.

.

.

.

Friday, March 23, 2012

KOTA ZA GEREZANI KUVUNJWA !!!

NYUMBA 106 zilizopo katika eneo la Gerezani Kota- Kariakoo jijini Dar es Salaam zitaanza kubomolewa leo alfajiri baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutupilia mbali pingamizi la madai yaliyokuwa yamewasilishwa na wakazi wa eneo hilo tangu 2008. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuondoka mapema na kuokoa mali zao kabla ya kubomolewa nyumba zao ili kupisha ujenzi wa kituo cha Mradi wa Mabasi ya Kasi (DART). Alisema kuwa awali Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilitayarisha mpango wa uendelezaji upya wa eneo hilo lililokuwa likimilikiwa na Shirika la Reli na Mamlaka ya Bandari na baada ya mpango huo kukamilika, ulitangazwa kwenye Gazeti la Serikali la Januari 25, 2002. “Katika juhudi za Serikali kufanikisha ujenzi wa kituo kwenye eneo hilo Aprili 8, 2008 ilitangaza kutwaliwa rasmi kwa eneo hilo kwa manufaa ya umma na kupangwa kujengwa kituo cha mabasi ya Dart, ilitangaza mwenye malalamiko, pingamizi au madai ajitokeze lakini hapakuwa na aliyejitokeza,” alisema. Alisema kutokana na hilo ilifanyika tahmini ya eneo hilo na zikatolewa Sh bilioni 2.7 kwenda Wakala wa Majengo (TBA) na familia 34 kati ya hizo 106 ndiyo zilizojitokeza kuchukua fidia zao lakini nyingine 72 ziligoma na kuungana kufungua kesi hiyo mahakamani. Alisema tangu kipindi hicho kesi hiyo imekuwa ikisikilizwa kwa kusuasua na wiki iliyopita Mahakama ilitupilia mbali shauri hilo lakini wakati Serikali ikijiandaa kuanza kutekeleza amri ya Mahakama ya kuwahamisha watu hao, wananchi hao walipeleka pingamizi lingine mahakamani Jumatatu wiki hii. “Pingamizi hili lilitupiliwa mbali juzi lakini baadaye wakapeleka tena na jana limetupiliwa mbali hivyo tunawataka wahame na ubomoaji utaanza alfajiri na utafanywa na Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart,” alisema.

No comments:

Post a Comment