.

.

.

.

Thursday, January 12, 2012

MCHUJO KIDATO CHA PILI WAREJEA MWAKA HUU


Fredy Azzah na Boniface Meena
 SERIKALI imerejesha mchujo kwenye mtihani wa kidato cha pili, ikisema kuanzia mwaka huu wanafunzi watakaopata wastani wa chini ya alama 30 katika masomo yote, watalazimika kurudia darasa.Katika uamuzi huo, ada ya mtihani wa kidato cha pili imerejeshwa na itaendelea kuwa Sh10,000 na ada kwa mitihani ya kidato cha nne na sita ni Sh35,000.
Tamko hilo la Serikali lilitolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo akisema Serikali imerudisha makali ya mtihani wa kidato cha pili baada ya  kuona ufaulu wa wanafunzi katika kidato cha nne unashuka kwa asilimia kubwa. “Matokeo ya mtihani wa kidato cha pili hupewa uzito mkubwa katika matokeo ya jumla ya mtihani wa kidato cha nne kama sehemu ya upimaji endelevu,” alisema na kuongeza:

“Hivyo, kuanzia mwaka huu mwanafunzi atakayepata wastani wa chini ya asilimia 30 katika mtihani wa kidato cha pili hataruhusiwa kuendelea na kidato cha tatu.” “Mwanafunzi huyo atatakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili na fursa hii itatolewa mara moja tu. Atakayekariri kidato cha pili na kushindwa kufikia wastani wa asilimia 30 ataondolewa katika mfumo rasmi wa elimu.”

Waziri huyo alisema mtihani wa kidato cha pili ulianzishwa mwaka 1984 kwa madhumuni ya kutathmini maendeleo ya wanafunzi baada ya miaka miwili ya elimu ya sekondari. “Mtihani huu ni tathmini ya kati inayopima kiwango cha maarifa na ujuzi alioupata mwanafunzi kutokana na masomo aliyojifunza katika kidato cha kwanza na cha pili,” alisema na kuongeza:

“Mtihani wa kidato cha pili ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa wadau wote wakiwemo wanafunzi, walimu na wazazi wanawajibika ipasavyo katika utoaji wa elimu ambapo kwa kufanya hivyo, tutapata wanafunzi wazuri na kuweka misingi bora ya wanafunzi katika kujifunza.”

1 comment:

  1. serikali haina maana mara iondoe mtahani mara ilete tunataka msimamo wa serikali

    ReplyDelete