Katika hatua nyingine, kundi la viongozi na marafiki wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) lililopo Dodoma, jana lilitaharuki baada ya kupokea taarifa za kurushiwa makombora, huku Rais Kikwete akiwazodoa kwa kuwaambia: ‘Msitutishe,’ ishara ya kukerwa na taarifa kwamba vijana hao walitishia kuhamia Chadema ikiwa Umoja wao utavunjwa.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao cha CC kilichomalizika juzi usiku zinasema, ajenda kuhusu UVCCM ni kama haikuwa rasmi lakini baada ya kuibuliwa na Nape ilisababisha Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Benno Malisa kusakamwa ipasavyo na kutishwa kwamba hatima yake kisiasa inaweza kuwa mbaya.
“Yule bwana mdogo (Benno) alipata wakati mgumu sana, maana wale wazee walimshughulikia ipasavyo, alijaribu kujitetea lakini haikusaidia, kweli nilimwonea huruma sana maana hakuwa na mtetezi mle ndani,” kilisema chanzo kingine kutoka ndani ya CC.
Taarifa hizo ziliendelea kudai kuwa Nape aliomba kikao hicho kimpe majibu ya kutoa kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa wakimwuliza kuhusu suala hilo ambalo alisema hakuwa na majibu.
“Nimeambiwa UVCCM viongozi wa mikoa na baadhi ya wilaya wako hapa, mwenyekiti naomba nipate majibu nisaidiwe katika hili, kama ni Baraza Kuu linakutana nifahamu na kama kuna mkutano mwingine nijue pia, lakini hali hii inaniweka katika wakati mgumu mimi kama mwenezi,” alinukuliwa Nape na chanzo chetu ndani ya CC.
Maelezo hayo yalisababisha Benno kusimama kutoa utetezi ambao hata hivyo, haukusikilizwa na hapo wajumbe wawili, Mawaziri, William Lukuvi na Steven Wassira kila mmoja kwa wakati wake, aliushambulia umoja huo.
Inadaiwa kuwa Rais Kikwete ndiye aliyegongelea msumari wa mwisho pale aliponukuliwa na mtoa taarifa wetu akisema: “Mnataka kututisha, msitutishe hata kidogo maana nasikia kwamba mnataka kwenda Chadema, nendeni hata kesho, au mnasubiri tuuvunje ndiyo muondoke!”
Kadhalika Rais alinukuliwa akihoji vijana hao walikopata fedha zinazowawezesha kukaa hapa kwa muda wote huku akiwakumbusha kwamba CCM hakiwezi kuyumba ikiwa kitawatimua kwani kimewahi kufanya hivyo kwa viongozi wa ngazi za juu.
Pamoja na hali hiyo, viongozi wengi wa UVCCM wa mikoa na wilaya mbalimbali nchini bado wapo Dodoma na baadhi yao walisema huenda wakatoa tamko baada ya kikao cha NEC kumalizika.
No comments:
Post a Comment