wamekataa posho hizo.Kanuni 143 (1) ya Bunge inabainisha kuwa kuhudhuria vikao ndiyo wajibu wa kwanza wa kila mbunge na kwamba asipohudhuria mikutano mitatu ya Bunge bila ruhusa ya Spika atapoteza ubunge wake.
Kwa maana hiyo, Zitto anaweza kufukuzwa Bunge ikiwa hatasaini mahudhurio ya vikao vyote vya Mkutano wa Bunge la Bajeti, vikao vya mkutano ujao ambao kwa kawaida huwa wa Oktoba na mkutano wa kwanza wa mwaka 2012.
"Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria Mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake kwa mujibu wa Ibara ya 71 (1) (c) ya Katiba na Spika ataiarifu Tume ya Uchaguzi," inaeleza kanuni hiyo namba 143 (2) ambayo iko chini ya sehemu ya 10 ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007.
No comments:
Post a Comment