.

.

.

.

Wednesday, October 12, 2011

BARAZA LA VIONGOZI WA DINI LAZINDULIWA

RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi amesema Watanzania wananuka kwa dawa za kulevya na kwamba wamesababisha viongozi wakuu wa nchi kusachiwa sawa na raia wengine wakati wanaposafiri nchi za nje.

Rais huyo, alisema kadhia hiyo imesababishwa na baadhi ya viongozi wa dini na watu wengine wasio waaminifu kutumia vibaya nembo za taasisi za dini kusafirisha dawa za kulevya nchi za nje.Hayo aliyaeleza jana jijini Dar es salaam wakati akizindua baraza la viongozi wa dini la kupambana na athari za dawa za kulevya.

Akisimulia mkasa uliomkuta wakati alipokuwa Rais wa Serikali ya awamu ya pili ya Tanzania, Mwinyi alisema siku moja alioposafiri kuelekea Ujerumani akiwa na ujumbe wa watu takribani 10, alisachiwa.

“Wakati wa zamu yangu ya kugongewa muhuri katika pasi ya kusafiria nilipojieleza kuwa natokea Tanzania ghafla mtu wa ukaguzi akanisachi kila sehemu, lakini hakuridhika akaniambia niingie katika chumba maalumu cha kusachia abiria.

“Nilipoingia humo akaniamuru nivue viatu na koti, lakini wakati anafanya hivyo mmoja wa walinzi wangu akamweleza yule aliyekuwa akinikagua kuwa ni kiongozi wa watu, lakini yule mkaguzi akajibu kuwa sijali, nikavua akanikagua tena mpaka aliporidhika,’’ alifafanua Mwinyi.

Mwinyi alisema alipojiuliza kwanini alikaguliwa licha ya kuwa ni kiongozi, alibaini kwamba wakaguzi walimtilia shaka kwa kuwa alikuwa ameshika tasbil.

“Nilipojiangalia nikajikuta nimeshika tasbil nikagundua kwamba watu wa dini kutoka Tanzania, wanapitisha dawa za kulevya katika nchi hizo kwa kujificha kupitia mavazi na tasbil, tukio like lilinifedhehesha, lakini sikumkasirikia kwa kuwa alifanya kazi yake.

“Napenda kusema kuwa wachungaji wacha Mungu wanatumiwa kuficha vidonge vya ulevi na kadri tunavyovaa nguo nyingi ndivyo tunavyohisiwa zaidi,” alisema Mwinyi.Baraza hilo lina wajumbe 14 na wajumbe saba na limedhaminiwa na Tume ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Pia baraza hilo limefadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani kupitia Centers for Disease Control and Prevention (CDC) pamoja na taasisi ya American International Health Alliance (AIHA).


No comments:

Post a Comment