.

.

.

.

Thursday, March 22, 2012

MESSI AWEKA REKODI MPYA

BARCELONA, Hispania

  Juzi LIONEL Messi alifunga mara tatu na kufikisha mabao 234 tangu ajiunge Barcelona na kuvunja rekodi ya mabao iliyowekwa miaka 60 iliyopita na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Cesar Rodriguez (57).Messi (24) alipachika mabao hayo katika mechi ya Ligi Kuu Hispania dhidi ya Granada, ambapo Barcelona ilishinda 5-3 na hivyo kuipiku rekodi ya muda mrefu ya mabao 232 iliyowekwa na Rodriguez. Nyota huyo wa Argentina aliyecheza Barcelona kwa mara ya kwanza mwaka 2004, aliifikia rekodi ya Cesar kwa kufunga bao la kwanza kwa guu lake la kushoto katika dakika ya 17, kisha akafunga lingine dakika ya 67 na kuifanya Barca kuwa mbele kwa mabao 3-2. Aliongeza bao lake la tatu kwenye mchezo huo lililokamalisha kuvunja rekodi hiyo katika dakika ya 86 na hivyo kufikisha mabao 54 kwa msimu huu. "Kipa wa Barcelona, Victor Valdez alisema,"amethibitisha kwamba hizi ni zama zake." Kwa jumla, Messi ameshapachika kwenye kamba mabao 234 katika mechi 314 alizocheza Barcelona. Messi, mchezaji bora mara tatu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) , amefunga mara 17 katika mechi saba zilizopita na anaongoza orodha ya wafungaji bora Hispania kwa kufikisha mabao 34, mawili mbele ya mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo. Katika mechi 45 alizocheza msimu huu, amefunga mabao 54.'Hat trick' ya Messi usiku wa kuamkia juzi, ilikuwa ya 18 tangu alipojiunga Barcelona na kufikisha mabao 154 katika mechi 153 zilizopita. Kana kwamba hiyo haitoshi, mabao matatu aliyofunga juzi ilikuwa ni mara yake ya sita kwa Barcelona msimu huu pekee na hivyo kufikia rekodi kama hiyo iliyowekwa na Ronaldo msimu uliopita. Kwa kiwango kikubwa anachoendelea kukionyesha msimu huu kinaweza kumfikisha hata rekodi ya kufunga mabao 70.Baada ya mechi ya juzi usiku, wachezaji wenzake Messi walimpongeza na kuongea mengi, akiwemo Pique. "Ni changamoto kubwa kuwa katika kizazi kama chake," alisema Pique na maelezo yake kuwekwa kwenye tovuti ya mawasiliano ya Barcelona. "Naamini yeye (Messi) ndiye mchezaji bora zaidi katika historia. "Haijalishi anacheza wapi, kwenye joto, baridi siku zote huonyesha ni kwa kiasi gani yeye bi bora." Andres Iniesta alisema,"ushindi mkubwa, hata kimchezo tunazidi kuongeza pointi. Hongera sana Leo, mfungaji mahiri wa Barca." Kocha wa Barca, Pep Guardiola aliwapongeza wachezaji wake katika mkutano wa baada ya mchezo. "Kuna wachezaji wachache wanaweza kutawala, lakini yeye anatawala. Unaweza kumlinganisha vizuri na Jordan," alisema Guardiola. "Tunaendelea kushuhudia mazuri kila wakati kutoka kwake. "Anafanya yote, na anafanya kila baada ya siku tatu."


 REKODI YA MABAO:
 •2007-08: 16 Magoli 
 •2008-09: 38 
 •2009-10: 47 
 •2010-11: 53 
 •2011-12: 54 mpaka sasa.

No comments:

Post a Comment