.

.

.

.

Friday, September 09, 2011

MOTO WA TIBAIJUKA WAANZA KUWAKA


Fidelis Butahe
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ameanza kuchukua hatua kali, kukabiliana na uvamizi, uporaji na rushwa katika sekta ya ardhi nchini na kisha kutangaza kufuta hati za viwanja 42 jijini Dar es Salaam.

Mbali na kufuta hati hizo, Profesa Tibaijuka pia ametangaza kwamba halmashauri za majiji, Manispaa na miji nchini ambazo zimekithiri kwa migogoro ya ardhi, zitanyang’anywa madaraka yake na kurudishwa chini ya wizara yake.

Profesa Tibaijuka alitangaza mpango huo jijini Dar es Salaam jana huku akisisitiza: “Tunaanza kwa kasi zaidi na nguvu zaidi na kurejesha hali salama katika miji yetu”.

Hati zafutwa Dar
Akizungumzia hali ilivyo katika Jiji la Dares Salaam, Profesa Tibaijuka alisema katika wilaya zake tatu, wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na maeneo ya wazi 88 yaliyovamiwa kati ya 110 yaliyochunguzwa.

Waziri Tibaijuka alisema; “Kwa mujibu wa sheria za nchi, mtu yeyote haruhusiwi kufanya maendeleo mjini bila kibali cha maandishi kutoka mamlaka za mipango miji”.

Alisema hati za viwanja zilizofutwa mpaka sasa ni 42 ambazo viwanja 12 vipo eneo la Mikocheni mabwawa ya maji na viwanja 30 vipo Mbezi.

Tibaijuka alisema eneo la bwawa la maji lililopo Mikocheni limevamiwa na kupimwa viwanja 12(namba 1116-1127). Alisisitiza kuwa viwanja hivyo ni batili na vimefutwa.

“Hivi sasa hakuna atakayeweza kuishi kwa ujanjaujanja jijini Dar es Salaam, kama una hati yako, lakini una mashaka nayo nenda kamuone Kamishna wa Ardhi mapema,” alisema Tibaijuka,

Aliongeza: “ Kama una kiwanja umeshindwa kukiendeleza kwa miaka mitatu kitachukuliwa, ila kwa sasa Wizara ya Ardhi haitapima viwanja mpaka kuwe na barabara ili kuwezesha maeneo hayo kuwa na huduma muhimu za jamii jambo ambalo litawafanya wananchi kujenga nyumba kwa wingi,”.

Profesa Tibaijuka alisema mpango huo umebarikiwa na Rais Jakaya Kikwete na kwamba, amemuhakikishia kuwa kila kitu lazima kitatekelezwa kwa kufuata sheria.

“Hati miliki zote zilizotolewa kinyume na sheria zitafutwa kama ilivyofanyika katika eneo la Ocean Road, Palm Beach, Jangwani Beach na Mbezi Beach,” alisema Tibaijuka.

Tibaijuka ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT), alisema ametoka katika shirika hilo kwa lengo la kufanya kazi katika wizara hiyo, hivyo kitendo cha kukithiri kwa migogoro ya ardhi kinamnyima nafasi ya kutekeleza majukumu yake.

Alisema kwamba, uchunguzi uliofanywa katika maeneo ya wazi 153 ya manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam na Kamati iliyoundwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, William Lukuvi, ulibaini kuwapo kwa udanganyifu mkubwa.

“Maeneo 88 sawa na asilimia 80 kati ya maeneo 110 ya wazi yaliyopo Manipsaa ya Kinondoni yamevamiwa,” alisema Tibaijuka.

Alisema katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala maeneo ya wazi yaliyokaguliwa ni 30 ambapo kati ya hayo 11 yamevamiwa sawa na asilimia 37.

“Manispaa ya Temeke inaonekana kuwa na asilimia ndogo ya uvamizi ambapo yalibainika maeneo matano sawa na asilimia 30 ya maeneo 14 yaliyotembelewa,” alisema Tibaijuka.

Waziri Tibaijuka alisema wananchi wanaoishi katika maeneo ya wazi na kando ya Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam, wanatakiwa kuondoka.

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Goodluck ole Madeye, alisema jijini Dar es Slaam eneo la Kawe ndio linaongoza kwa kuwagawa maeneo kiholela.

“Haturidhiki na utendaji huo mfano ni Mto Kawe ambao hivi karibuni ulivamiwa huku uongozi wa Serikali ya Mtaa ukilifumbia macho suala hilo,” alisema Ole Madeye.

No comments:

Post a Comment