.

.

.

.

Thursday, July 14, 2011

ROSTAM AZIZ AACHIA NGAZI CCM


MBUNGE wa Igunga, Bw. Rostam Aziz amekuwa mwanachama wa kwanza wa Chama cha Mapunduzi (CCM) kujivua gamba baada kuachia ngazi nyadhifa zake zote alizonazo kupitia
chama hicho ikiwemo kiti cha Ubunge.

Uamuzi huo umekuja wakati siku 90 zilizotolewa na chama hicho kikiwataka watuhumiwa wa ufisadi wajivue gamba la sivyo wangefukuzwa zikiwa zimetimia, hivyo kusubiri uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM itakayokutaka hivi karibuni.

Hata hivyo, mapema akizungumza na wazee wa Jimbo la Igunga jana, Bw. Aziz alisema amefikia uamuzi huo wa kuachia nafasi zote za uongozi alizopata kwa tiketi ya CCM na uamuzi huo haukutokani wala kumaanisha kukubaliana na shinikizo la utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba.

Alisema hiyo ni dhamira ya dhati ya kuachana na 'siasa uchwara' ili atumie muda wake kushughulika na biashara zake, kwani tangu matukio yanayogusa jina lake yaanze kutokea miezi michache tu baada ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005 imekuwa ikimwathiri kibiashara.

Alisema baada ya kukaa na wanafamilia yake, marafiki na washirika wake wa kibiashara ameona halitakuwa jambo la busara kuendelea kuvutana na viongozi wa chama chake na wanachama wenzake wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.

"Sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara," alisema Bw. Aziz.

Alisema kama ilivyo katika maeneo mbalimbali nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapatikana katika nyanja za elimu, afya, makazi bora na kilimo katika kipindi chote akiwa mbunge wa Igunga kwa miaka 18 wananchi wake wamekuwa na imani kubwa na kuunga mkono kwa dhati naye alijitahidi kwa kadiri alivyoweza kutimiza matarajio ya wananchi wa jimbo hilo.

Alisema miongoni mwa mafanikio makubwa waliyoyafikia kupitia ushirikiano wake na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora lakini leo ndiyo ya kwanza, ina taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.

Alisema katika kipindi chote cha utumishi wake wazee hao walikuwa mhimili muhimu ambao umemwezesha kutimiza wajibu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu akitambua namna ambavyo wamekuwa na imani kubwa juu yake.

Alisema wananchi wa Igunga wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini na matukio mengine ndani ya CCM ambako yeye alikuwa mwanachama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) akiwakilisha Mkoa wa Tabora.

"Nafanya hivyo nikitambua vyema kwamba, kama si nyinyi wazee wangu na wengine wengi ambao hatuko nao hapa leo kwa sababu mbalimbali, ambao mmekuwa na imani kubwa nami nisingeweza kufikia hapa nilipofika sasa," alisema.

Anatambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wake wananchi wa Igunga wamekuwa na imani kubwa na kumuunga mkono kwa dhati, anaamini kwamba kwa upande wake pia amejitahidi kwa kadiri alivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

"Naamini kwamba katika kufuatilia kwenu mtakuwa mmebaini kuwapo kwa matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakitokea huku yakiligusa jina langu na wakati fulani nafasi yangu kama kiongozi wa CCM," alisema.

Alisema alipokuwa katika ziara zake jimboni na wakati mwingine wananchi walipowasiliana naye kwa njia mbalimbali wamekuwa wakionesha kuguswa, kushtushwa na kutaka kujua kulikoni kuhusu mambo hayo yanayotokea naye siku zote amekuwa mwepesi kuwaeleza kuhusu kila kinachotokea ili kuwaondoa hofu.

Bw. Aziz alisema pia kuwa amekuwa akiwahakikishia kwamba masuala yasiyo na msingi hususani yale yanayogusa siasa za kitaifa hayawezi kuondoa katika mstari sahihi wa kuwahudumia wananchi wa Igunga, wakiwamo wazee hao ambao walimwamini na kumtuma kuwawakilisha.

Alisema anaamini na ataendelea kuamini kwamba walifanya uamuzi sahihi wa kuyapuuza matukio hayo kwani mbali ya kuendelea kutimiza malengo mbalimbali yaliyokuwamo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, pia wananchi hao waliendelea kumwamini kwa nafasi yake ya kuwa mwakilishi wao bungeni na hata wamruhusu kubeba jukumu jingine kubwa la kuwa Mjumbe wa NEC aliyewakilisha mkoa wa kihistoria wa Tabora.

'Wazee wangu, nyinyi ndiyo watu mnaolifahamu vyema jimbo letu la Igunga na hakika nyinyi ni sehemu muhimu ya watu wanaojua historia ya kisiasa ya Mkoa wa Tabora kwa miaka mingi hata kabla ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini," alisema Bw. Aziz.

Alisema alifanya kazi ya kuijenga CCM katika mazingira yenye mizizi hasa ya upinzani akiwa mbunge na mjumbe wa NEC kutoka Mkoa wa Tabora haijapata kuwa rahisi na itaendelea kuwa ngumu na ambayo mapambano yake ni makali.

Matunda ya kazi hiyo kubwa yanaonekana pamoja na kuwa kitovu cha kihistoria cha siasa za upinzani, Tabora ndiyo mkoa pekee katika eneo hili ambao unaongozwa na wabunge wote kutoka CCM baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na hata kabla ya hapo.

Alisema ukiacha mafanikio makubwa yaliyopata katika jimbo na wilaya ya Igunga, kuna mambo mengine ya msingi ya kujivunia hivyo kwa moyo wa dhati na unyenyekevu mkubwa anawapongeza kwa namna walivyojitoa kukipigania na kuitetea CCM kwa ari na nguvu ya kipekee.

Alisema anakubaliana na uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ya kuamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha chama kiendelee kuwa pekee kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania wengi.

Dhamira ya mwelekeo huo wa kufanya mabadiliko ya ndani ya CCM yaliyotangazwa na Mwenyekiti Rais Kikwete wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma hotuba yake aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya Kujivua Gamba anaungana nayo.

Alisema hatua ya kwanza ya utekelezaji wa azimio hilo na mwelekeo huo sahihi ilifanyika mjini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya CCM ambacho yeye alikuwa mjumbe.

Wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya CCM ya wakati huo kwa kauli moja walikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa mwenyekiti fursa nzuri ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa chama.

"Wazee wangu, tulifanya hivyo tukionesha kuunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho bado naendelea kuamini kuwa ni mawazo sahihi na yenye mwelekeo thabiti ya Mwenyekiti wetu ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakiakisi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa Oktoba mwaka jana," alisema Aziz.

Alisema ingawa ni kweli Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umekirudisha CCM madarakani kwa kukipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kiwango cha ushindi CCM ilichopata kimeonesha waziwazi dalili za wananchi kupunguza imani yao kwao kulinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005.

"Tungekuwa ni chama cha siasa cha ovyo iwapo tungepuuza kupungua kwa kura za rais kutoka zaidi ya asilimia 80 tulizopata mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 61 mwaka jana kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 20 ya kura katika kipindi cha miaka mitano tu, hasa ikizingatia ukweli kwamba mgombea urais ni mtu yule yule," alisisitiza Bw. Aziz.

Alisema kingekuwa chama cha siasa kilichokosa umakini iwapo wangekaa pasipo kuchukua hatua zozote za kujiimarisha baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kuonesha wazi kukua kwa upinzani ambao umeongeza idadi ya wabunge na madiwani katika pande zote mbili za muungano.

Alisema kwa sababu ya kutambua ukweli kwamba hakuna haki isiyo na wajibu, yeye na wenzake waliokuwa katika Kamati Kuu waliona ulazima, haja na umuhimu wa kukubali kwa kauli moja wito wa kuwataka tujiuzulu ikiwa ni hatua moja ya kujipanga na kukijenga upya chama hicho.

Alisema kilichotokea baada ya kujiuzulu kwao kila aliye ndani na nje ya CCM amekisikia na anakifahamu, chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu mpya, Bw. Wilson Mukama na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali.

Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya CCM, alisema ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu wakiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye.

Mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ambayo naamini Mwenyekiti Kikwete aliianzisha kwa nia njema ilianza kuenezwa ikichukua tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.

Alisema wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Bw. John Chiligati na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.

Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walikuwa wakilengwa na maamuzi hayo, likiwamo la Mbunge wa Igunga.

"Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa kwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya kujivua gamba ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu," alisema Bw. Aziz.

Kauli yake

Wazee wangu, nimetafakari sana na kimsingi nimefikia hatua ya kupima yale ambayo yamekuwa yakisemwa na kuandikwa juu yangu na ambayo kwa mtazamo wangu unaoungwa mkono na wanafamilia yangu, marafiki zangu na washirika wangu wa kibiashara walio ndani na nje ya nchi, naona umefika wakati muafaka wa kuchukua hatua.

Kwa sababu ya kutambua uzito wa hatua ninazokusudia kuzichukua, niliona halitakuwa jambo la hekima hata kidogo iwapo ningefanya hivyo pahala pengine popote bali hapa Igunga mbele ya nyie wazee wangu.

Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.

Wazee wangu, sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara.

Kutokana na ukweli huo na sababu zote hizo basi, kwa moyo wa dhati na kwa nia thabiti, hatua ya kwanza niliyoiona kuwa ninapaswa kuichukua ilikuwa ni hii ya kuitikia wito unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi yangu wa kuamua kukomesha kabisa malumbano na mivutano isiyo na manufaa kwangu binafsi, kwa viongozi wa chama changu na chama chenyewe.

Msukumo huo si mwingine bali ni ule wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu nisingelikuwa nazo.

Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.

Waandamana mitaani, wazirai

Mara baada ya kutoa tamko hilo hilo, vurugu ziliibuka mjini hapa baada ya vijana wenye mabango kujitokeza wakidai wanapinga kujiuzulu kwake, wakitaka kumshinikiza aendelee na nyadhifa zake kwa kuwa bado walikuwa wanampenda.

Wengine walizirai na kupelekwa hospitali, akiwamo katibu Mwenezi wa kata ya Chabutwa, Bw. Athuman Mihayo, Mwenyekiti wa UV-CCM Nzega, Bw. Daud Ng'onge na wanachama wawili, Zainab Athumani na Catherine Mabula.

Katika purukushani hiyo, mkazi mmoja wa Igunga aliyepiga simu chumba cha habari Majira na kujitambulisha kama Mahame Ahmed alidai kukamatwa na polisi na kunyang'anywa bango lake lilieleza hisia tofauti za wenzake.

"Mimi nilikuwa na mawazo tofauti, wengine waliletwa wakiwa na mabango ya kuonesha wanapinga uamuzi wake, mimi nikaonesha bango langu likiwa na ujumbe unaosema 'Tanzania bila Rostam inawezekana; na Igunga bila Rostam inawezekana'.

"Ninacholalamika, ni kwamba sikutendewa haki. Hao wengine wameruhusiwa kuonesha hisia zao, mimi nimechukuliwa, nikahojiwa na kuachiwa baadaye lakini bango langu wamelichukua polisi," alisema.

Maoni ya Wabunge

Mbunge wa Simanjiro, Bw. Christopher Ole Sendeka alimpongeza Bw. Aziz akisema kuwa ameonesha ujasiri na nidhamu kwa chama chake.

Naye Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuachia ngazi wa Bw. Aziz ni ishara kuwa yale yaliyosemwa na chama chake, CHADEMA kilipota watuhumiwa 11 wa ufisadi yametimia, kwa mmoja wao kuachia ngazi, bado wenzake 10
.

No comments:

Post a Comment